Cerca

Vatican News
Biashara haramu ya silaha duniani ni janga kwa Bara la Afrika! Biashara haramu ya silaha duniani ni janga kwa Bara la Afrika!  (AFP or licensors)

Biashara haramu ya silaha duniani ni janga kwa Bara la Afrika!

Utafiti uliofanywa kuhusiana na matumizi ya silaha ndogo ndogo katika kipindi cha miaka mitano, yaani kuanzia mwaka 2012 hadi mwaka 2017, unaonesha kwamba, watu zaidi ya 140, 000 wameuwawa kutokana na matumizi ya silaha za moto!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Biashara haramu ya silaha duniani ni tishio kwa: amani, ustawi, maendeleo, mafao ya wengi na usalama duniani. Lakini, waathirika wakuu ni watu wanaotoka katika nchi maskini zaidi duniani, Bara la Afrika likiwa linashikilia nafasi ya kwanza. Utafiti uliofanywa kuhusiana na matumizi ya silaha ndogo ndogo katika kipindi cha miaka mitano, yaani kuanzia mwaka 2012 hadi mwaka 2017, unaonesha kwamba, watu zaidi ya 140, 000 wameuwawa kutokana na matumizi ya silaha za moto!

Kuna ongezeko kubwa la biashara haramu ya silaha Barani Afrika na mara nyingi silaha hizi zinaishia mikononi mwa makundi ya kigaidi kama vile Boko Haram, Al Qaeda, Ansar dine, pamoja na kikundi cha kigaidi cha Al Shabaab kutoka Somalia.  Kwa sababu hiyo, Vatican inapaza sauti kualika juhudi za pamoja sio tu kutokomeza biashara haramu ya silaha duniani lakini pia kupambana na shughuli zote za uhalifu zinazohusiana na: ugaidi, biashara ya binadamu na utumwa mamboleo mambo ambayo yanadhalilisha utu na heshima ya binadamu! Bwana Matthias Nowak, mtafiti kuhusu madhara ya silaha ndogo ndogo kutoka, Geneva Uswiss anasema, vita na mipasuko ya kijamii inayoendelea nchini Libya imekuza sana biashara haramu ya silaha kusini mwa Jangwa la Sahara.

Watu wana hamu ya kuona kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inadhibiti kwa umakini mkubwa biashara haramu ya silaha duniani, ili kujenga dunia inayosimikwa katika misingi ya haki, amani na utulivu. Mataifa mengi yanaonesha utashi wa kutaka kuwa na udhibiti wa biashara ya silaha duniani, ingawa utashi huu unakwamishwa na baadhi ya mataifa na makampuni makubwa yanayojihusisha na biashara ya silaha duniani. Kuna idadi kubwa sana ya silaha inayosafirishwa kutoka Kaskazini mwa Afrika kwenda kwenye nchi zilizoko Kusini mwa Jangwa la Sahara! Matokeo yake ni watu kutekwa nyara na hata wakati mwingine kutokomea mahali kusikojulikana.

Baba Mtakatifu Francisko daima anasema, amani na utulivu haviwezi kupatikana ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa itashindwa kudhibiti biashara haramu ya silaha duniani pamoja na uhamiaji wa shuruti. Biashara haramu ya silaha duniani inakwamisha juhudi za kutafuta amani na usalama kati ya watu. Vatican kwa upande wake, itaendelea kuihamasisha Jumuiya ya Kimataifa kutafuta na kudumisha amani, kwa kufanya maamuzi mazito ili kukomesha kuenea kwa biashara ya silaha duniani.

Biashara silaha Afrika
09 November 2018, 09:38