Tafuta

Vatican News
Madaktari wa CUAMM wanaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya uwepo wao nchini Tanzania Madaktari wa CUAMM wanaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya uwepo wao nchini Tanzania 

Jubilei ya miaka 50 ya Madaktari wa CUAMM, nchini Tanzania

CUAMM ilianzishwa mwaka 1950 na kuanza kujielekeza katika huduma bora, makini, ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu Barani Afrika. Chama hiki cha Madaktari kinajihusisha na utekelezaji wa malengo ya muda mfupi na mrefu katika huduma ya afya, ili kuhakikisha kwamba, wananchi wanapata huduma bora ya afya, inayoweza kufikiwa na watu wengi zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Chama cha Madaktari kwa ajili ya Afrika, CUAMM, mwaka 2018 kinasherehekea Jubilei ya Miaka 50 ya uwepo na huduma yake kwa familia ya Mungu nchini Tanzania, kama sehemu ya mchakato wa kupambana na magonjwa yanayoendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu pamoja na kuwatumbukiza watu katika umaskini na majanga mbali mbali ya maisha. CUAMM imekuwa ikishirikiana kwa karibu sana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto katika mchakato wa maboresho ya afya nchini Tanzania, lakini kwa namna ya pekee, mkoani Iringa.

CUAMM ilianzishwa kunako mwaka 1950 na kuanza kujielekeza katika huduma bora, makini, ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu Barani Afrika. Chama hiki cha Madaktari kinajihusisha na utekelezaji wa malengo ya muda mfupi na mrefu katika huduma ya afya, ili kuhakikisha kwamba, wananchi wanapata huduma bora ya afya, inayoweza kufikiwa na watu wengi zaidi.

Mkurugenzi wa CUAMM, Padre Dante Carraro anasema, maadhimisho haya ni mbinu mkakati wa kutaka kusonga mbele zaidi kwa ajili ya maboresho ya afya hasa kwa wananchi wanaoishi vijijini, kwa kuwajibika zaidi katika kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. CUAMM ina amini kwamba, mwelekeo wa Serikali ya Tanzania katika maboresho ya sekta ya afya yataliwezesha taifa kuwa na watu wenye afya bora zaidi, tayari kupambana na changamoto za maisha ya kila siku. Lakini, ikumbukwe kwamba, afya bora ni haki ya kila mwananchi na wala si upendeleo kwa watu wachache ndani ya jamii.

CUAMM inajivunia uwepo na huduma yake kwa familia ya Mungu nchini Tanzania, na hasa zaidi, kwa maskini na watu wanaoishi vijijini. CUAMM itaendelea kutoa ushirikiano wa dhati katika huduma ya afya kadiri ya alama za nyakati! Kwa upande wake, Bwana Roberto Mengoni, Balozi wa Italia nchini Tanzania, anaipongeza CUAMM kwa ushuhuda na majitoleo yake kwa ajili ya huduma vijijini na kwamba, Serikali ya Italia, itaendelea kuunga mkono juhudi zinazotekelezwa na CUAMM nchini Tanzania.

Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa wa Jimbo Katoliki la Iringa, amewapongeza CUAMM kwa moyo wao wa ukarimu na upendo kwa maskini na wagonjwa, kielelezo makini cha ushuhuda wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Mchango wa CUAMM mjini Tosamaganga, Iringa ni mfano bora wa kuigwa katika mchakato wa kudumisha ushirikiano na mshikamano unaofumbatwa katika kanuni ya auni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. CUAMM imekuwa ikiwashirikisha viongozi mahalia kujadili, kupanga na utekelezaji wa yale mambo msingi yaliyoamriwa kwa pamoja.

Huduma ya afya kwa sasa inataka kujielekeza zaidi katika mapambano dhidi ya: ugonjwa wa Ukimwi, Kisukari pamoja na Sonona, magonjwa yanayokuja kwa kasi nchini Tanzania na Afrika katika ujumla wake. Kipaumbele cha kwanza ni huduma ya Mama na mtoto; udhibiti wa maambukizi ya virusi vya ukimwi kutoka kwa Mama kwenda kwa mtoto. Ugonjwa wa Malaria, Kifua Kikuu na majiundo makini ya wafanyakazi katika sekta ya afya ni kati ya mambo muhimu yanayofanyiwa kazi na CUAMM.

Takwimu zinaonesha kwamba, katika kipindi cha miaka 50 ya maisha na utume wa CUAMM inayotekeleza utume wake katika mikoa ya: Dodoma, Iringa, Njombe, Singida, Sinyanga Simiyu, Kagera, Mtwara, Ruvuma, Zanzibar na Pemba, zaidi ya madaktari 315 wamesadaka maisha yao, kwa ajili ya huduma ya afya kwa wananchi wa mikoa hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Dr. Giovanni Dall’Olmo, daktari wa kwanza wa CUAMM, aliwasili kwa mara ya kwanza nchini Tanzania kunako mwaka 1968 na kufungua Hospitali ya kwanza Ikonda, huko Njombe. CUAMM pia inaendelea kutoa huduma katika nchi saba, zilizoko Kusini mwa Jangwa la Sahara nazo ni: Angola, Ethiopia, Msumbizi, Sierra Leone, Sudan ya Kusini, Uganda na Tanzania.

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

07 August 2018, 14:59