Tafuta

Vatican News
Bwana Kofi Annan akisalimiana na Papa Francisko Novemba 2017 Bwana Kofi Annan akisalimiana na Papa Francisko Novemba 2017  

Aliyekuwa katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan afariki dunia

Mtuzwa Nobel ya amani na mwafrika wa kwanza Kofi Annan kuongoza kUmoja wa Mataifa, atambukwa kwa ajili ya jitihada za amani, hata kutafuta kusitisha utumiaji wa nguvu kwa upande wa nchi wanachama. Mwezi Novemba 2017 alizungumza kuhusu suala la wakimbzi na silaha za kinyuklia alipokutana na Papa Francisko katika nyumba ya Mtakatifu Marta.

Sr. Angela Rwezaula - Vatican.

Aliyekuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 80 tarehe 18 Agosti 2018. Annan alikuwa ni mwafrika mweusi wa kwanza kuchaguliwa kuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, akihudumu mihula miwili kuanzia mwaka 1997 hadi 2006. Baadaye akahudumu kama mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Siria na kuchangia kupatikana kwa suluhisho la amani la mzozo wa nchi hiyo, japokuwa ikaibuka tena vita katika nchi hiyo.

Hata hivyo, taarifa kutoka kwa familia na kwenye wakfu wa Kofi Annan ilitangaza kifo chake siku ya Jumamosi 18 Agosti 2018 asubuhi. Katika taarifa kupitia kwenye mtandao wa kijamii, taarifa hiyo ilisema "Kofi Annan, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na aliyewahi kupewa tuzo ya Amani ya Nobel ameaga dunia leo Jumamosi" baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Familia inaomba faragha wakati huu wa maombolezo na mipango ya kuenzi maisha yake pamoja na mipango ya msiba itatangazwa baadaye. Mke wake bi Nane na watoto wao Ama, Kojo na Nina walikuwa pamoja naye wakati umauti ulipomfika. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema amesikitishwa sana na habari za kifo cha mtangulizi wake akimtaja kuwa alikuwa ni "nguvu iliyoongoza kwa mema".

Kofi Annan raia wa wa Ghana, aliyeishi nchini Uswis, alikuwa mwanadiplomasia, mpole na mtulivu, alijulikana sana kwa kuongoza kwa uthabiti jumuiya hiyo ya ulimwengu katika siasa za kimataifa, tangu mwaka 1997 hadi 2006. Hakika tunampoteza mtu wa watu na mwenye kupenda amani ya wa dunia nzima katika haraka zake za hapa na pale.

Mambo makuu katika maisha ya Kofi Annan.

Alizaliwa mwaka 1938 huko Kumasi ambao sasa ni mji wa pili kwa ukubwa nchini Ghana. Mwaka 1962 alianza kufanya kazi kwenye Umoja wa Mataifa huko Geneva, Uswis. Mnamo mwaka 1965 akamuoa bibi Titi Alakija na kupata watoto wawili mvulana na msichana. Mwaka 1984 akamuoa Nane Lagergren  wakili raia wa sweden, baada ya talaka mwaka uliotangulia kwa mke wa kwana, na mwaka 1991 dada yake ambaye ni pacha Efua alifariki dunia.

Kunako mwaka 1993 alichaguliwa kuwa mkuu wa oparesheni za kulinda amani. Na tangia mwaka 1997 akateuliwa kuwa katibu mkuu wa saba wa Umoja wa Mataifa. Ikumbukwe katika harakati za amani, ni mmoja wa washindi wa tuzo la Amani mwaka 2001. Baada ya miaka kumi ya kuhudu, yaani mwaka 2006 akang’atuka kama katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa.

18 August 2018, 16:23