Tafuta

Vatican News
Ulinzi na usalama wa watoto wahamiaji na wakimbizi upewe kipaumbele cha pekee. Ulinzi na usalama wa watoto wahamiaji na wakimbizi upewe kipaumbele cha pekee.  (ANSA)

Ulinzi, usalama na maendeleo ya watoto yapewe kipaumbele cha kwanza.

Kutokana na vita, nyanyaso, kinzani, mipasuko ya kidini, kijamii na kifamilia bila kusahau athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi, watoto wengi wamejikuta wakijiunga na makundi ya wahamiaji na wakimbizi bila ya ulinzi wala uwepo wa wazazi na walei wao. Watoto hawa wanapaswa kulindwa na kutunzwa vyema vinginevyo watageuzwa kuwa watumwa katika mifumo mbali mbali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Bwana Valerio Neri, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kimataifa la “Save the Children” anasema, tangu mwaka 1919, Shirika lake limekuwa mstari wa mbele kuokoa maisha ya watoto sehemu mbali mbali za dunia pamoja na kuwahakikishia leo na kesho iliyo bora zaidi kwa njia ya elimu. Anasema, changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji inapaswa kushughulikiwa kwa kutoa kipaumbele kwa sera na mikakati ya kulinda watoto. Watoto wakimbizi na wahamiaji wamejikuta wakitumbukia katika biashara ya binadamu na viungo vyake!

Ni watoto ambao wako hatarini sana kuingizwa kwenye mifumo ya utumwa mamboleo, hali inayo dhalilisha utu na heshima yao kama binadamu! Kumbe, Mkutano wa Jumuiya ya Ulaya unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni, hauna budi kutoa kipaumbele cha pekee katika utekelezaji wa sera inayojikita katika: kuwapokea, kuwalinda na kuwashirikisha katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwakarimu!

Bwana Valerio Neri anasikitika kusema, Jumuiya ya Umoja wa Ulaya imeshindwa kuwa na sauti na sera moja kuhusu wakimbizi na wahamiaji. Viongozi wa Ulaya wanaendelea kujiimarisha kwa kulinda mipaka ya nchi zao. Lakini, nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zinapaswa kufanya kazi kwa ushirikiano, ili kukabiliana na changamoto mamboleo. Shirika la Kimataifa la “Save the Children” linawataka wakuu wa Jumuiya ya Ulaya kujizatiti zaidi katika kuibua mbinu mkakati na sera kwa ajili ya kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso na dhuluma! Wahakikishe kwamba, haki msingi za watoto hawa zinalindwa na kuheshimiwa.

 

26 June 2018, 09:09