Tafuta

Vatican News
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hivi karibuni limepitisha sheria kupambana na biashara ya binadamu ulimwenguni. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hivi karibuni limepitisha sheria kupambana na biashara ya binadamu ulimwenguni.  (AFP or licensors)

Baraza la Usalama la UN na mapambano dhidi ya biashara ya binadamu ulimwenguni!

Biashara ya binadamu pamoja na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo ni mambo ambayo yanaendelea kunyanyasa na kudhalilisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ni matukio yanawapokonya watu haki zao msingi na kuwageuza kuwa sawa na bidhaa, jambo ambalo halikubaliki hata kidogo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo ni mambo ambayo yanafumbatwa kwa namna ya pekee kabisa, katika kazi za suluba, ukahaba, biashara haramu ya viungo vya binadamu, biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na uhalifu wa magenge; matendo yote haya ni uhalifu dhidi ya ubinadamu na yanapaswa kutambulika hivi kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa,  viongozi wa kidini, kisiasa na kijamii kama yanavyobainishwa na sheria za kitaifa na kimataifa bila kupindishwa pindishwa au kufumbiwa macho!

Hivi karibuni, Baraza la Usalama wa Umoja wa Mataifa limepitisha azimio la vikwazo vya uchumi dhidi ya watu sita wanaotuhumiwa kujihusisha na ulanguzi na biashara haramu ya binadamu kutoka Eritrea na Lybia, nchi ambazo kwa sasa zimekuwa ni kitovu cha biashara ya binadamu na utumwa mamboleo. Akaunti za fedha za watuhumiwa hawa zimetaifisha na kwamba, wamepigwa rufuku kusafiri nje ya nchi zao. Hawa ni Bwana Ermias Ghemay na Fitiwi Abdelrazak kutoka Eritrea. Wengine ni Ahmad Oumar al Dabbashi, Mus’ab Abud Qarin, Mohammed Kachlaf pamoja na Al Rahama Al Milad, wote kutoka nchini Lybia.

Matukio ya biashara haramu ya binadamu yana madhara makubwa sana si tu kwa utu na heshima ya binadamu, bali hata kwa ustawi, maendeleo, usalama na amani nchini Lybia. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linasema, litatekeleza kwa vitendo azimio hili kama onyo kwamba, Jumuiya ya Kimataifa haina tena mchezo dhidi ya biashara haramu ya binadamu inayodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu anasema Nikki Haley, Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba kuna zaidi ya watu milioni 46 waliotumbukizwa katika utumwa mamboleo sehemu  mbali mbali za dunia. Hawa ni watu wanaofanyishwa kazi za suluba viwandani, migodini na mashambani kwa ujira “kiduchu”! Baadhi yao hasa wanawake wanajikuta wakitumbukia katika ndoa za shuruti, kazi za majumbani na biashara ya ngono!

Baba Mtakatifu Francisko kwa kushirikiana na viongozi mbali mbali wa kidini dunia amekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza mapambano dhidi ya utumwa mamboleo anaendelea kufafanua kwamba, katika miaka ya hivi karibuni kumekuwepo mikutano ya wakuu wa dini pamoja na mameya wa miji mikuu kutoka sehemu mbali mbali duniani waliokutana na kuamua kujifunga kibwebwe ili kupambana na hatimaye, kung’oa kabisa utumwa mamboleo unaonyanyasa utu na heshima ya binadamu; matukio ambayo yamekuwa na umuhimu wa pekee kabisa katika mapambano haya.

Kikundi cha Kimataifa cha Mtakatifu Martha,  hii ni taasisi ya kimataifa iliyoanzishwa kunako mwezi Aprili 2014 na Baba Mtakatifu Francisko na kuongozwa na Kardinali Vincent Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Wales, kwa kushirikiana na wakuu wa Majeshi ya Polisi na Maaskofu kutoka sehemu mbali mbali za dunia; wanaendelea kufanya kazi kwa pamoja ili kung'oa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo pamoja na kutoa huduma za kichungaji kwa wahanga wa vitendo hivi kwa kinyama. Kikundi hiki kinapania pamoja na mambo mengine, kuibua mbinu mkakati wa kuzuia vitendo hivi vya kinyama vinavyodhalilisha utu na heshima ya binadamu pamoja na kuendelea kutoa huduma za kichungaji  na kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo, donda ndugu katika ulimwengu mamboleo.

 

12 June 2018, 09:24