Tafuta

Vatican News
Tarehe 3 Mei 2018 Jumuiya ya Kimataifa imeadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Kimataifa Tarehe 3 Mei 2018 Jumuiya ya Kimataifa imeadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Kimataifa  (AFP or licensors)

Siku ya Uhuru wa Vyombo Vya Habari Duniani 2018

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Bwana Antonio Guterres katika ujumbe wake kwa Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani kwa mwaka 2018 anasema, vyombo vya habari ni muhimu sana katika mchakato wa ujenzi wa amani na haki msingi za binadamu sehemu mbali mbali za dunia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Jumuiya ya Kimataifa, tarehe 3 Mei 2018 inaadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani sanjari na Jubilei ya Miaka 25 tangu siku hii ilipoanzishwa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 1993. Itakumbukwa kwamba, mwaka huu pia, Umoja wa Mataifa unasherehekea kumbu kumbu ya miaka 70 tangu Tamko la Haki Msingi za Binadamu litolewe.

Hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya kumbu kumbu ya miaka 70 tangu Tamko la Haki msingi za Binadamu litolewe na Umoja wa Mataifa alisema, kuna haja ya kujenga na kudumisha amani duniani inayofumbatwa katika ukweli, haki, mshikamano tendaji na uhuru wa kweli. Pia kuna umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu kama msingi wa kukuza na kudumisha amani duniani. Dhamana hii inaweza kutekelezwa kwa njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kuheshimiana na kuthaminiana.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Bwana Antonio Guterres katika ujumbe wake kwa Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani kwa mwaka 2018 anasema, vyombo vya habari ni muhimu sana katika mchakato wa ujenzi wa amani na haki msingi za binadamu. Kumbe, kuna haja ya kujenga jumuiya zinazosimikwa katika misingi ya ukweli na uwazi; demokrasia pamoja na kuwawajibisha wale walioko madarakani. Wafanyakazi katika tasnia ya habari ni chachu muhimu sana ya maendeleo endelevu ya binadamu kwani hutanabaisha kuhusu changamoto za kitaifa na kimataifa, kwa kutoa taarifa zinazohitaji kuelezwa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema, huduma ya waandishi wa habari ina thamani kubwa sana katika umma. Kumbe, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, Sheria zinazolinda na kusimamia uandishi huru wa habari zinakuza uhuru wa watu kujieleza na kuhakikishwa. Uhalifu dhidi ya waandishi wa habari lazima uvaliwe njuga na hatua za kisheria zichukuliwe.  Bwana Antonio Guterres anahitimisha ujumbe wake kwa njia ya video katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani kwa mwaka 2018 kwa kutoa wito kwa Serikali mbali mbali duniani kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari sanjari na kuwalinda waandishi wa habari. Anakaza kusema, kuchagiza vyombo huru vya habari ni kusimamia haki ya watu kupata ukweli!

Kama sehemu ya maadhimisho haya, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa muda wa siku mbili kuanzia tarehe 2 hadi 3 Mei 2018 kwa kushirikiana na Rais Nana Akufo-Addo wa Ghana wameadhimisha siku hii kimataifa kwa kubainisha mchango wa tasnia ya habari katika kuiwajibisha serikali na kudumisha ukweli na uwazi katika mchakato mzima wa uchaguzi mkuu pamoja na kubainisha mbinu mkakati kwa vyombo vya sheria kukuza na kudumisha uhuru wa vyombo vya habari. Usalama wa waandishi wa habari ni mada ambayo pia imechambuliwa kwa kina mapana kutokana na ukweli kwamba, hawa ni watu ambao wanatekeleza dhamana na majukumu yao katika mazingira hatarishi na tete sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa Siku ya 52 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni ambayo kwa mwaka huu inaadhimishwa hapo tarehe 13 Mei 2018, Siku kuu ya Kupaa Bwana Mbinguni, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Kweli itawaweka huru: habari za kughushi na uandishi wa habari wa amani anakazia umuhimu wa familia ya Mungu duniani kupata habari za ukweli na kwamba, wafanyakazi wa tasnia ya mawasiliano ya jamii wanayo dhamana ya kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni wahudumu wa ukweli, kwa kutafuta na kuambata ukweli; kwa kukuza na kudumisha uandishi wa habari unaofumbatwa katika amani, upendo na mshikamano wa dhati.

Hivi karibuni Baba Mtakatifu Francisko akizungumza na viongozi wakuu wa Gazeti la  “Avvenire” linalomilikiwa na kuendeshwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, amekazia umuhimu wa vyombo vya habari vya Kanisa katika huduma ya binadamu kama inavyofafanuliwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican; kwa kuheshimu tunu msingi za maisha ya binadamu na kuzielekeza tena kwenye chemchemi yake ya Kimungu ili ziweze kusafishwa na kupyaishwa tena! Kanisa katika mchakato wa maisha na utume wake, linataka kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili; kukuza na kudumisha majadiliano; kutafuta na kuambata ukweli katika hali ya unyenyekevu, ili kulinda na kudumisha ukweli unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu!

 

03 May 2018, 09:49