Mchango wa Vatican Katika Kukuza na Kudumisha Utu, Heshima na Haki Msingi!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA79 ulioanza kikao chake tangu tarehe 24 hadi 30 Septemba 2024 iliongozwa na kauli mbiu “Hakuna kumwacha yeyote nyuma: kushirikiana ili kuendeleza amani, maendeleo endelevu na utu wa binadamu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.’’ (Leaving no one behind: Acting together for the advancement of peace, sustainable development and human dignity for present and future generations.” Katika Kipindi cha Mwaka 2024 mjadala huu umefanyika kwa wakuu wa nchi na serikali kutoa hotuba zao kwa kujikita katika maeneo kama vile: Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGS; Mabadiliko ya tabianchi; Afya ya umma; Ukosefu wa usawa; mahitaji msingi ya kibinadamu, amani na usalama bila kusahau maendeleo ya sayansi na teknolojia. Ni katika muktadha huu, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, katika hotuba yake ya tarehe 28 Septemba 2024 amekazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika kutafuta na kudumisha amani, bila kumwacha mtu yeyote nyuma. Vita ni janga la Kimataifa kwani imepelekea mauaji ya watu wasiokuwa na hatia pamoja na uharibifu wa mali za watu na miundombinu. Hii ni pamoja na uharibifu wa nyumba za Ibada, shule, hospitali pamoja na kuacha athari kubwa katika mazingira nyumba ya wote. Katika mkutano huu, Vatican pia imeadhimisha kumbukizi ya miaka 70 tangu ilipokubaliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwa ni mtazamaji kwenye Umoja wa Mataifa na hivyo kuendelea kujikita katika kulinda na kudumisha: utu, heshima, haki msingi za binadamu; usawa, uhuru na haki za kila nchi kujiamria mambo yake yenyewe; kutafuta na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano.
Vatican inaunga mkono Mkataba wa Kimataifa unaopiga rufuku utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za nyuklia. Hii inatokana na ukweli kwamba, matumizi ya silaha hizi hayana macho wala pazia, na hayawezi kuchagua wala kubagua! Katika kipindi kifupi tu, matumizi ya silaha hizi yanaweza kusababisha maafa makubwa na yatakayodumu kwa muda mrefu kwa binadamu na mazingira yake. Vatican inasikitika kusema kwamba, mashambulizi ya nyumba za Ibada, shule na hospitali linaanza kuwa ni jambo la kawaida, kiasi cha kuathiri maisha ya watu wengi. Kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika mchakato wa kutafuta na kudumisha amani, ili kulinda maisha, mali na kuendelea kutunza mazingira nyumba ya wote. Mtakatifu Yohane XXXIII katika Wosia wake wa Kitume, “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” anasema amani inasimikwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru. Kumbe, kuna haja ya kukuza na kudumisha utamaduni wa kuheshimu: utu, heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu sanjari na haki msingi za binadamu na kwamba, kila mtu anapaswa kuwajibika, ili kujenga na kuimarisha mafungamano ya kijamii na mahusiano pamoja na Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, amani inawezekana ikiwa tu watu wataweka nia ya dhati kabisa kuitafuta, kuilinda na kuidumisha kwa njia ya diplomasia, majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kung’oa mambo yote yanayopelekea kinzani, migogoro na vita. Jambo la kwanza ni kuhakikisha kwamba, baa la njaa linalopekenya na kusigina utu, heshima na haki msingi za binadamu linatokomezwa.
Mapambano dhidi ya umaskini ni kati ya vipaumbele vya Jumuiya ya Kimataifa inayopaswa kujikita katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Lakini kwa bahati mbaya, Jumuiya ya Kimataifa imeendelea kutumia rasilimali fedha nyingi kwa ajili ya utenegenezaji, ulimbikizaji na ununuzi wa silaha, hali inayoonesha tabia ya kutokuaminiana baina ya Jumuiya ya Kimataifa pamoja na Taasisi za fedha Kimataifa. Adhabu ya kifo hii ni kielelezo cha ukatili wa hali ya juu kabisa na wala haiwezi kukubalika tena, kwani inakwenda kinyume cha mwanga wa Injili. Hii ni changamoto kwa Serikali na wadau mbalimbali kujizatiti katika kulinda, kutunza na kudumisha uhai wa binadamu tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti yanapomfika kwani kimsingi uhai ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwa nchi zile ambazo bado zinaendekeza adhabu ya kifo, sasa ni wakati wa kutafuta adhabu mbadala, ili kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Ni katika muktadha huu pia biashara haramu ya binadamu pamoja na viungo vyake inapaswa kusitishwa mara moja. Utu, heshima na haki msingi za wakimbizi, wahamiaji na wafungwa zinapaswa kulindwa na wote. Kanuni maadili na utu wema zinapaswa kufuatwa na wote katika matumizi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Vita kati ya Ukraine na Urusi; Israeli na Palestina pamoja na sehemu mbalimbali za dunia ambako bado moshi wa kinzani na vita bado unafuka, wanapaswa kusitisha mara moja na hivyo kuanza kujielekeza katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mateka na wafungwa wa kivita wanapaswa kuachiliwa wote bila ya masharti. Hali ya Lebanon kwa sasa ni hatari sana kwa usalama, amani, ustawi na maendeleo huko Mashariki ya Kati. Vita Ukanda wa Mashariki ya kati vinaendelea kusababisha idadi kubwa ya wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum. Kumbe, kuna haja ya kuzingatia Sheria ya Kimataifa. Vita nchini Siria, Sudan ya Kusini pamoja na Sudan Kongwe; Jimbo la Cabo Delgato, nchini Msumbiji, pamoja na DRC; Haiti na Myanmar inaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watoto, wanawake na wazee! Wakristo ni kati ya waamini wanaoendelea kuteseka, kunyanyasswa na kuuwawa kikatili. Uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini unatiwa shaka na Serikali ya Nicaragua hasa kwa vitendo vyake dhidi ya viongozi wa Kanisa.
Vatican iko tayari kukaa na Serikali ya Nicaragua ili kujadili shida na changamoto hii, ili hatimaye, kukuza na kudumisha: haki, amani, utulivu, ustawi; umoja, udugu na mshikamano wa kibinadamu, kwa kuondokana na maamuzi mbele. Vatican inasikitishwa na hali inayovyoendelea huko Venezuela hasa baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika hivi karibuni. Huu ni mwaliko wa kulinda na kudumisha: Utu, heshima, haki msingi za binadamu; Uhuru wa dhamiri na uhuru wa kuabudu ni mambo msingi yanayopaswa kudumishwa. Mifumo mbalimbali ya ukoloni wa kiitikadi inaendelea kusigina tunu msingi za maisha ya mwanadamu. Mashambulizi dhidi ya Kanisa katika kipindi cha mwaka 2023 yameongezeka maradufu, changamoto na mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika tunu msingi za Jumuiya ya Kimataifa. Majadiliano katika ukweli na uwazi; Kipaumbele kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ni mwanzo mzuri wa kulinda na kudumisha haki, amani na maridhiano duniani.