Mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA 79: Matumaini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mjadala mkuu wa Mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA79 umeanza kwenye makao makuu ya UN jijini New York, Marekani ikiwa ni baada ya kutamatika kwa Mkutano wa Zama Zijazo, SOTF. Kaulimbiu ya kikao hiki cha Septemba, cha 79, ni (Leaving no one behind: Acting together for the advancement of peace, sustainable development and human dignity for present and future generations). Yaani “Hakuna kumwacha yeyote nyuma: kushirikiana ili kuendeleza amani, maendeleo endelevu na utu wa binadamu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.’’ Katika maamuzi yaliyofanywa kwa ushauriano mkubwa na Rais wa UNGA79, Philemon Yang, viongozi wengi wa nchi wanaweza kurejea tena kwenye kauli mbiu hii katika hotuba zao ingawa hawawajibishwi kufanya hivyo. Katika Kipindi cha Mwaka 2024 mjadala huu unafanyika kwa siku sita ambapo wakuu wa nchi na serikali wanatoa hotuba zao kwa kujikita katika maeneo kama vile: Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGS; Mabadiliko ya tabianchi; Afya ya umma; Ukosefu wa usawa; mahitaji msingi ya kibinadamu, amani na usalama bila kusahau maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Ni katika muktadha huu, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, katika hotuba yake, Jumatatu tarehe 23 Septemba 2024, amekazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kuwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi kwa kujikita katika: Utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na kusimama kidete kupambana na umaskini; kwa kukuza na kudumisha haki na amani, kama kichocheo cha maendeleo endelevu ya binadamu; mageuzi makubwa katika mfumo wa fedha katika Taasisi za Fedha Kimataifa pamoja na utekelezaji wa sera na mkakati wa kusamehe deni la nje kwa nchi changa zaidi Ulimwenguni. Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kufanya upembuzi yakinifu kuhusu matumizi bora zaidi ya teknolojia ya akili mnemba, kwa kukazia kanuni maadili na utu wema; Ulinzi na usalama, Uwajibikaji pamoja na kuangalia athari za matumizi ya teknolojia mnemba katika mfumo mzima wa utengenezaji wa ajira.
Hii ni changamoto ya kupambana na umaskini pamoja na mifumo ya unyonyaji. Kuhusu matumizi ya maneno ya “afya ya uzazi”, Kardinali Parolin anasema, mahusiano kati ya mwanaume na mwanamke hayana budi kuongozwa na kanuni maadili na utu wema na kwamba, utoaji mimba ni kitendo cha ukatili dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kuhusu usawa wa kijinsia, Vatican inatambua uwepo wa jinsi ya kiume na kike na kwamba, jinsi hizi mbili zinakamilishana kadiri ya mpango wa Mungu. Kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujitahidi kujenga familia kubwa ya binadamu inayosimikwa katika misingi ya haki na amani pamoja na kujitahidi kuondokana na vita na misigano ya kijamii.