Tafuta

Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora, katika maadhimisho ya Sherehe ya Pasaka ya Bwana, Dominika tarehe 31 Machi 2024 amekazia kuhusu imani na ushuhuda wa Fumbo la Pasaka. Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora, katika maadhimisho ya Sherehe ya Pasaka ya Bwana, Dominika tarehe 31 Machi 2024 amekazia kuhusu imani na ushuhuda wa Fumbo la Pasaka. 

Ujumbe wa Kardinali Protase Rugambwa Kwa Kipindi cha Pasaka 2024

Kardinali Protase Rugambwa, katika maadhimisho ya Sherehe ya Pasaka amekazia kuhusu: Imani na ushuhuda wa Fumbo la Pasaka na kwamba: Ufufuko wa Kristo Yesu ni ukweli wa kihistoria na hivyo, kwa njia ya Ubatizo wakristo wanaingizwa katika maisha mapya, maisha ya Kristo, changamoto ya kukumbatia imani na mwanga wa Ufufuko wa Kristo Yesu, ambaye ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Waamini wajiepushe na dhambi.

Na Kardinali Protase Rugambwa, Jimbo kuu la Tabora, Tanzania.

Wapendwa katika Kristu, Bwana amefufuka!! Tumeyasikia hayo jana wakati tunaadhimisha Mkesha wa Pasaka na leo tena tunalirudia tunapoadhimisha Jumapili ya Ufufuko wa Bwana: Kristu ameshinda mauti, yu mzima na hafi tena Aleluya!!!   Kwa kweli leo Kanisa linaadhimisha Sherehe muhimu sana katika Mwaka wa Kiliturujia yaani, Ufufuko wa Bwana.  Muda mfupi uliopita tumelisikia simulizi kutoka katika Injili ya Yohana kuhusu safari ya Maria Magdalena, Petro na Yohane walivyokwenda Kaburini na wasimkute Yesu, siku tatu baada ya kuwa amezikwa humo.  Mtu anaweza kujiuliza: Haiwezekani kuwa mwili wake ulikuwa umechukuliwa au kuibiwa? (Vijana kama ninyi wenye kupenda kuuliza na wakati mwingine kuwa na mashaka kwa kila kitu).  Yohane analijibu swali hili kwa kukanusha na kusema kuwa alipofika Kaburini aliviona vitambaa vya sanda vimelala, na Simoni Petro pia alipoingia Kaburini alivitazama vitambaa vya Sanda vilivyolala na hata ile leso iliyokuwa kichwani pake ambayo ilikuwa imezongwa zongwa na kuwa sehemu nyingine.  Bila shaka Mwinjili Yohane anataka kutuambia kuwa, kama Yesu angekuwa amechukuliwa basi hivyo viliyoonekana hapo visingekuwepo.  Inaonekana ni kama Yesu alinyanyuka kutoka katika ndoto na akatoka Kaburini! na kweli ilikuwa hivyo.  Ndugu zangu, Kristo amefufuka!! Mwili wake uliokuwa umekufa uligeuzwa na kubadilishwa na hakubaki kuonekana kama alivyokuwa kabla ya kifo chake. Kama anavyosema Mtume Petro katika somo la kwanza: “Nasi tu mashahidi wa mambo yote aliyoyatenda katika nchi ya Wayahudi na katika Yerusalemu; ambaye walimwua wakimtundika mtini. Huyo Mungu alimfufua siku ya tatu” Hili linatusaidia kujua kuwa Ufufuko wa Yesu ni ukweli wa ki-historia ni si kitu kilichobuniwa na Mitume.  Na kwetu Wakristu, ufufuko wa Yesu si suala la wakati uliopita bali ukweli ambao unatufuata kwani katika ubatizo tumepata na kuingizwa katika maisha ya Kristo, maisha mapya.  Kila siku na hasa siku ya leo, tunaonja na inabidi tuendelee kuyaonja hayo mabadiliko katika misha yetu ya kutoka katika kifo na kuingia katika maisha mapya, aliyoyaleta Bwana wetu Yesu Kristu Mfufuka.

Imani na Ushuhuda wa Fumbo la Pasaka:
Imani na Ushuhuda wa Fumbo la Pasaka:

Ndugu zangu yanapotupata matatizo mbali mbali katika maisha: Magonjwa, kukosa watu wa kukaa nasi karibu, tunapokumbwa na mikasa mbalimbali, kuwapoteza ndugu zetu, kukosa kazi, kushindwa mitihani, nk., tunaumia sana na tunajisikia kwa namna fulani kama vile tunapoteza maisha na tuko katika kufa. Katika hali kama hizi za matatizo, hatupaswi kubaki pekepeke tumejifungia katika mageto yetu, bali tunapaswa kumuomba Mwenyezi Mungu atusaidie, tukimuomba ageuze hayo “maisha ya kufa” katika maisha ya uzima. Tunapojikuta tuko kwenye giza la maisha, sisi Waamini yabidi tukumbuke daima kuwa, kamwe mwanga wa Imani na mwanga wa ufufuko wa Yesu hautatutupa na kutuacha. Ni kweli kabisa kuwa tunapojitizama sisi wenyewe na hata tunapoyaona yale yanayotokea sehemu mbali mbali nahata kwa jirani zetu, tunayaona mambo na matukio yanayokatisha tamaa, vita, kutoelewana, njaa, umaskini, nk. Hata katika hali hizi sisi wenye Imani hatupaswi kusahau kuwa Mwanga wa Kristu aliyeukomboa Ulimwengu wote kwa kuufia utafika huko kwenye hali hizi za kukatisha tamaa.  Yeye aliyachukua masumbufu ya Mwanadamu na kila kilichoumbwa na aliyabeba mabegani pake kwa mateso aliyoyapitia. Na kwa ufufuko wake ameyapeleka mbele ya huruma ya Mungu Baba. Kumbe Mungu naye anakuwa karibu nasi na kuwa tayari kuyatatua hayo yaliyo magumu na yenye kuumiza, kwa nanma mbali-mbali ambazo tunashindwa kuziona na kuzifahamu. Hili linafanyika kwa namna ya pekee kupitia kwenye Kanisa lake na kila aliyetayari kumshuhudia Kristo Msulubiwa na aliyefufuka kwa kuyafanya yale aliyoyafunua kwetu na akayafanya yeye mpaka mwisho wa uhai wake. Tujiulize ni Mapadri wangapi, Wawekwa wakfu na hata Walei wanaojitoa kama wapelekwa wa Kristo kwenda na kupeleka upendo katika maeneo hayo ya wenye shida na mahangaiko, kumbe kama anavyosema Papa Fransisko likawa ni “Kanisa maskini kati ya maskini na wanaoteseka."

Ushuhuda wa Ufufuko ni kaburi wazi
Ushuhuda wa Ufufuko ni kaburi wazi

Mbali na matatizo hayo tuliyoyasema, kile kinacholeta kifo kibaya na kweli kile ambacho ungekiita kifo cha kiroho, ni dhambi.  Yaani pale tunapoamua kumweka Mungu pembeni na kufanya yaliyo yetu, kama tunavyotaka, na hivyo kukana yale aliyoyafunua kwetu, kwa maneno na matendo, huyo Kristu Mfufuka, tunayemshangilia tangu Jana.  Kama waamini, ni wazi kwamba tunapomweka Mungu kando tunajikuta katika mahangaiko, mateso na kukosa furaha ambayo yeye alitaka tuipate daima na ndio maana akamtuma huyo Mwanae aje kutupatanisha naye na hivyo kutukomboa.  Yote yaliyo kinyume na maagizo yake, yanatupeleka katika kifo na Ufufuko kwetu utafika iwapo njia tunayotaka kufuata katika maisha itakuwa ni hiyo ya Bwana Mfufuka.  Hata hivyo tusikate tamaa, kwani siku hii ya Ufufuko inakuja na habari njema kwetu kama tulivyoisikia kutoka katika somo la kwanza: “huyu ndiye aliye amuriwa na Mungu awe Mhukumu wa wahai na wafu. Huyo, manabii wote humshuhudia, ya kwamba kwa jina lake kila amwaminie atapata ondoleo la dhambi”.  Tukumbuke kuwa yawezekana kabisa kuwa nasi tunamweka Mungu kando ha hivyo kujikuta katika hali mbaya. Tusisahau kuwa Mungu hachoki hata mara moja kutusamehe. Ni sisi tu tunaochoka kumuomba msamaha. Hatuna budi pia kukumbuka kuwa, zawadi kubwa na ya pekee ya Yesu Mfufuka, ni msamaha.  Yeye mwenyewe alipowatokea Petro na mitume wengine waliokuwa wamemkana na kumsaliti aliwasamehe na kuwapenda.  Leo tunaalikwa nasi kila mmoja ajitamaze katika suala la mahusiano yukoje, katika familia zetu, shule, na kokote kule.  Tujifunze kutoka kwa Kristu, yeye aliyetupatanisha na Mungu, roho hiyo ya kusamehe.  Si rahisi kuyafanya hayo lakini kwa vile nguvu twaweza kuipata kutoka kwa huyo Mfufuka tumuombe atusaidie neema hiyo ya kupenda na kusamehe kama alivyofanya yeye, na kwa namna hiyo ndipo tutakapokuwa tunafufuka pamoja naye.  Wapendwa katika Kristo, hiyo habari njema ya ufufuko tuliyoipata na kwa kweli ndo inayotukutanisha hapa leo kama wa-Kristo, tusiimiliki sisi na tukabaki nayo bila kwenda kuwashirikisha wengine, katika masikitiko au furaha.  Tufanye kama alivyofanya huyo Maria Magdalene na akina Mama wenzake, twende kwa haraka na tuwashirikishe yanayokuwa yanatokea katika maisha yetu.   Tumwombe Mungu, na kwa maombezi ya Bikira Maria, ili furaha hii ya Pasaka tuliyoipata tena mwaka huu itusindikize daima katika maisha yetu ya usoni.  Tumsifu Yesu Kristo.   

Kristo Mfufuka ni nuru ya Mataifa
Kristo Mfufuka ni nuru ya Mataifa

Mahubiri ya Mkesha wa Pasaka ya Ufufuko wa Bwana. Wapendwa katika Kristu, kwa furaha kubwa tunapenda tumshukuru Mwenyezi Mungu, aliyetuwezesha tena kuisherehekea Siku kubwa hii ya Pasaka ya Mwaka huu 2024. Aleluya kweli Bwana amefufuka kama alivyosema!!!!! Tunapoadhimisha Mkesha huu wa Pasaka, nawaalika kwa namna ya pekee tupende kuimarisha na kuikuza Imani yetu katika Ufufuko na tuendelee kuishi kama wana wa Ufufuko katika maisha yetu ya kila siku.  Kama anavyosema Mtakatifu Augustino: “Imani ya wakristu ni ufufuko wa Kristo.” Ukweli kwamba Yesu alikufa, wote wanaamini, hata wapagani, na hata maadui wake hawana mashaka juu ya hilo.  Lakini kwamba amefufuka, ni Wakristu tu na huwatakuwa Wakristu wasio amini katika hilo, kwani kama Kristu hakufufuka basi Imani yetu ni bure!!!!! Napenda kumbe leo nipendekeze mambo matatu ambayo nayaona ni muhimu katika kutusaidia ili tukue katika Imani. Kwanza kabisa Imani katika ufufuko, kitu kilicho msingi katika makuzi ya Imani yetu linajengeka kama tutamfahamu Yesu ni nani, yaani yule Yesu wa historia, Yesu wa Nazareti. Yule ambaye hata wanafunzi wake hawakumfahamu vizuri kupitia kwenye Maandiko Matakatifu, kwamba ilibidi afufuke. Tunadaiwa kwenda kwenye Maandiko Matakatifu (na hasa Injili) na tuyasome vizuri kila mara ili tuweze kusaidiwa kuamini katika ufufuko wake.  Kumbe, pamoja na kuyasoma Maandiko hayo, kila mtu kwa wakati wake, itabidi tukuze utume wa Biblia katika Jumuiya zetu na Jimboni kwetu. (Kumbuka Maadhimisho ya Miaka 50 ya Jubilei ya Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristu katika Nchi za AMECEA).

Jubilei ya Miaka 50 ya Jumuiya Ndogondogo za Kikristo 2023-2024
Jubilei ya Miaka 50 ya Jumuiya Ndogondogo za Kikristo 2023-2024

La pili ambalo ni muhimu tunapotafuta kukuza Imani yetu katika ufufuko wa Bwana, ni suala zima la kuwa mashahidi wa Kristu aliyefufuka katika maisha yetu kwa ushujaa na bila woga. Ni kuyataja na kuyasambaza yote tuliyoyajua kumhusu yeye na kuyaishi katika maisha yetu tukifuata nyayo za hao wafuasi wa kwanza wa Kristu, mfano ni Maria Magdalena na akina Mama wenzake ambao bila woga hawakuchoka kumtafuta huyo aliyekuwa Mwalimu wao na baadae kumtangaza kwa wengine. Hawa wamekuwa ni wamisionari wa kwanza kabisa, ambao walikwenda kutoa Habari Njema kwa hao Mitume ambao bado hawakuamini katika hilo waliloambiwa.  Katika Masomo tutakayo yasikia katika Kipindi hiki cha Pasaka, wako akina Mtakatifu Petro pia ambao hawaogopi kumtaja na kuzungumza juu ya Kristo na Ufufuko wake na nguvu alizo nazo: “Nasi tu mashahidi wa mambo yote aliyoyatenda katika nchi ya Wayahudi na katika Yerusalemu; ambaye walimwua wakimtundika mtini. Huyo Mungu alimfufua siku ya tatu…manabii wote humshuhudia ya kwamba kwa jina lake kila amwaminie atapata ondoleo la dhambi”. Na yote hayo tutaweza kuyafanya katika Imani, tukimtanguliza Kristu Mfufuka ili atuongoze katika yote tuyasemayo na tutakayotenda.  Na kwa namna hiyo Pasaka itakuwa kwetu wakati unaofaa wa Neema, unaotukumbusha wajibu wetu kama Wakristu wa kuishi daima tukiwa na Kristu ambaye labda yawezekana tulikuwa tumemsaliti kama ilivyokuwa kwa Yuda au tumemkana kama alivyofanya Petro na tukawa tumemweka kaburini. 

Waamini wanaalikwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka
Waamini wanaalikwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka

Kumbe, Pasaka ya leo itutoe katika hali hiyo ya kumweka Kristu na maisha yetu kaburini na badala yake tufufuke na tubadilike tukilenga kutembea kwenye maisha mapya ya Ufufuko. Kristu aliyefufuka atangazwe na atutangulie nasi tumfuate ili atupeleke katika maisha hayo mapya na kututoa kwenye giza linalotuangamiza. Mwisho kabisa napenda niwakumbushe kuwa Imani inakua kama inashirikishwa na kupelekwa kwa wengine. Hii kazi ya kupeleka kwa wengine Imani ambayo mtu kaipata tayari, ni fursa ya kukua katika Imani. Hili adhimisho la ufufuko wa Bwana yabidi litukumbushe wabatizwa wote wajibu tulionao wa uinjilishaji unaotokana na Imani thabiti.  Waraka wa Kitume wa Furaha ya Injili, “Evangelii gaudium” uliochapishwa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 24 Novemba 2013, miaka kumi iliyopita, unatoa kipaumbele cha kwanza kwa furaha ya Injili, kwa kuwaalika waamini kushirikisha furaha yao inayopata chimbuko kutoka katika huruma na upendo wa Mungu kwa wanadamu. Katika mwono huu, Kristo ni kiini cha Injili na kwamba, Kanisa linaalikwa kufanya mageuzi makubwa kama sehemu ya Uinjilishaji Mpya. Waraka huu ni ramani inayotoa dira na mwongozo thabiti wa shughuli za kichungaji unaopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa kwa siku za usoni kwa kuwa na mwono wa kinabii na mwelekeo chanya, licha ya vikwazo na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa Kanisa, ili Kristo Mfufuka aendelee kupeperusha bendera ya ushindi. Waraka huu wa kitume unachota utajiri wake katika mapendekezo yaliyotolewa na Mababa wa Sinodi juu ya Uinjilishaji Mpya kama njia ya kutangaza na kushuhudia imani ya Kikristo.

Waamini wajenge utamaduni wa kusoma, kulitafakari na kulimwilisha Neno.
Waamini wajenge utamaduni wa kusoma, kulitafakari na kulimwilisha Neno.

Baba Mtakatifu Francisko anatualika sote tuwe wainjilishaji. Rej. Evagelii gaudium, Na.121. Na tukifanya hivyo basi tutakuwa mashahidi wa Habari Njema ya Wokovu.  Hatuwezi kuyafanya hayo kama Imani yetu inalegalega.  Kumbe tukisukumwa na Imani katika Kristu mfufuka, waamini wote twaweza kuwa ni wahudumu imara na wamisionari wa Kristu tukiamini kuwa kazi hiyo tunaifanya tukiwa na Kristu mwenyewe mfufuka ambaye yu kati yetu na tayari kutenda pamoja nasi kama alivyoahidi na kusema: “Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba na Mwana na Roho Mtakatifu na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi. Na tazama mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa Dahari”. Mt. 28: 19-20. Wapendwa waamini mnaopenda kuendelea kukua na kukaa katika Imani hiyo mliyopokea baada ya kubatizwa na wale wote watakaoingia katika Familia ya wanaomfuata Kristo mfufuka kwa ubatizo watakaopewa usiku huu, tumwombe Kristo aliyefufuka, kwa maombezi ya Bikira Maria Mama wa Mitume ili Pasaka yetu ya Mwaka huu, ituimarishe tena katika Imani, tuweze kwa nguvu zaidi kumshuhudia Kristu Mfufuka katika maisha yetu ya kila siku. Tumsifu Yesu Kristu.

Kardinali Protase Pasaka
01 April 2024, 15:10