Tafuta

Maparoko 300 walioteuliwa na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki toka sehemu mbalimbali za dunia, wanashiriki mkutano maalum kuanzia tarehe 28 Aprili hadi tarehe 2 Mei 2024 mjini Vatican. Maparoko 300 walioteuliwa na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki toka sehemu mbalimbali za dunia, wanashiriki mkutano maalum kuanzia tarehe 28 Aprili hadi tarehe 2 Mei 2024 mjini Vatican.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Maparoko Kwa Ajili ya Sinodi: Mkutano wa Kimataifa 28 Aprili - 2 Mei 2024

Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, Baraza la Kipapa la Kwa Ajili ya Makanisa ya Mashariki, Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu pamoja na Baraza la Kipapa kwa Ajili ya Makleri, kwa pamoja wameandaa mkutano wa kimataifa unaowashirikisha Maparoko 300 kutoka sehemu mbalimbali za dunia, kushiriki mkutano maalum kuanzia tarehe 28 Aprili hadi tarehe 2 Mei 2024 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Maparoko Kwa Ajili ya Sinodi." Ushiriki wa Maparoko!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, Baraza la Kipapa Kwa Ajili ya Makanisa ya Mashariki, Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu pamoja na Baraza la Kipapa kwa Ajili ya Makleri, kwa pamoja wameandaa mkutano wa kimataifa unaowashirikisha Maparoko 300 walioteuliwa na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki toka sehemu mbalimbali za dunia, kushiriki mkutano maalum kuanzia tarehe 28 Aprili hadi tarehe 2 Mei 2024 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Maparoko Kwa Ajili ya Sinodi. Mkutano wa Kimataifa.” Lengo ni kuendelea kujenga utamaduni wa kusikiliza, kusali na kufanya mang’amuzi ya pamoja kutoka katika Makanisa mahalia. Hii ni sehemu ya utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na Mababa wa Sinodi kuhakikisha kwamba, mchakato huu, unawahusisha: mashemasi, mapadre na maaskofu, ili kusikiliza sauti na mchango wao. Mkutano huu umejikita katika mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa kusikilizana, sera na mikakati ya shughuli za kichungaji, majadiliano na wataalam pamoja na maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa. Uteuzi wa Maparoko wanaoshiriki katika Maadhimisho haya ni kama ule uliotumika kwa ajili ya kuwachagua wajumbe wa Sinodi ya Maaskofu iliyofanyika mwezi Oktoba 2023. Maparoko walioteuliwa ni wale wenye mchango mkubwa katika kukuza na kudumisha Kanisa la Kisinodi katika medani mbalimbali za maisha na utume wa Kanisa. Maparoko hawa watapata fursa ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Matunda ya kazi hii ya Maparoko kutoka sehemu mbalimbali za dunia, yatachangia kutengeneza Hati ya Kutendea Kazi, “Instrumentum laboris” katika Maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu 2021-2024, itakayofikia kilele chake mwezi Oktoba 2024.

Maparoko kwa ajili ya Sinodi. Mkutano wa Kimataifa
Maparoko kwa ajili ya Sinodi. Mkutano wa Kimataifa

Baba Mtakatifu Francisko mwanzoni kabisa mwa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu 2021-2024, Jumamosi tarehe 9 Oktoba 2021, alitoa hotuba elekezi, ambayo ni msingi wa maadhimisho ya Sinodi katika hatua mbalimbali za maisha na utume wa Kanisa kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Watu wa Mungu wakajitambua kuwa wao ni sehemu ya Kanisa la Kisinodi, tayari kutangaza na kushuhudia Ufalme wa Kristo Yesu, kwa kushirikiana na binadamu wote, kusikiliza kwa makini kile ambacho Roho Mtakatifu anataka kuyaambia Makanisa. Huu ni wakati wa kuanza tena kufanya hija hii ya kitume, kama mwendelezo wa Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu iliyozinduliwa kunako mwaka 2021 na itafikia kilele chake Mwezi Oktoba 2024. Hii ni sehemu ya barua kutoka katika Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu kama sehemu ya maandalizi kwa ajili ya Kanisa la Kisinodi na Kimisionari hatua muhimu kuelekea Sinodi ya Mwaka 2024. Sekretarieti kuu ya Sinodi imekwisha kuchapisha mwongozo utakaotumika katika Maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu.

Kwa ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume
Kwa ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume

Kardinali Lazzaro You Heung-sik, “Yu Hung Shik” Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Makleri, katika salam zake kwa Maparoko wanaohudhuria mkutano huu, amekazia umuhimu wa kusali kila siku, kusikiliza na kuhudumia, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu, kielelezo cha ushuhuda wa furaha ya Injili, tayari kuimwilisha katika maisha na utume wa Kipadre. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanakazia pamoja na mambo mengine umuhimu wa Kanisa linalofumbatwa katika: Fumbo, Ushirika na Utume, changamoto na mwaliko kwa waamini kuendelea kulitafakari Fumbo la Kanisa, kwa kuendelea kujielekeza katika umisionari unaowashirikisha watu wote wa Mungu katika maisha na utume wa Kanisa. Hii ndiyo dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Ushirika na utume ni dhamana inayomwilishwa katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, kwa watu wote wa Mungu kuweza kutembea bega kwa kwa bega katika umoja na ushirika. Huu ndio mtindo wa maisha na utume wa Kisinodi, unaowashirikisha wabatizwa wote katika Kanisa, kila mtu akitekeleza dhamana na wajibu wake. Huu ni wajibu mkubwa ambao Roho Mtakatifu amewakabidhi wachungaji wa Kanisa, ili Parokia ziweze kuwa ni mahali pa kushiriki maisha, tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka anayetembea bega kwa bega na waja wake.

Ujenzi wa utamaduni wa kusikilizana na kufanya mang'amuzi ya pamoja
Ujenzi wa utamaduni wa kusikilizana na kufanya mang'amuzi ya pamoja

Kwa upande wake, Kardinali Mario Grech, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu ameelezea umuhimu wa Kanisa mahalia kuwa ni sehemu ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu anatembea bega kwa bega na waja wake katika furaha, majonzi, matumaini na hali ya kukata na kujikatia tamaa; kifo na maisha. Lakini ikumbukwe kwamba, haya ni matokeo ya historia ya maisha ya mwanadamu ambayo Mwenyezi Mungu anaendelea kuiandika bado katika maisha ya waja wake, parokiani, majimboni na katika jamii ya binadamu katika ujumla wake. Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa ni kutembea pamoja na Mwenyezi Mungu, anayetembea na waja wake. Ni sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, ambalo linatembea pamoja na Kristo Yesu, kama sehemu ya utekelezaji wa historia ya Mungu katika maisha ya mwanadamu na kama sehemu ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Ikumbukwe kwamba, Paroko kimsingi ni mtu wa watu kwa ajili ya watu wa Mungu, ambaye yuko tayari kusoma barua kutoka kwa Kristo Yesu iliyoandikwa na Roho Mtakatifu. Parokia ni mahali muafaka pa uinjilishaji wa kina na kwamba, mkutano huu ni fursa kwa Maparoko kushirikisha mang’amuzi na uzoefu wao.

Maparoko na Sinodi
30 April 2024, 15:47