Tafuta

Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, tarehe 8 Aprili 2024 limechapisha Tamko kuhusu: “Utu Usio na Kikomo, Tamko Juu ya Utu wa Mwanadamu” Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, tarehe 8 Aprili 2024 limechapisha Tamko kuhusu: “Utu Usio na Kikomo, Tamko Juu ya Utu wa Mwanadamu”   (Copyright Marlon Lopez MMG1design. All rights reserved.)

Baraza la Kipapa: "Utu Usio na Kikomo, Tamko Juu ya Utu wa Mwanadamu."

Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, tarehe 8 Aprili 2024 limechapisha Tamko kuhusu: “Utu Usio na Kikomo, Tamko Juu ya Utu wa Mwanadamu” “Declaration “Dignitas Infinita” On Human Dignity.” Hili ni tamko ambalo limefanyiwa kazi kwa muda wa miaka mitano na linahusisha mamlaka fundishi ya Kanisa “Magisterium” katika kipindi cha miaka kumi iliyopita: Umaskini, vita, biashara ya binadamu, mifumo ya utumwa mamboleo na nyanyaso kidijitali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Msingi wa hadhi, utu na heshima ya mwanadamu ni Mungu mwenyewe aliyependa kumwuumba mwanadamu kwa sura na mfano wake. Hadhi, utu, heshima na thamani ya Mwanadamu vipo katika asili yake babisa, siyo kitu anachopewa na mtu yeyote yule. Ni Mungu ambaye amependa kumshirikisha mwanadamu umungu wake na utakatifu wake. Na ndiyo maana mwanadamu safi, kwa msukumo wa kiu ya ndani ya roho, daima hujibidiisha kutafuta Muungano na Muumba wake. Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, tarehe 8 Aprili 2024 limechapisha Tamko kuhusu: “Utu Usio na Kikomo, Tamko Juu ya Utu wa Mwanadamu” “Declaration “Dignitas Infinita” On Human Dignity.” Hili ni tamko ambalo limefanyiwa kazi kwa muda wa miaka mitano na linahusisha mamlaka fundishi ya Kanisa “Magisterium” katika kipindi cha miaka kumi iliyopita. Hili ni Tamko linalojikita katika kanuni msingi za utu, heshima na haki msingi za binadamu. Orodha ya mambo yanayokiuka utu wa binadamu ikiwa ni pamoja na umaskini, vita, biashara haramu ya binadamu na mifumo ya utumwa mamboleo. Utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za utoaji mimba na upandikizaji wa mimba, “In Vitro Fertilization (IVF)” ambao kimsingi ni mchakato wa kuunganisha yai la mwanamke na mbegu za mwanaume nje ya mwili wa binadamu katika maabara na kisha kurudishwa kwenye mwili wa mwanamke ili mimba ikue. Itikadi za kijinsia na uhalifu kwa njia ya kidijitali.

Vita ni kati ya mambo yanayosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu
Vita ni kati ya mambo yanayosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu

Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa linafanya rejea katika Tamko la Haki za Binadamu Duniani (The Universal Declaration of Human Rights, 1948, UDHR) lililotiwa mkwaju tarehe 10 Desemba 1948 na Mataifa yakakubaliana kulinda haki msingi za binadamu hasa haki ya kuishi ambayo ndiyo msingi wa haki nyingine zote. Tamko hili ni matokeo ya tafakari ya kina iliyofanywa na viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuhusu: Athari zilizokuwa zimesababishwa na Vita kuu ya kwanza na ile ya Pili ya dunia; ambapo kuna watu wengi walipoteza maisha na mali; utu na heshima yao vikawekwa rehani. Walitaka kuweka kanuni msingi ambazo zimengefuatwa na Jumuiya ya Kimataifa. Hizi ni haki ambazo zinafumbatwa katika uhuru, haki na amani duniani. Huu ni urithi wa binadamu wa nyakati zote na mahali pote bila ubaguzi, kwani zinapata chimbuko lake kutoka kwa binadamu mwenyewe aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba ni sehemu ya asili ya binadamu. Mambo yanayosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu ni pamoja na: Utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za utoaji mimba na kifo laini pamoja upandikizaji mimba; sanjari na ulinzi na usalama wa maskini, wakimbizi na wahamiaji.

Eutanasia ni kinyume cha haki msingi za binadamu: haki ya kuishi
Eutanasia ni kinyume cha haki msingi za binadamu: haki ya kuishi

Mama Kanisa kadiri ya mwanga wa Injili anakiri na kutangaza utu, heshima na haki msingi za binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; kumbe wito wa binadamu ni ushirika la Muumba wake. Utu wa binadamu unawakumbatia na kuwaambata wote; watoto ambao hawajazaliwa bado, wazee, walemavu na watu wote bila ubaguzi.  Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa linaorodhesha vitendo vinavyosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu: mauaji ya kimbari, sera za utoaji mimba na kifo laini pamoja na kifo cha mtu kujinyonga. Mambo mengine ni pamoja na biashara kongwe ya utumwa, biashara ya ngono, biashara ya binadamu na viungo vyake; mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo pamoja na adhabu ya kifo inayokwenda kinyume cha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Umaskini ni kati ya mambo yanayosigina utu wa binadamu katika ulimwengu mamboleo na kwamba, dhana ya vita ya haki na halali imepitwa na wakati na kwamba, mauaji ya wanawake ni vitendo vya kinyama. Huduma za tiba shufaa (Palliative care) inatiliwa mkazo na kwamba, maisha ni haki ya mtu na wala si kifo, kumbe, maisha hayana budi kuhudumiwa kikamilifu.

Mauaji ya kimbari ni kusigina utu, heshima na haki msingi za binadamu
Mauaji ya kimbari ni kusigina utu, heshima na haki msingi za binadamu

Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa linajadili pia nadharia ya jinsia na kuwataka waamini kuachana na tabia ya kuwabagua, kuwanyanyasa na kuwadhalilisha "mashoga na wasagaji" kutokana na mielekeo yao ya kijinsia. Tamko hili linashutumu nadharia ya jinsia inayokumbatiwa na ukoloni wa kiitikadi, unaopania kufuta tofauti za kijinsia kati ya mwanaume na mwamke. Ikumbukwe kwamba, tofauti za kijinsia ni amana na utajiri kutoka kwa Mwenyezi Mungu, unaowataka watu kukamilishana na kwa ajili ya huduma. Ubadilishaji wa jinsi ni hatari inayotishia utu, heshima na haki msingi za binadamu, zinazopaswa kuheshimiwa, kulindwa na kuendelezwa tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi kifo kinapomkuta kadiri ya mapenzi ya Mungu. Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa linabainisha mifumo mipya ya ukatili na udhalilishaji wa kimtandao, kwa kuchapisha picha chafu za ngono. Michezo ya kamari na upatu ni donda ndugu linaloendelea kusababisha maafa na majanga makubwa katika maisha ya watu sehemu mbali mbali za dunia. Mchezo wa kamari na upatu ni matokeo ya myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa. Kamari ni dhambi kubwa inayopukutisha maisha ya watu na kudhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu na hivyo kuwa ni chachu ya rushwa, ufisadi na kizingiti katika ustawi, maendeleo fungamani na mafao ya wengi. Hii ni michezo ambayo inaanza kuingia kwa kasi katika mitandao ya kijamii. Kumbe, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapewa kipaumbele cha kwanza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi katika mifumo yote ya kisheria.

Utu wa Binadamu
08 April 2024, 14:31