Askofu mkuu Henryk Mieczysław Jagodziński, Balozi wa Vatican Afrika ya Kusini na Lesotho
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu Henryk Mieczysław Jagodziński, kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Afrika ya Kusini na Lesotho. Kabla ya uteuzi huu alikuwa ni Balozi wa Vatican nchini Ghana. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Henryk Mieczysław Jagodziński alizaliwa tarehe Mosi, Januari 1969 huko Małogoszcz, nchini Poland. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 3 Juni 1995 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre na Askofu Kazimierz Ryczan wa Jimbo Katoliki la Kielce. Baada kufanya utume wake wa Kipadre Parokiani kwa muda wa miaka miwili, alipelekwa na Jimbo lake kujiendeleza kwa masomo Chuo Kikuu cha Kipapa cha “Santa Croce” kilichoko mjini Roma na kujipatia shahada ya Uzamivu katika Sheria za Kanisa.
Tarehe 1 Julai 2001 akajiunga na utume wa diplomasia ya Kanisa na kupelekwa nchini Belarus kati ya mwaka 2001 hadi mwaka 2005; Croatia kati ya Mwaka 2005 hadi mwaka 2008 na baadaye akahamishiwa kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican, Idara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Kati ya Mwaka 2015 hadi mwaka 2018 akatumwa nchini India na baadaye Bosnia na Herzegovina kati ya mwaka 2018 hadi tarehe 3 Mei 2020 alipoteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu mkuu na Balozi wa Vatican nchini Ghana na hatimaye, kuwekwa wakfu kuwa Askofu mkuu tarehe 18 Julai 2020. Tarehe 16 Aprili 2024, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Balozi wa Vatican nchini Afrika ya Kusini na Lesotho. Ni mwandishi mzuri wa makala na vitabu.