Tafuta

Kardinali Raniero Cantalamessa Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa, katika tafakari yake ya tatu ya Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2024, amejikita katika utambulisho wa Kristo Yesu: Mchungaji Mwema. Kardinali Raniero Cantalamessa Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa, katika tafakari yake ya tatu ya Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2024, amejikita katika utambulisho wa Kristo Yesu: Mchungaji Mwema.  (Vatican Media)

Mahubiri ya Kardinali Cantalamessa Kipindi cha Kwaresima: Mchungaji Mwema

Kardinali Cantalamessa Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa, katika tafakari yake ya tatu ya Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2024, amejikita katika utambulisho wa Yesu anayesema: Yeye ni mchungaji mwema: Sifa za mchungaji mwema ni mwaliko wa kuzama katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu bila woga bali kwa ujasiri, ari na moyo mkuu na kwamba, Mwenyezi Mungu ni kimbilio lao na kuwa Mungu yuko pamoja na waamini wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Mahubiri ya Kipindi cha Kwaresima yanayotolewa na Kardinali Raniero Cantalamessa Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa kwa mwaka 2024 yananogeshwa na kauli mbiu “Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? Mt 16:15. Huu ni mwaliko kwa kila mwamini binafsi kutoa jibu muafaka kadiri ya mwanga wa Injili iliyoandikwa na Yohane: Mimi ni mkate wa uzima ule uliotoka mbinguni.; Mimi ni nuru ya ulimwengu, Mimi ni mchungaji mwema, Mimi ndimi huo ufufuo na uzima! Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2024 unanogeshwa na kauli mbiu “Kupitia Jangwani Mungu Anatuongoza Kwenye Uhuru: Mimi ni BWANA, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa.” Kut 20:2. Baba Mtakatifu katika ujumbe huu, anakazia zaidi wito wa ukombozi kutoka utumwani, ili kukutana na Mwenyezi Mungu, huku wakiacha nyuma yao kongwa la utumwa, mwaliko kwa Kipindi hiki cha Kwaresima ni kufungua macho yao ili kujionea wenyewe hali halisi. Katika safari ya kutoka utumwani, ni Mwenyezi Mungu anayeona, ongoza na kuwakirimia waja wake uhuru kamili. Kwaresima ni mwaliko wa kutambua ukuu wa Mungu, toba, wongofu wa ndani sanjari na kuambata uhuru na kwamba, haya ni mapambano ya jangwa la maisha ya kiroho. Kwaresima ni kipindi cha kujizatiti katika sala na matendo ya huruma kama ilivyokuwa kwa yule Msamaria mwema, tayari kumwilisha wema, huruma na upendo wa Mungu kwa watu waliojeruhiwa: kiroho na kimwili. Ni kipindi cha kujikita katika utekelezaji wa maamuzi ya kijumuiya. Itakumbukwa kwamba, mihimili mikuu ya Kipindi cha Kwaresima ni: Kufunga, Sala, Tafakari ya Neno la Mungu sanjari na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Kristo Yesu ndiye Mchungaji mwema
Kristo Yesu ndiye Mchungaji mwema

Ni katika muktadha huu, Mahubiri ya Kipindi cha Kwaresima yanayotolewa na Kardinali Raniero Cantalamessa Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa kwa mwaka 2024 yananogeshwa na kauli mbiu “Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? Mt 16:15. Huu ni mwaliko kwa kila mwamini binafsi kutoa jibu muafaka kadiri ya mwanga wa Injili iliyoandikwa na Yohane: Mimi ni mkate wa uzima ule uliotoka mbinguni. Mtu yeyote akiula mkate huu, ataishi milele. Mkate huu ni mwili wangu, ambao nitautoa kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.” Yn 6:51. “Basi Yesu akawaambia tena akasema, Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.” Yn 8:12. “Mimi ni mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake. Mtu wa kuajiriwa ambaye si mchungaji, na wala kondoo si mali yake, anapoona mbwamwitu anakuja, huwaacha kondoo na kukimbia, kisha mbwamwitu huwakamata na kuwatawanya. Yeye hajali kitu juu ya kondoo kwa sababu yeye ni mtu wa mshahara tu. Mimi ni mchungaji mwema. Nawajua walio wangu, nao walio wangu wananijua mimi, kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Mimi nayatoa maisha yangu kwa ajili yao.” Yn 10: 11-15.

Kristo Yesu ni Mkate wa uzima wa milele
Kristo Yesu ni Mkate wa uzima wa milele

Kardinali Raniero Cantalamessa Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa, katika tafakari yake ya tatu ya Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2024, amejikita katika utambulisho wa Kristo Yesu anayesema kwamba, Yeye ni mchungaji mwema: Sifa za mchungaji mwema ni mwaliko wa kuzama katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu bila woga bali kwa ujasiri, ari na moyo mkuu na kwamba, Mwenyezi Mungu ni kimbilio lao na kuwa Mungu yuko pamoja na waamini wake. Kristo Yesu katika Agano Jipya anawaambia Mitume wake, ikiwa kama kati yao kuna mtu anataka kuwa “Mchungaji” au Kiongozi lazima awe mnyenyekevu na mtumishi wa wote. Rej. Lk. 22:25. Katika Injili kama ilivyoandikwa na Yohane, 10: 1-19 Kristo Yesu, anataja na kupembua sifa za Mchungaji mwema kuwa ni: Mlango wa kondoo na kondoo humsikia sauti yake; naye huwaita kondoo wake kwa majina yao, na kuwapeleka nje. Anawaonesha dira na njia ya kufuata kwa maana waijua sauti yake. Kristo Yesu alikuja ulimwenguni ili watu wawe na uzima, kisha wawe nao tele! Kristo Yesu ni mchungaji mwema na anafahamiana na kondoo wake. Anakazia umoja miongoni mwa wanakondoo wake. Baba yake wa mbinguni anampenda, kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, amefunua huruma na upendo wa Baba yake wa milele kwa binadamu.

Kristo Yesu ni Nuru ya uzima wa milele
Kristo Yesu ni Nuru ya uzima wa milele

Kristo Yesu ni utimilifu wa ahadi ya Baba wa milele kwa waja wake kuhusu Mchungaji mwema, anayesadaka maisha yake kwa ajili ya upendo unaomwilishwa katika huduma kwa kuwaondolea dhambi zao, kuwatakasa, kuwaponya magonjwa na kuwalisha wenyewe njaa. Kielelezo hiki cha Kristo Mchungaji mwema, kinapotoshwa sana na vyombo vya mawasiliano ya jamii. Lakini, katika historia mahusiano na mafungamano kati ya mchungaji na kondoo yalisimikwa si tu katika masuala ya kijamii na kiuchumi, lakini walifahamiana kwa dhati kabisa, kiasi hata cha kutambua sauti ya Mchungaji mwema. Hawa katika Agano la Kale walikuwa ni: Wafalme, Makuhani na wakuu wa watu wa Mungu. Lakini pia kwenye msafara wa Mamba, Kenge hakosekani, katika historia ya wokovu kumekuwepo pia wachungaji wabaya. Lakini Mwenyezi Mungu anaahidi kwamba: “Mimi mwenyewe nitawalisha kondoo wangu, nami nitawalaza, asema Bwana MUNGU. Nami nitawatafuta waliopotea, nitawarudisha waliofukuzwa, nitawafunga waliovunjika, nitawatia nguvu wagonjwa; nao wanono na wenye nguvu nitawaharibu; nitawalisha hukumu.” Eze 34:15-16.

Mahubiri ya Kipindi cha Kwaresima 2024: Utambulisho wa Kristo Yesu
Mahubiri ya Kipindi cha Kwaresima 2024: Utambulisho wa Kristo Yesu

Uhusiano kati ya Mchungaji mwema na Kondoo unafafanuliwa na Mtakatifu Agostino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa akisema, “Kwenu ninyi mimi ni Askofu na kati yenu mimi ni Mkristo”: “Vobis sum episcopus, vobiscum sum christianus.” Kumbe kuna haja kwa Mama Kanisa kuyafahamu madonda yake, ili kuwaganga na kuwaponya watoto wake. Kwa vile Mwenyezi Mungu ndiye Mchungaji mkuu, waamini hawana sababu ya kuogopa, kuhusu hali ya maisha yao, wakuu wa ulimwengu huu. “No lite timere! Hakuna sababu ya kuogopa kwani Kristo Yesu ameushinda ulimwengu. Rej. Yn 16:33. Katika Uilimwengu mamboleo, mwanadamu anaelemewa sana na hofu ya yale yaliyoko mbele yake, kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu kabla ya mateso na kifo chake Msalabani. Mk 14:33-34. Lakini Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu anasema “Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.” Yn 28: 20. Uwepo wa Kristo Yesu unajidhihirisha kwa njia ya neema na uwepo wa Roho Mtakatifu. Huu ni mwaliko kwa waamini kujisikia zaidi kuwa ni Kondoo wa Kristo Yesu ambaye ndiye Mchungaji mwema. Kristo Yesu anaendelea kuteseka na wote wanaoelemewa na woga, upweke hasi, magonjwa, dhuluma na nyanyaso, wakimbizi na wahamiaji pamoja na wale wote wanaoathirika kwa vita. Huu ni mwaliko kwa waamini kujitahidi pia kuwa ni wachungaji wema. Kristo Yesu anaendelea kujitwika mabegani mwake, mateso na mhangaiko ya ndugu zake. Kristo Yesu anaendelea kutembea na waja wake, hata kama nyayo za miguu yake hazionekani.

Mchungaji Mwema
08 March 2024, 15:53