Tafuta

Kardinali Raniero Cantalamessa katika mahubiri yake awamu ya tano, Ijumaa tarehe 22 Machi 2024, yamenogeshwa na kauli mbiu “Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Kardinali Raniero Cantalamessa katika mahubiri yake awamu ya tano, Ijumaa tarehe 22 Machi 2024, yamenogeshwa na kauli mbiu “Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima.   (Vatican Media)

Mahubiri ya Kardinali Cantalamessa Kipindi cha Kwaresima: Ufufuo na Uzima

Kardinali Raniero Cantalamessa katika mahubiri yake awamu ya tano, Ijumaa tarehe 22 Machi 2024, yamenogeshwa na kauli mbiu “Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi.” Yn 11:25. Kristo Yesu anawaambia wafuasi wake kwamba, Yeye ndiye njia, ukweli na uzima. Ni Neno wa Baba wa milele, Yeye ni njia, mwaliko wa kumfuasa, kumwamini, kumpenda na kushiriki katika maisha na utume wa kuinjilisha watu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Mahubiri ya Kipindi cha Kwaresima yanayotolewa na Kardinali Raniero Cantalamessa Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa kwa mwaka 2024 yananogeshwa na kauli mbiu “Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? Mt 16:15. Huu ni mwaliko kwa kila mwamini binafsi kutoa jibu muafaka kadiri ya mwanga wa Injili iliyoandikwa na Yohane: Mimi ni mkate wa uzima ule uliotoka mbinguni.; Mimi ni nuru ya ulimwengu, Mimi ni mchungaji mwema, Mimi ndimi huo ufufuo na uzima! Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2024 unanogeshwa na kauli mbiu “Kupitia Jangwani Mungu Anatuongoza Kwenye Uhuru: Mimi ni BWANA, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa.” Kut 20:2. Baba Mtakatifu katika ujumbe huu, anakazia zaidi wito wa ukombozi kutoka utumwani, ili kukutana na Mwenyezi Mungu, huku wakiacha nyuma yao kongwa la utumwa, mwaliko kwa Kipindi hiki cha Kwaresima ni kufungua macho yao ili kujionea wenyewe hali halisi. Katika safari ya kutoka utumwani, ni Mwenyezi Mungu anayeona, ongoza na kuwakirimia waja wake uhuru kamili. Kwaresima ni mwaliko wa kutambua ukuu wa Mungu, toba, wongofu wa ndani sanjari na kuambata uhuru na kwamba, haya ni mapambano ya jangwa la maisha ya kiroho. Kwaresima ni kipindi cha kujizatiti katika sala na matendo ya huruma kama ilivyokuwa kwa yule Msamaria mwema, tayari kumwilisha wema, huruma na upendo wa Mungu kwa watu waliojeruhiwa: kiroho na kimwili. Ni kipindi cha kujikita katika utekelezaji wa maamuzi ya kijumuiya. Itakumbukwa kwamba, mihimili mikuu ya Kipindi cha Kwaresima ni: Kufunga, Sala, Tafakari ya Neno la Mungu sanjari na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Kupitia Jangwani Mungu Anatuongoza Kwenye Uhuru
Kupitia Jangwani Mungu Anatuongoza Kwenye Uhuru

Ni katika muktadha huu, Mahubiri ya Kipindi cha Kwaresima yanayotolewa na Kardinali Raniero Cantalamessa Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa kwa mwaka 2024 yananogeshwa na kauli mbiu “Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? Mt 16:15. Huu ni mwaliko kwa kila mwamini binafsi kutoa jibu muafaka kadiri ya mwanga wa Injili iliyoandikwa na Yohane: Mimi ni mkate wa uzima ule uliotoka mbinguni. Mtu yeyote akiula mkate huu, ataishi milele. Mkate huu ni mwili wangu, ambao nitautoa kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.” Yn 6:51. “Basi Yesu akawaambia tena akasema, Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.” Yn 8:12. “Mimi ni mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake. Mtu wa kuajiriwa ambaye si mchungaji, na wala kondoo si mali yake, anapoona mbwamwitu anakuja, huwaacha kondoo na kukimbia, kisha mbwamwitu huwakamata na kuwatawanya. Yeye hajali kitu juu ya kondoo kwa sababu yeye ni mtu wa mshahara tu. Mimi ni mchungaji mwema. Nawajua walio wangu, nao walio wangu wananijua mimi, kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Mimi nayatoa maisha yangu kwa ajili yao.” Yn 10: 11-15. Kardinali Raniero Cantalamessa katika mahubiri yake awamu ya tano, Ijumaa tarehe 22 Machi 2024, yamenogeshwa na kauli mbiu “Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi.” Yn 11:25. Kristo Yesu anawaambia wafuasi wake kwamba, Yeye ndiye njia, ukweli na uzima. Ni Neno wa Baba wa milele, ni ukweli na amefanyika mwili na kwamba, Yeye ni njia na mwaliko ni kumfuata Yeye na kwamba, hii ni tema inayobeba uzito wa pekee katika Injili kama ilivyoandikwa na Mwinjili Yohane. Kutembea ni mwaliko kwa wafuasi wa Kristo Yesu, ili kumwamini na kumpenda, ili hatimaye, kuweza kushiriki katika maisha na utume wake wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kardinali Cantalamessa katika tafakari yake amekazia kuhusu dhana nzima ya ufuasi, Karamu ya Mwisho na kazi ya Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa la Mwanzo; Karama na Matunda ya Roho Mtakatifu na kwamba, Kristo Yesu ndio huo ufufuo na uzima.

Mimi Ndimi huo ufufuo na uzima.
Mimi Ndimi huo ufufuo na uzima.

Kumfuasa Kristo Yesu ni tema inayobeba uzito wa juu katika Injili kama ilivyoandikwa na Yohane. “Nifuate” Kwa Kigiriki maana yake ni “Akolouthia”. Kristo Yesu anajipambanua kuwa ni njia ambayo wafuasi wake wanapaswa kuifuata kama sehemu ya maisha yao kiasi hata cha kuvumilia mateso na madhulumu ya imani. Kumfuasa Kristo Yesu maana yake ni kumwamini, kumpenda na hatimaye, ni kushiriki katika maisha na utume wake wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Huu ni ufuasi unaojikita katika huduma makini kwa watu wa Mungu. Kuna watu katika historia ya Kanisa walioamua kweli kumfuasa Kristo Yesu kwa namna ya pekee kabisa. Hawa ni akina Mtakatifu Benedikto, Ababe, Mtakatifu Dominic, Mtakatifu Francisko wa Assisi, Inyasi wa Loyola pamoja na watakatifu wengi waliotangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya maisha yao matakatifu na adili. Kristo Yesu anawajalia wafuasi wake: Sheria, Neema ya imani inayoganga na kuponya. Kristo Yesu, siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, wakati wa Karamu ya Mwisho, aliwausia wanafunzi wake kuhusu: Kazi, dhamana na utume wa Roho Mtakatifu katika Kanisa la Mwanzo: “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.” Yn 16:13. Huu ni mwaliko kwa waamini kufuata ushauri wa Roho Mtakatifu, ili waweze kuwa watakatifu, huku wakitekeleza mapenzi ya Mungu kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Mama Theresa wa Calcutta tarehe 10 Septemba 1946 akiwa njiani kuelekea mjini Darjeeling akasikia sauti ikimwambia ndani mwake: “nina kiu” na hivyo akayakumbuka maneno ya Kristo Yesu pale Msalabani! Haya ni maneno ambayo yataendelea kuandikwa kwenye nyumba zote zilizoanzishwa na Mama Theresa wa Calcutta, kama muasisi wa Shirika la Wamisionari wa Upendo na kwamba huduma ya upendo ni utambulisho na karama yao! Tarehe 16 Agosti 1948 akaondoka kutoka katika Shirika la Bikira Maria wa Loreto, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini na watu waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii.

Mama Theresa wa Calcutta ni mfano wa Msamaria mwema.
Mama Theresa wa Calcutta ni mfano wa Msamaria mwema.

Mpango wa Mungu umebadili maisha ya watu wengi katika historia ya wokovu kama Mzee wetu wa imani Abrahamu, pamoja na Musa Mtumishi mwaminifu wa Mungu. Kardinali Cantalamessa anasema, karama ya unabii inapaswa kusindikizwa na mang’amuzi na kwamba, watu watawatambua kwa matunda yao ambayo kimsingi ni kazi ya Roho Mtakatifu. Mang’amuzi hayawezi kwenda kinyume cha mapenzi ya Mungu kama yanavyofafanuliwa kwenye Maandiko Matakatifu, Mafundisho ya Kanisa; Kanuni, maadili na utu wema. Mtakatifu Paulo, Mtume wa Mataifa anabainisha kwamba: Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria. Rej. Gal 5: 22. Ni kweli kwamba, katika mazoezi, mambo ni magumu zaidi. Msukumo unaweza kutoka kwa Mungu na bado kusababisha usumbufu mkubwa. Lakini hii haitokani na uvuvio ambao ni mtamu na wa amani kama kila kitu kitokacho kwa Mungu; badala yake, inatokana na upinzani dhidi ya msukumo au kutokana na ukweli kwamba inatuomba kitu ambacho hatuko tayari kutoa. Ikiwa msukumo unakaribishwa, moyo haraka hujikuta katika amani kuu. Mungu hulipa kila ushindi mdogo katika uwanja huu, na kuifanya nafsi kuhisi kibali chake, ambayo ni furaha safi zaidi iliyopo duniani. Kardinali Raniero Cantalamessa katika mahubiri yake awamu ya tano, anasema, lengo la tafakari za kipindi hiki cha Kwaresima ni kupyaisha undani wa maisha ya mwamini kwa mwanga na maongozi ya Roho Mtakatifu, ili kuweza kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha. Ikiwa kukaribisha maongozi ni muhimu kwa kila Mkristo, ni muhimu kwa wale walio na majukumu ya kuongoza katika Kanisa. Ni kwa njia hii tu Roho wa Kristo anaruhusiwa kuliongoza Kanisa lake kupitia wawakilishi wake wa kibinadamu. Ni kwa njia ya maongozi ya Kimungu yaliyokubaliwa kwa ujasiri na Mtakatifu Yohane XXIII Mtaguso wa Pili wa Vatican uliweza kuadhimishwa na kwa njia hiyo hiyo, ishara nyingine za kinabii ziliweza kuzaliwa baadaye, ambazo zitaendelea kutambuliwa na vizazi vijavyo. Maadhimisho ya Pasaka ya Mwaka huu yawajalie waamini kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu Mshindi anayesema, “Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi.” Yn 11:25.  

Kwaresima 2024
22 March 2024, 14:34