Tafuta

Maadhimisho ya Siku ya Wahispania Wanaofanya Utume wao huko Amerika ya Kusini “Día de Hispanoamérica” inaadhimishwa tarehe 3 Machi 2024. Maadhimisho ya Siku ya Wahispania Wanaofanya Utume wao huko Amerika ya Kusini “Día de Hispanoamérica” inaadhimishwa tarehe 3 Machi 2024. 

Maadhimisho ya Siku ya Wahispania Wanaofanya Utume Wao Amerika ya Kusini

Maadhimisho ya Siku ya Wahispania Wanaofanya Utume wao huko Amerika ya Kusini “Día de Hispanoamérica” inaadhimishwa tarehe 3 Machi 2024, ili kuonesha moyo wa shukrani kutoka kwa Kanisa kwa ajili ya Mapadre wa Majimbo kutoka Hispania wanaotekeleza wito na utume wao huko Amerika ya Kusini. Muungano huu wa Mapadre kutoka Hispania “OCSHA” ulianzishwa kunako mwaka 1949. Kauli mbiu: Wanathubutu Kuhatarisha Maisha yao kwa Ajili ya Injili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya Wahispania Wanaofanya Utume wao huko Amerika ya Kusini “Día de Hispanoamérica” inaadhimishwa tarehe 3 Machi 2024, ili kuonesha moyo wa shukrani kutoka kwa Mama Kanisa kwa ajili ya Mapadre wa Majimbo kutoka Hispania wanaotekeleza wito na utume wao huko Amerika ya Kusini. Muungano huu wa Mapadre kutoka Hispania “OCSHA” ulianzishwa kunako mwaka 1949. Kumbe, hii ni siku ya sala, tafakari pamoja na kukusanya michango mbalimbali kwa ajili ya kuenzi maisha na utume wa Mapadre kutoka Hispania wanaoendelea kusadaka maisha yao kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili katika nchi za Amerika ya Kusini. Ujumbe wa Kardinali Robert Francis Prevost, O.S.A., Rais wa Tume ya Kipapa Kwa Ajili ya Amerika ya Kusini katika maadhimisho haya unanogeshwa na kauli mbiu “Wanathubu kuhatarisha maisha yao kwa ajili ya Injili.”  Hawa ni wale Mapadre ambao wamepokea wito huu kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na wito huu, wanapenda kuwashirikisha watu wa Mungu, lakini kwa namna ya pekee kabisa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii, ili kuambata na kukumbatia upendo wenye huruma kutoka kwa Kristo Yesu, anayewaalika Mapadre kujisadaka kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu wote. Mtakatifu Oscar Armulfo Romero ni shuhuda wa Injili ya Kristo Yesu, anayewakumbusha wakristo kwamba, wanapaswa kuwa ni wafiadini, yaani mashuhuda wa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Waamini wanatumwa kutangaza na kushuhudia ujumbe wa ukombozi, unaowaweka wote huru kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti.

Daraja Takatifu ya Upadre ni zawadi kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu
Daraja Takatifu ya Upadre ni zawadi kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu

Mtakatifu Oscar Romero ni mfano wa mchungaji mwema aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake kwa njia ya huduma kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Huu ni mwaliko wa kupambana na ubaya wa dhambi, ili kweli ulimwengu uweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Mtakatifu Oscar Armulfo Romero katika maisha na utume wake, alipenda kukazia zaidi: upendo kwa Mungu na jirani; toba na wongofu wa ndani na kwamba, upendo kwa Kristo Yesu, iwe ni chachu kwa waamini hata kuthubutu kuhatarisha maisha yao kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Hii ni changamoto ya kuthubutu kutoka katika fahari na utukufu wa kisiasa, kiuchumi na kijamii; kwa maneno machache ni kujiondoa kutoka katika malimwengu, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Siku ya Wahispania wanaoishi na kutekeleza wajibu wao Amerika ya Kusini.
Siku ya Wahispania wanaoishi na kutekeleza wajibu wao Amerika ya Kusini.

Kardinali Robert Francis Prevost, O.S.A., Rais wa Tume ya Kipapa Kwa Ajili ya Amerika ya Kusini anahitimisha ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku ya Wahispania Wanaofanya Utume wao huko Amerika ya Kusini “Día de Hispanoamérica” kwa kuwaweka Mapadre hawa chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Guadalupe, ili aweze kuwaombea kutoka kwa Kristo Yesu: Upendo na Ujasiri wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mungu Amerika ya Kusini. Takwimu zinaonesha kwamba, hadi mwaka 2024 kuna Mapadre 140 kutoka nchini Hispania wanaotekeleza dhamana na wajibu wao huko Amerika ya Kusini. Idadi kubwa ya Mapadre kwa Mwaka 2023 ni wale waliotoka katika Majimbo ya Madrid na Toledo na hawa walitumwa nchini Mexico na Perù. Mwaka 2023 watu wa Mungu kutoka Hispania walichangia jumla ya Euro 60, 000 kwa ajili ya kugharimia miradi mbalimbali ya maendeleo huko Amerika ya Kusini. Itakumbukwa kwamba, kuna baadhi ya majimbo yanayochangia moja kwa moja katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu huko Amerika ya Kusini.

Siku ya Mapadre wa Kihispania

 

 

03 March 2024, 15:24