Tafuta

Ishara ya haki. Pasipo haki hakuna amani ya kudumu. Ishara ya haki. Pasipo haki hakuna amani ya kudumu. 

Vatican:uhuru wa kidini uliokiukwa ni karibu theruthi ya Nchi duniani!

Katika Kikao cha 55 cha Baraza la Haki za Kibinadamu kinachoendelea huko Geneva,Askofu Mkuu Balestrero,Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,alionesha hofu kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu duniani na kusisitiza kwamba katika mchakato wa maamuzi na katika diplomasia ya kimataifa ni muhimu kuweka hadhi ya binadamu katikati.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Desemba iliyopita tuliadhimisha kumbukumbu ya miaka 75 tangu kupitishwa kwa Azimio la Kimataifa la Haki za Kibinadamu. Hili lilikuwa hatua muhimu katika kuweka kiwango cha kimataifa cha haki za kimsingi za binadamu na uhuru. Ndivyo alianza hotuba yake  Askofu Mkuu Balestrero, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican katika  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika Kikao cha 55 cha Baraza la Haki za Kibinadamu kinachoendelea huko Geneva, Uswiss. Katika hotuba hiyo, Mwakilishi wa Vatican alibainisha wasiwasi kwamba ukiukwaji wa haki za binadamu bado unatokea duniani kote licha ya kupita kwa wakati, ikiwa ni pamoja na wale wanaopinga uhuru wa mawazo, dhamiri na dini. Ubaguzi na mateso kwa waamini yanazidi kuongezeka. Uhuru wa kidini unakiukwa katika karibu thuluthi moja ya nchi za ulimwengu, na kuathiri karibu watu bilioni 4.9. Katika baadhi ya nchi za Magharibi, ubaguzi wa kidini na udhibiti unaendelezwa kwa kisingizio cha ‘uvumilivu na ushirikishwaji’. 

Changamoto za kiutamaduni na kijamii

Sheria ambazo awali zililenga kupambana na ‘hotuba ya chuki’, mara nyingi hutumiwa kupinga haki ya uhuru wa mawazo, dhamiri, na dini, na hivyo kusababisha udhibiti na ‘mazungumzo ya kulazimishwa’. “Ulimwengu wetu umekuwa wa pande nyingi na wakati huo huo mgumu sana kwamba mfumo tofauti wa ushirikiano mzuri unahitajika. Tunahitaji kuguswa na mifumo ya kimataifa kwa afya ya umma ya mazingira, changamoto za kiutamaduni na kijamii, hasa ili kujumuisha heshima kwa haki za kimsingi za binadamu. Kama vile Papa Francisko anavyosisitiza mara kwa mara kuwa, “kila kitu kimeunganishwa” na “hakuna anayeokolewa peke yake.”

Umakini wa kutumia akili mnemba

Mwakilishi wa Kudumu katika hotuba hiyo alisema kuwa ili kuboresha diplomasia ya pande nyingi, ni muhimu kuzingatia maadili ambayo yamejikita katika utu wa binadamu. Hili linahitaji kujenga upya maono ya pamoja ya asili yetu ya asili, ambayo inahusisha wajibu na kanuni za maadili ambazo zinaweza kueleweka kupitia akili za kibinadamu na lazima ziheshimiwe. Kimsingi, hatuwezi kutenganisha lililo jema na lililo kweli na ambalo limekita mizizi katika asili yetu ya kibinadamu. Utu wa mwanadamu lazima uwe kanuni elekezi pia katika ukuzaji na utumiaji wa akili Mnemba. Maendeleo katika nyanja hii yanapaswa kuheshimu haki za kimsingi za binadamu na yanapaswa kutumikia, sio kushindana, na uwezo wetu wa kibinadamu. Wanapaswa kukuza, sio kuzuia, uhusiano wa kibinafsi, udugu, fikra makini, na uwezo wa utambuzi. Kuheshimu utu wa binadamu kunahitaji kwamba tukatae jaribio lolote la kupunguza upekee wa binadamu ili kutambuliwa au kupunguzwa kwa mienendo au seti ya  takwimu na kwamba haturuhusu mifumo ya kisasa kuamua hatima ya wanadamu kwa uhuru. Ukuzaji wa akili mnemba unaweza tu kuchukuliwa kuwa na mafanikio ikiwa tutatenda kwa uwajibikaji na kuzingatia maadili ya kimsingi ya binadamu.

Jamii lazima ziinue msingi wa ufahamu wa udugu wa ulimwengu

Mwakilishi wa Vatican aidha alisisitiza kwamba changamoto nyingi tunazokabiliana nazo leo zinatokana na ukosefu wa heshima kwa utu na kushindwa kutambua uhusiano wetu. Hii mara nyingi husababisha matokeo mabaya, ambayo yanaonekana katika jamii yetu. Majaribio ya sasa ya kuanzisha kile kinachoitwa “haki mpya” si mara zote yanaendana na kile ambacho ni kizuri kwa binadamu. Majaribio kama haya yanasababisha “ukoloni wa kiitikadi” ambao unadhoofisha utu wa mwanadamu, na kuunda migawanyiko kati ya tamaduni, jamii, na Mataifa, badala ya kukuza umoja na amani. Jamii zetu “lazima ziendelee kuinuka katika misingi ya ufahamu sahihi wa udugu wa ulimwengu wote na heshima kwa utakatifu wa kila maisha ya mwanadamu, ya kila mwanamume na kila mwanamke, maskini, wazee, watoto, wasio na uwezo, wasio na kazi, walioachwa, wale wanaochukuliwa kuwa wa kutupwa kwa sababu wanazingatiwa tu kama sehemu ya takwimu.” Kanuni za udugu wa kibinadamu na mshikamano zinapaswa kuwa kiini cha kazi yetu tena.

Kikao cha Baraza la jaki za binadamu lishughulikie ukiukwaji wa haki

Udugu umekuwa katika thamani ya msingi ya mfumo wa kimataifa tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa, alisisitiza. "Dibaji na Vifungu vya kwanza vya Mkataba wa mwanzilishi wa Umoja wa Mataifa vinatambua kwamba wanadamu wote wamezaliwa huru na sawa katika utu na haki, na wanapaswa kutenda kwa kila mmoja kwa roho ya udugu. Udugu wa ulimwengu wote ni hali muhimu kwa utambuzi kamili wa haki za binadamu katika ulimwengu wa leo. Tunaposhindwa kukiri kwamba sote tumeunganishwa, sote tunateseka." Na hatimaya alisema kuwa ujumbe wake ni matumaini kwamba "kikao cha Baraza la Haki za Kibinadamu kitabainisha na kushughulikia kwa ukamilifu ukiukwaji unaoendelea wa haki za kimsingi za binadamu, kubainisha sababu za msingi, na kuchukua hatua madhubuti ili kukomesha ukiukwaji huu na ukatili unaosababisha mara nyingi." Ni matumaini kwamba utu na udugu utawaongoza katika majuma haya ya kikao hicho.

29 February 2024, 17:10