Tafuta

Profesa Deogratias Frederick Rutatora, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei Taifa, nchini Tanzania akisalimiana na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 12 Februari 2024. Profesa Deogratias Frederick Rutatora, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei Taifa, nchini Tanzania akisalimiana na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 12 Februari 2024.  (Vatican Media)

Ujumbe wa Mwenyekiti Halmashauri Walei Taifa Nchini Tanzania

Uamuzi wa Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuambatana na wawakilishi wa Waamini Walei Tanzania ikiwa ni pamoja na wawakilishi wa Vyama, Mashirika na Jumuiya za Kitume ambao kwa umoja wao wanaunda Halmashauri ya Walei Tanzania, unaendana na msukumo wa Hati ya Utume wa Walei ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Barua ya Kitume ya Baba Mtakatifu Yohane Paulo II juu ya Wito wa Utume wa Walei sanjari na maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu.

Na Deogratias Frederick Rutatora, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei Taifa, Vatican

Ndugu wapendwa katika Kristo, Tumsifu Yesu Kristo. Kwanza kabisa naomba nichukue nafasi hii ya kipekee kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwezesha Ziara ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Vatican akiwa pamoja na ujumbe wake, kufanikiwa kwa viwango vya hali ya juu. Pili, kwa niaba ya Halmashauri ya Walei Tanzania na kwa niaba ya ujumbe niliombatana nao naomba kwa heshima zote nimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt, Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kuteua wawakilishi wa Walei na Vyama, Mashirika na Jumuiya za Kitume (VMJ) ngazi ya Taifa kuambatana nae katika ziara hii. Katika ziara hii, Mhe. Rais aliambatana na wawakilishi wa Walei wafuatao kutoka Kanisa Katoliki Tanzania: Bi Evaline Malisa Ntenga, Mwenyekiti wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) na Rais wa Wanawake Wakatoliki- Afrika; Profesa Deogratias Frederick Rutatora, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei Taifa; Bw. Leonard Mapolu, Mwenyekiti wa Vijana Wafanyakazi Wakatoliki Tanzania (VIWAWA); Bw. Dalmas Gregory, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei, Zanzibar; na Bi Theresia Paschas Seda, Mwenyekiti wa Utoto Mtakatifu Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Ujumbe wa Tanzania na Baba Mtakatifu Francisko
Ujumbe wa Tanzania na Baba Mtakatifu Francisko

Ndugu wapendwa katika Kristo, uamuzi wa Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuambatana na wawakilishi wa Waamini Walei Tanzania ikiwa ni pamoja na wawakilishi wa Vyama, Mashirika na Jumuiya za Kitume (VMJ); ambao kwa umoja wao wanaunda Halmashauri ya Walei Tanzania, unaendana sambamba na msukumo wa Hati ya Utume wa Walei ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ijulikanayo kama Apostolicam Actuositatem (AA) na Barua ya Kitume ya Baba Mtakatifu Yohane Paulo II juu ya Wito wa Utume wa Walei ijulikanayo kama Christifideles Laici. Hati ya Utume wa Walei ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Barua ya Kitume ya Baba Mtakatifu Yohane Paulo II vinatamka rasmi kuwa Utume wa Walei hauwezi kutoweka kamwe katika Kanisa (AA 1); na kwamba Walei siyo tu wamo ndani ya Kanisa bali vile vile wao ni Kanisa (CL 9). Aidha, Kanisa Katoliki Tanzania linatambua kuwa Uinjilishaji wa Kanisa hauwezi kukamilika bila mchango wa waamini walei, na kwamba Jumuiya Ndogondogo za Kikristo (JNNK) ni moja ya Familia ya Mungu (EA 89). Kwa mantiki hii, azma ya Mhe. Rais, Dkt. Samia kuambatana na wawakilishi wa Waamini walei na Vyama, Mashirika na Jumuiya za Kitume imezingatia miongozo ya Kanisa Katoliki iliyopo.

Ujumbe wa Tanzania ukiwa na Balozi wa Tanzania nchini Italia
Ujumbe wa Tanzania ukiwa na Balozi wa Tanzania nchini Italia

Kwa kuzingatia umuhimu na mchango wa waamini walei, tarehe 12 Februari 2024, Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiwa ameambatana na ujumbe wa watu wasiopungua kumi alitembelea mjini Vatican na kupokelewa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko kwenye ofisi za Papa. Katika Ofisi za Papa, Baba Mtakatifu Francisko alifanya mazungumzo ya faragha na Mhe. Rais, Dkt, Samia; na baadaye Baba Mtakatifu Francisko alikutana na ujumbe mzima wa Rais. Baada ya mkutano na Baba Mtakatifu, Mhe. Rais alikutana na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa kwa ajili ya mazungumzo ya faragha. Katika mazungumzo yao ya faragha yaliyodumu kwa takribani dakika ishirini na tano, wameridhika na uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Tanzania; mchango na dhamana ya Kanisa Katoliki katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Tanzania, hususan katika sekta ya: elimu, afya na ustawi wa jamii pamoja na changamoto ambazo Tanzania inapitia kwa sasa. Baadaye, wamejielekeza zaidi katika masuala ya kijamii nchini Tanzania; masuala ya kikanda na Kimataifa na umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa katika kujikita katika kudumisha amani ulimwenguni.

Maadhimisho ya Sinodi: 30 Septemba Mafungo! 2 Oktoba-27 Oktoba 2024
Maadhimisho ya Sinodi: 30 Septemba Mafungo! 2 Oktoba-27 Oktoba 2024

Ndugu waumini wenzangu pamoja na watu wote wa Mungu, ziara hii ya Mhe. Rais nchini Vatican imefanyika wakati mwafaka kwa kuwa Kanisa Katoliki lipo kwenye kipindi cha Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yananogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume yanayotegemewa kuanza tarehe 30 Septemba 1 Oktoba kwa siku mbili za mafungo ya kiroho kuhitimishwa tarehe 27 Oktoba 2024. Msisitizo mkuu ni watu wote tuwe wasikivu na tutembee pamoja. Katika maadhimisho haya, Baba Mtakatifu anakazia ujenzi wa utamaduni wa kusikiliza, kukutana na kufanya mang’amuzi ya pamoja; matukio haya yakiongozwa na upendo wa dhati. Katika kipindi hiki na baadae sote tunaalikwa kuishi kama kaka na dada au kama ndugu wa familia moja. Kwa ufupi, maana ya Sinodi ni kutembea kwa pamoja au kuwa na mwondoko mmoja kwa pamoja, na wakati mwingine ueleweka kama kusafiri kwa kushikana mikono bila kumwacha yeyote yule nyuma. Kwa kipindi hiki, kila mmoja wetu anaalikwa kuwa mwanaushirika, mshiriki na pia mmisionari wa kuwa shahidi wa Habari Njema ya Wokovu wetu katika nyakati na ulimwengu wetu wa leo.

Jubilei ya Miaka 50 ya Jumuiya Ndogondogo za Kikristo 2023-2024
Jubilei ya Miaka 50 ya Jumuiya Ndogondogo za Kikristo 2023-2024

Aidha, ziara hii ya Mhe. Rais imefanyika wakati Kanisa katika nchi za AMECEA, na Tanzania ikiwa mojawapo, likiwa linajiandaa kusherekea kilele cha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya Ndogondogo za Kikristo (JNNK), maadhimisho ambayo yatahitimishwa Julai, 2024. Azma ya maadhimisho ya JNNK kama ilivyo kauli mbiu ya Kanisa la Kisinodi inatutaka tutembee pamoja, tushiriki na kudumisha upendo, ukarimu, umoja na mshikamano. Ziara ya Mhe. Rais inazingatia tunu msingi tajwa hapo juu na inaendena na matakwa ya Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania inayotutaka tudumishe amani, upendo, umoja na mshikamano. Tunu msingi tajwa hapo juu zipo sambamba na Zaburi (133:1) isemayo “Tazama jinsi ilivyo vyema, na kupendeza, ndugu kuishi pamoja, kwa umoja.”

Omnia vincit amor! Upendo hushinda yote!
Omnia vincit amor! Upendo hushinda yote!

Kwa ujumla ziara ya Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na ujumbe alioambatana nao imepokelewa vizuri tendo ambalo linazidisha kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia kati ya Vatican na Tanzania. Kwa niaba ya wenzangu nilioambatana nao, naomba nichukue fursa ya kipekee kumshukuru Mhe. January Makamba (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kuratibu vyema ziara ya Mhe. Rais na ujumbe wake; na kuhakikisha inafanikiwa kwa viwango vya kimataifa. Aidha, kwa heshima na unyenyekevu mkubwa, naomba nishukuru sana uongozi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa kutupatia ruhusa na baraka zote ili tuweze kushiriki ipasavyo kwenye ziara hii ya aina yake. Daima tutazidi kuomba baraka za Bwana, tumwinulie Mungu akili zetu, ili kwa Roho wake Mtakatifu atutie nguvu katika ushirika, atuongoze kwenye ukweli wote na kuendelea kutuangazia ili nuru yetu izidi kung’ara tupate kuyatakatifuza malimwengu. Mwisho, naomba niwashukuru sana Watanzania waishio Roma na kufanya utume wao mjini Vatican na maeneo mengine ya Italia kwa kutupokea vizuri sana na kuhakikisha ziara ya Mhe. Rais inafana sana. Niombe kuchukua nafasi hii kumshukuru sana Padre Richard A. Mjigwa na Angella Rwezaula kwa ukarimu wao waliotuonesha na kutusaidia kututembeza kwenye viunga vya Ofisi za Radio Vatican. Baba Mjigwa asante sana (grazie mille) na Mungu akuzidishie baraka tele na afya njema. Kweli, “Upendo Hushinda Yote” (Omnia Vincit Amor). Nimalizie kwa kusema: Omnia ad Majorem Dei Gloriam."

Walei Tanzania
20 February 2024, 15:31