Tafuta

Kardinali Raniero Cantalamessa katika tafakari yake ya kwanza ya Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2024, Ijumaa tarehe 23 Februari 2024 amejikita katika utambulisho wa Kristo Yesu Kardinali Raniero Cantalamessa katika tafakari yake ya kwanza ya Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2024, Ijumaa tarehe 23 Februari 2024 amejikita katika utambulisho wa Kristo Yesu  (Vatican Media)

Mahubiri ya Kipindi Cha Kwaresima 2024: Yesu Ni Mkate wa Uzima

Kardinali Raniero Cantalamessa katika tafakari yake ya kwanza ya Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2024, Ijumaa tarehe 23 Februari 2024 amejikita katika utambulisho wa Kristo Yesu kuwa “Yeye ni mkate wa uzima ule uliotoka mbinguni.” Huu ni mwaliko kwa mwamini kuingia katika undani wa maisha tayari kujiinjilisha ili kuweza kuinjilisha, kwa kujazwa na uwepo angavu wa Kristo Yesu, mwingi wa huruma na mapendo, tayari kuungana naye kutoka katika undani wa maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Kwaresima ni kipindi cha kujizatiti katika sala na matendo ya huruma kama ilivyokuwa kwa yule Msamaria mwema, tayari kumwilisha wema, huruma na upendo wa Mungu kwa watu waliojeruhiwa: kiroho na kimwili. Ni kipindi cha kujikita katika utekelezaji wa maamuzi ya kijumuiya. Itakumbukwa kwamba, mihimili mikuu ya Kipindi cha Kwaresima ni: Kufunga, Sala, Tafakari ya Neno la Mungu sanjari na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Ni katika muktadha huu, Mahubiri ya Kipindi cha Kwaresima yanayotolewa na Kardinali Raniero Cantalamessa Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa kwa mwaka 2024 yananogeshwa na kauli mbiu “Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? Mt 16:15. Naye Mtume Petro anamshuhudia akisema “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.” Mt 16:16 Hili ni swali ambalo Kristo Yesu anapenda kumuuliza kila mwamini binafsi. Lakini Mwinjili Yohane, ameufafanua utambulisho wa Kristo Yesu mwenyewe anayesema kwamba, “Yeye ni mkate wa uzima ule uliotoka mbinguni; Yeye ni nuru ya ulimwengu na tena ni mchungaji mwema na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa.”

Mahubiri Kipindi cha Kwaresima: Utambulisho wa Yesu
Mahubiri Kipindi cha Kwaresima: Utambulisho wa Yesu

Kardinali Raniero Cantalamessa katika tafakari yake ya kwanza ya Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2024, Ijumaa tarehe 23 Februari 2024 amejikita katika utambulisho wa Kristo Yesu kuwa “Yeye ni mkate wa uzima ule uliotoka mbinguni.” Huu ni mwaliko kwa mwamini kuingia katika undani wa maisha yake, tayari kujiinjilisha ili kuweza kuinjilisha, kwa kujazwa na uwepo angavu wa Kristo Yesu, mwingi wa huruma na mapendo, tayari kuungana naye kutoka katika undani wa maisha. Kristo Yesu anasema kwamba Yeye ndiye chakula cha uzima; yeye ajaye kwake hataona njaa kabisa, naye amwaminiye hataona kiu kabisa. Baada ya Kristo Yesu kuwashibisha mkutano mkuu wa watu kwa mikate mitano na vipande viwili vya samaki, anachukua fursa hii kuwafafanulia “alama” iliyojificha chini ya muujiza huu, kama alivyojitaabisha kumfafanulia yule Mwanamke Msamaria kuhusu maana ya maji ya uzima kwamba, ni Kristo Yesu mwenyewe aliyekuwa anazungumza naye.

Kristo Yesu ni Mkate wa uzima wa milele
Kristo Yesu ni Mkate wa uzima wa milele

Na kwa umati mkubwa wa watu anawajibu pia kwamba: “Yeye ni mkate wa uzima ule uliotoka mbinguni.” Mababa wa Kanisa wanasema, Kristo Yesu anawalisha waja wake kwa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na kwa Neno la Mungu. Hiki ni chakula kinachorutubisha roho na Neno ambalo ni dira na mwongozo wa maisha; amana na utajiri mkubwa wa Kanisa. Mkate wa uzima wa milele anasema Martin Luther ni Neno la Mungu ambalo Mama Kanisa analigawa kwa njia ya kulitangaza na kulishuhudia na chakula hiki kinaliwa kwa imani. Huu ni muhtasari wa mazingira ya kiekumene yanayofafanua maneno ya Kristo Yesu “Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.” Mt 4:4. Lengo ni kuimarisha uhusiano na mafungamano ya dhati na Kristo Yesu katika mazingira ya kiekumene. Kimsingi Ibada ya Misa Takatifu imegawanyika katika sehemu kuu mbili: Liturujia ya Neno la Mungu inayoundwa na Neno la Mungu kutoka Agano la Kale, Nyaraka za Mitume pamoja na Injili pamoja na Liturujia ya Ekaristi Takatifu, chemchemi ya furaha. Kristo Yesu ni Mkate wa uzima wa milele kwa jinsi alivyo na kwa jinsi anavyojitokeza kuwa ni chakula cha wasafiri huku bondeni kwenye machozi. Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu ni chemchemi ya utakatifu wa maisha unaopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha, ili kuweza kuzaa matunda: “Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi.” Yn 12:24. Huu ni mwaliko wa kuyatakatifuza malimwengu badala ya kugumisha nyoyo kwa chuki, uhasama pamoja na “litania za malalamiko.”

Curia Romana ni mahali pa huduma ya upendo na mshikamano
Curia Romana ni mahali pa huduma ya upendo na mshikamano

Lakini ikumbukwe kwamba, maisha ya kijumuiya ni kitubio kikubwa sana: “Vita communis mortificatio.” Lakini mwisho wa siku, waamini wanapaswa kuwa waaminifu na wa kweli katika maisha na wito wao. Wafanyakazi wa Sekretarieti kuu ya Vatican wanazo fursa na nafasi nyingi katika mchakato wa kujitakatifuza kwa njia ya huduma. “Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi. Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu.” Kol 3: 12 – 13. Waamini wajenge na kudumisha nia njema katika kufikiri na kutenda. Waamini wajitaabishe kujifahamu jinsi walivyo, wajitahidi kujishusha kwa njia ya unyenyekevu na kwa kwamba, wanapewa fursa ya kujishusha kwa njia ya unyekevu kama sehemu muhimu sana ya kujitakasa na kujitakatifuza na kwamba, ukweli utawaweka huru kama ulivyo mchakato wa kutengeneza mkate, ambao ndio unaounda Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa, changamoto ya waamini kupendana, kuimarishana katika imani na upendo usiogawanyika. Kardinali Raniero Cantalamessa Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa amehitimisha mahubiri yake ya kwanza kwa Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2024 kwa kutoa mwaliko kwa waamini kumwendea Kristo Yesu kwani “Ni chakula kishukacho kutoka mbinguni, kwamba mtu akile wala asife. Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.” Yn 6:50-51. Ni kwa njia hii, waamini wataweza kujenga upendo, mahusiano na mafungamano ya dhati na Kristo Yesu, Mkate ulioshuka kutoka mbinguni!

Mahubiri Kwaresima
23 February 2024, 14:48