Kardinali Cantalamessa: Mahubiri ya Kwaresima Kwa Mwaka 2024
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2024 unanogeshwa na kauli mbiu “Kupitia Jangwani Mungu Anatuongoza Kwenye Uhuru: Mimi ni BWANA, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa.” Kut 20:2. Baba Mtakatifu katika ujumbe huu, anakazia zaidi wito wa ukombozi kutoka utumwani, ili kukutana na Mwenyezi Mungu, huku wakiacha nyuma yao kongwa la utumwa, mwaliko kwa Kipindi hiki cha Kwaresima ni kufungua macho yao ili kujionea wenyewe hali halisi. Katika safari ya kutoka utumwani, ni Mwenyezi Mungu anayeona, ongoza na kuwakirimia waja wake uhuru kamili. Kwaresima ni mwaliko wa kutambua ukuu wa Mungu, toba, wongofu wa ndani sanjari na kuambata uhuru na kwamba, haya ni mapambano ya jangwa la maisha ya kiroho.
Kwaresima ni kipindi cha kujizatiti katika sala na matendo ya huruma kama ilivyokuwa kwa yule Msamaria mwema, tayari kumwilisha wema, huruma na upendo wa Mungu kwa watu waliojeruhiwa: kiroho na kimwili. Ni kipindi cha kujikita katika utekelezaji wa maamuzi ya kijumuiya. Itakumbukwa kwamba, mihimili mikuu ya Kipindi cha Kwaresima ni: Kufunga, Sala, Tafakari ya Neno la Mungu sanjari na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Ni katika muktadha huu, Mahubiri ya Kipindi cha Kwaresima yanayotolewa na Kardinali Raniero Cantalamessa Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa kwa mwaka 2024 yananogeshwa na kauli mbiu “Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? Mt 16:15. Huu ni mwaliko kwa kila mwamini binafsi kutoa jibu muafaka kadiri ya mwanga wa Injili iliyoandikwa na Yohane: Mimi ni mkate wa uzima ule uliotoka mbinguni. Mtu yeyote akiula mkate huu, ataishi milele. Mkate huu ni mwili wangu, ambao nitautoa kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.” Yn 6:51.
“Basi Yesu akawaambia tena akasema, Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.” Yn 8:12. “Mimi ni mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake. Mtu wa kuajiriwa ambaye si mchungaji, na wala kondoo si mali yake, anapoona mbwamwitu anakuja, huwaacha kondoo na kukimbia, kisha mbwamwitu huwakamata na kuwatawanya. Yeye hajali kitu juu ya kondoo kwa sababu yeye ni mtu wa mshahara tu. Mimi ni mchungaji mwema. Nawajua walio wangu, nao walio wangu wananijua mimi, kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Mimi nayatoa maisha yangu kwa ajili yao.” Yn 10: 11-15. “Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi.” Yn 11:25.
“Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa; ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye. Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye.” 3:14-17. Kardinali Raniero Cantalamessa Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa anasema, mahubiri haya yatalenga kupembua kwa kina na mapana matatizo, changamoto na fursa za Mama Kanisa katika Ulimwengu mamboleo. Hii ni fursa pia kwa kila mwamini kujichunguza kutoka katika undani wa maisha yake, ili kuinjilishwa, tayari kuinjilisha; ili kujazwa na uwepo wa Kristo Yesu, ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, tayari kuwashirikisha wengine mang’amuzi na uzoefu, si kutokana na yale waliyosikia au kuambiwa! Mahibiri haya yanatolewa kila Ijumaa yaani: Ijumaa tarehe 23 Februari, Ijumaa tarehe 1 Machi, Ijumaa tarehe 8 Machi, Ijumaa tarehe 15 Machi na Ijumaa tarehe 22 Machi 2024. Mahubiri haya yanatolewa kwa Makardinali, Maaskofu, Wakuu wa Mashirika na wale wote wanaotamani kushiriki!