Tafuta

Wanawake wa Israel waandamana kuachiliwa kwa mateka huko Gaza. Wanawake wa Israel waandamana kuachiliwa kwa mateka huko Gaza. 

Rachel Goldberg Polin:Jiunge nami katika kuunganisha ulimwengu

Siku 100 baada ya shambulio la Hamas na kutekwa nyara kwa mateka,Rachel Goldberg Polin,mama wa Hersh,msemaji wa familia za mateka, ambaye alikutana na Papa Francisko mwezi Novemba 2023, aliandika makala hii maalumu kwa ajili ya Gazeti la Osservatore Romano.

Rachel Goldberg Polin - Tel Aviv

Dominika tarehe 14 Januari itakuwa ni siku 100 tangu mwanangu wa pekee, Hersh, alipochukuliwa kutoka kwangu. Hersh ni raia ambaye alikuwa akihudhuria tamasha la muziki. Kabla ya kutekwa nyara, mkono wake ulikatwa kwenye kiwiko cha mkono. Ana uraia wa Marekani na Israel. Hakuna maneno ambayo yanaweza kuelezea vya kutosha jinsi ambavyo siku 100 zilizopita zimekuwa kwangu na familia yangu. Tangu alipotekwa nyara, hatujui  lolote kuhusu yeye.

Lakini katika wakati huu wa giza tumezama katika huruma, neema, upendo na msaada. Kilichokuwa cha maana hasa ni msaada wa jumuiya ya Kikristo ulimwenguni kote. Tumepokea mamia ya maelfu ya ujumbe kutoka kwa Wakristo wema na wanaojali wakitutumia baraka zao kwamba Hersh atakuwa na nguvu na kurudi nyumbani kwetu. Picha za meza ya chakula cha jioni cha familia ya Noeli, na sahani tupu iliyo na jina la Hersh, na watu wakiwasha mishumaa usiku wa manane. Kuhisi uzuri na wororo kama huo kutoka kwa majirani zetu Wakristo ulimwenguni pote kulituchochea kufikia hisia ya kina chetu.


Nilipata fursa ya kipekee ya kukutana na Baba Mtakatifu nikiwa sehemu ya kikundi kidogo cha familia zingine za mateka. Alitusikiliza na kushiriki  nasi maumivu yetu. Papa Francisko alisema jambo ambalo lilinibadilisha. Yaani, tuliyoyapata ni ugaidi na ugaidi huo ni “kutokuwepo kwa ubinadamu.” Yalikuwa rahisi, yenye hekima na yenye kutia moyo. Mpaka hapo nilikuwa nimeanza kutilia shaka ubinadamu. Lakini baada ya kusikia maneno haya, tumaini langu kwa ulimwengu lilirejeshwa. Tangu Hersh alipotekwa nyara, nimevaa kipande cha mkanda juu ya moyo wangu na idadi ya siku tangu kutoweka kwake. Ninatumia alama nyeusi na kuandika namba kila asubuhi. Hivi karibuni nilianza kuuomba ulimwengu ujiunge nami katika kuweka utepe, kama mimi nifanyavyo. Ni ishara ya mshikamano katika ulimwengu wetu uliovunjika. Ninaomba watu wote, wa dini zote, makabila, mataifa na rika zote wajiunge nami.

Katika ulimwengu wetu ambao unateseka sana, katika maeneo mengi na kwa njia nyingi, hii ni njia rahisi kwetu sisi sote kukusanyika na kusema ... inatosha. Inatosha kwa mateso ya watu wa pande zote mbili za mzozo. Hakuna machozi zaidi. Inatosha kwa kumwaga damu. Yanatosha na maumivu. Yanatosha. Hatua ya kwanza kuelekea huruma ni umoja. Hatua ya kwanza kuelekea umoja ni mshikamano. Na hatua ya kwanza kuelekea mshikamano inaweza kuwa ishara. Ungana nami katika ishara ya mama anayeteseka. Kama vile Mama Maria alivyolia, mimi pia naulilia ulimwengu wetu uliogawanyika. Ninaomba na kuamini kwamba wokovu kwa Hersh na mateka wengine wapendwa utafika hivi karibuni; na kwa maelfu yote ya watu wasio na hatia wanaoteseka huko Gaza. Wakati umefika. Amina. Na  iwe hivyo.

Ushuhuda wa Rachel Goldberg Polin
13 January 2024, 16:18