Tafuta

Watu wa Mungu nchini Uturuki, tarehe 3 Desemba 2023 wamezindua Maadhimisho ya Mwaka wa Ekaristi Takatifu yatakayofikia hatima yake tarehe 24 Novemba 2024 Watu wa Mungu nchini Uturuki, tarehe 3 Desemba 2023 wamezindua Maadhimisho ya Mwaka wa Ekaristi Takatifu yatakayofikia hatima yake tarehe 24 Novemba 2024   (Erzdiözese Wien/ Schönlaub Stephan)

Maadhimisho ya Mwaka wa Ekaristi Takatifu Nchini Uturuki 2023-2024

Watu wa Mungu nchini Uturuki, tarehe 3 Desemba 2023 wamezindua Maadhimisho ya Mwaka wa Ekaristi Takatifu yatakayofikia hatima yake tarehe 24 Novemba 2024 wakati wa Maadhimisho ya Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu. Lengo ni kuhakikisha kwamba waamini wanajitahidi kumfahamu, kumpenda na kumtumikia Kristo Yesu, daima wakitambua uwepo wake angavu katika maumbo ya Mkate na Divai, kama ilivyokuwa kwa wafuasi wa Emau.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Fumbo la Ekaristi Takatifu, ni kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Mwanga linalobubujika kutoka katika Neno la Mungu linalohitaji: kutangazwa na kushuhudiwa kama kielelezo cha imani tendaji. Lina hitaji usikivu wa kiibada na ukimya wa kitafakari uwezeshao Neno la Mungu kugusa akili na nyoyo za waamini. Ekaristi Takatifu ni chakula cha maisha ya kiroho na kielelezo cha uwepo endelevu, fungamani na angavu wa Kristo Yesu kati pamoja na waja wake.  Ekaristi takatifu ni shule ya upendo, ukarimu, umoja na mshikamano wa dhati kati ya watu wa Mungu. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti na shule ya Upendo; ni zawadi na sadaka ya Kristo Yesu Msalabani; kielelezo cha huduma inayomwilishwa na kuwasha moto wamapendo kwa Mungu na jirani. Hili ni Fumbo kubwa linalopaswa kuadhimishwa vyema; Kuabudiwa na Kutafakariwa kikamilifu. Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka wake wa Kitume, “Kaa Nasi Bwana”: Mane, Nobiscum Domine”, anawaalika waamini kujenga utambuzi hai wa uwepo halisi wa Kristo Yesu, katika adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu na katika Ibada nje ya Ibada ya Misa Takatifu. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa kufunga Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu Kimataifa huko nchini Ufilippini aliwatakia wajumbe wote imani thabiti na upendo kwa Kristo Yesu anayeendelea kuwepo katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, ili kweli waweze kuwa ni Wamisionari na wafuasi amini wa Kristo Yesu; kwa kujenga na kudumisha umoja wa Kanisa sanjari na kuendeleza ari na mwamko wa kimisionari katika Makanisa mahalia. Ekaristi Takatifu iwe ni chachu ya: haki, upatanisho na amani duniani kote. Ekaristi Takatifu iwe ni shule ya huduma ya unyenyekevu, tayari kujisadaka kwa ajili ya wengine; kiini cha umisionari na ufuasi wa Kristo. Waamini wawe mstari wa mbele kuonesha mshikamano wa udugu wa upendo na wema; wapanie daima kujenga maisha yao, kielelezo cha nguvu ya Ekaristi Takatifu inayopyaisha maisha na kubadili nyoyo za waamini, tayari kuwahudumia na kuwalinda maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii.

Mwaka wa Ekaristi Takatifu Nchini Uturuki 2023-2024
Mwaka wa Ekaristi Takatifu Nchini Uturuki 2023-2024

Ni mwaliko kwa waamini kujitahidi kuwa wakamiliifu kama Baba yao wa mbinguni alivyo mkamilifu, kwa kupinga ukosefu wa haki, kwa kusimama kidete dhidi ya rushwa na ufisadi; mambo yanayovuruga umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii na matokeo yake ni kusigina, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu iwasaidie waamini kuwa ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake; mahali pa katekesi endelevu katika maisha ya kiroho, kama ilivyokuwa kwa wale wanafunzi wa Emau, waliobahatika kufafanuliwa Maandiko Matakatifu na hatimaye, wakamtambua Kristo Yesu kwa kuumega Mkate. Mama Kanisa anatukumbusha kwamba, Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Sadaka; Shukrani na masifu kwa Mungu Baba; Ni kumbukumbu ya sadaka ya Kristo na ya Mwili wake; Kanisa ni kielelezo cha uwepo wa Kristo Yesu kwa nguvu ya Neno na Roho wake Mtakatifu. Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Imani na kutokana na ukuu wake, tunaweza kuthubu kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Thoma, kusema Bwana wangu na Mungu wangu! Mama Kanisa anataka kuwa kweli ni chombo cha haki, amani, umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Ekaristi Takatifu ni kumbukumbu endelevu ya Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, changamoto na mwaliko kwa waamini kuifia dhambi na kuanza kujikita katika mchakato wa toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. Ni katika muktadha wa umuhimu wa Ekaristi Takatifu katika maisha na utume wa Kanisa, watu wa Mungu nchini Uturuki, tarehe 3 Desemba 2023 wamezindua Maadhimisho ya Mwaka wa Ekaristi Takatifu yatakayofikia hatima yake tarehe 24 Novemba 2024 wakati wa Maadhimisho ya Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu. Lengo ni kuhakikisha kwamba watu wa Mungu nchini Uturuki wanajitahidi kumfahamu, kumpenda na kumtumikia Kristo Yesu, daima wakitambua uwepo wake angavu katika maumbo ya Mkate na Divai, kama ilivyokuwa kwa wafuasi wa Emau. Rej. Lk 2413-37. Mkazo ni maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Tafakari ya kina ya Neno la Mungu linalomwilishwa katika matendo ya huruma, na kielelezo cha ushuhuda wa imani tendani anasema, Askofu mkuu Martin Kmetec, O.F.M. Conv., Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uturuki. Huu ni mwaliko pia wa kujenga na kudumisha umoja wa Kanisa mahalia na Kanisa la Kiulimwengu. Kumbe, huu ni mwaka wa neema na baraka.

Jusikiliza na kujibu kilio cha Mama Dunia na maskini
Jusikiliza na kujibu kilio cha Mama Dunia na maskini

Baba Mtakatifu Francisko ameridhia kwamba, Maadhimisho ya Kongamano la 53 la Ekaristi Takatifu Kimataifa “53rd International Eucharistic Congress” (IEC) yaadhimishwe Jimbo kuu la Quito lililoko nchini Ecuador. Maadhimisho haya yataanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 8-15 Septemba 2024. Maadhimisho haya yananogeshwa na kauli mbiu “Udugu wa kuponya Ulimwengu: “Nanyi nyote ni ndugu.” Mt 23: 8. Ujumbe wa udugu wa kibinadamu unagusa masuala mbalimbali ya kijamii, ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kukimbilia Moyo Mtakatifu wa Yesu ili apate kuwaganga na kuwaponya. Maadhimisho haya yanakwenda sanjari na maadhimisho ya miaka 150 tangu Ecuador ilipowekwa chini ya ulinzi na mambolezi ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, kisima cha huruma na upendo tarehe 25 Machi 1874. Hii ikawa ni nchi ya kwanza kabisa duniani kujiweka chini ya ulinzi na maombezi ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Itakumbukwa kwamba, Jubilei ya Mwaka 2025 inanogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini” baada ya dhoruba ya maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 pamoja na patashika nguo kuchanika kutokana na vita inayoendelea kupiganwa vipande vipande sehemu mbalimbali za dunia. Jubilei hii ni muda muafaka wa kupyaisha imani, matumaini na mapendo thabiti, kwa kuishi kama ndugu wamoja, sanjari na kusikiliza pamoja na kujibu kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini. Ni muda wa toba na wongofu wa ndani na wa kiikolojia, tayari kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Ni muda muafaka kwa waamini kujikita katika kutangaza na kushuhudia imani na matumaini yanayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani; kwa kukazia umoja na utofauti wa wateule watakatifu wa Mungu.

Mwaka wa Ekaristi Takatifu Lengo ni kupyaisha imani katika matendo
Mwaka wa Ekaristi Takatifu Lengo ni kupyaisha imani katika matendo

Jubilei ni muda uliokubalika na Mwenyezi Mungu wa kuhakikisha kwamba, waamini wanajitahidi kumwilisha karama na mapaji yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Lengo ni kutangaza na kushuhudia imani na furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Kumbe, Maadhimisho ya Mwaka wa Ekaristi Takatifu nchini Uturuki ni sehemu muhimu sana ya maandalizi ya maadhimisho ya Kongamano la 53 la Ekaristi Takatifu Kimataifa “53rd International Eucharistic Congress” (IEC) huko Jimbo kuu la Quito nchini Ecuador sanjari na Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo pamoja na kukoleza Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu kwa watu wa Mungu nchini Uturuki.  Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu ni kielelezo cha hija ya maisha ya Wakristo, wanaoitwa na kukusanywa na Kristo kwa ajili ya kujenga na kuliimarisha Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Ni mwaliko wa kushiriki na kujenga: misingi ya haki, amani na upatanisho; umoja na mshikamano mambo yanayobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Hii ni meza ya Neno la Mungu na chakula cha maisha ya uzima wa milele, changamoto ya kuhakikisha kwamba, waamini wanaishi katika neema ya utakaso na kifungo cha upendo. Waamini waendelee kujikita katika mchakato wa utamadunisho; majiundo, katekesi makini na endelevu ili kupambana na changamoto mamboleo mintarafu maisha ya kiimani, kimaadili na kiutu. Waamini wawe ni mashuhuda na vyombo vya imani tendaji, mchakato unaopania kujikita katika utakatifu wa maisha. Kwa wale waliobahatika kupata nafasi katika masuala ya kisiasa, wajitahidi kuhakikisha kwamba, wanashiriki vyema zaidi katika mchakato mzima wa kutafuta, kupanga na kutekeleza mipango hiyo. Kumbe, kila Mkristo ajitahidi kuhakikisha anashiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu ni kikolezo makini cha Injili ya familia inayokumbatia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Mwaka wa Ekaristi Takatifu
04 January 2024, 14:03