Tafuta

kwa mwaka 2023 wamisionari  waliofia imani yao kwa Kristo Yesu ni 20  ulimwenguni. kwa mwaka 2023 wamisionari waliofia imani yao kwa Kristo Yesu ni 20 ulimwenguni.  (Vatican Media)

Fides:Wamisionari 20 waliuawa mwaka 2023

Shirika la Kipapa la Habari za Kimisionari Fides,katika kuelekea mwisho wa mwaka limechapisha taarifa kuhusu wamisionari waliouawa mnamo mwaka 2023.Kulingana na mtazamo wa kibara,kwa mwaka 2023 idadi kubwa zaidi imerekodiwa barani Afrika,ambapo wamisionari 9 waliuawa:mapadre 5 na watawa 2,mseminari 1 na mnovisi 1.

Na Angella Rwezaula - Vatican

Katika Katekesi ya Papa Francisko mnamo tarehe 19 Aprili 2023 alisema: “Wafiadini hawapaswi kuonekana kama ‘mashujaa’ ambao walitenda kibinafsi, kama maua yaotayo jangwani, bali ni kama matunda yaliyoiva na yaliyo bora ya shamba la mizabibu la Bwana, ambalo ni Kanisa.” Kwa njia hiyo katika taarifa zilizokusanywa na Shirika la Kipapa la Habari za Kimisionari Fides zinafichua kwamba kwa mwaka 2023, wamisionari 20 waliuawa duniani. Hawa ni Askofu 1, mapadre 8, mabruda 2, mseminari 1, novisi 1 na walei 7 wanaume na wanawake. Ingawa orodha zilizokusanywa na Shirika la Fides huwa wazi kila mara kwa masasisho na masahihisho, wamisionari 2 zaidi waliuawa ikilinganishwa na mwaka 2022. Kulingana na mtazamo wa kibara, mwaka 2023 idadi kubwa zaidi imerekodiwa barani Afrika, ambapo wamisionari 9 waliuawa: mapadre 5, na watawa 2, mseminari 1, novisi 1. Huko Amerika, wamisionari 6 waliuawa: Askofu 1, mapadre 3, walei 2. Huko Asia, wanaume na wanawake 4 walifariki, wakiuawa na ghasia. Hatimaye, mlei mmoja aliuawa barani Ulaya.

Kwa mujibu wa Mwandishi Stefano Lodigini anabainisha kuwa kama ilivyokuwa miaka iliyopita, Shirika la Kipapa la Habari za Kimisonari Fides linatumia neno ‘mmisionari’ kwa wote waliobatizwa, kwa kutambua kwamba ‘kwa sababu ya Ubatizo uliopokelewa, kila mshiriki wa Watu wa Mungu amekuwa mfuasi wa kimisionari. Kila mtu aliyebatizwa, bila kujali kazi yake katika Kanisa na kiwango cha elimu ya imani yake, ni funzo tendaji la uinjilishaji” kama asemavyo Papa Francisko katika Waraka wa Evangelii gaudium, 120. Zaidi ya hayo, orodha ya kila mwaka ya Fides kwa muda mrefu haijawahusu wamisionari ad gentes, yaani wa Watu tu kwa maana nzito, lakini kwa kuzingatia watu wote waliobatizwa waliohusika katika maisha ya Kanisa na ambao walikufa kwa njia ya vurugu, hata kama hii haifanyiki waziwazi ya kuchukia imani’... Kwa sababu hii “tunapendelea kutotumia neno ‘mashahidi’, isipokuwa katika maana yake ya neno halisi la  ‘mashahidi’, ili tusiingie katika hukumu ambayo Kanisa inaweza kutoa juu ya baadhi yao kwa kuwapendekeza, baada ya uchunguzi wa makini,  kwa ajili ya kutangazwa kuwa mwenyeheri au kutangazwa kuwa watakatifu.

Mojawapo ya sifa bainifu ambazo wengi wa wahudumu wa kichungaji waliouawa mwaka wa 2023 wanafanana bila shaka ni maisha yao ya kawaida: yaani, hawakufanya vitendo vya kustaajabisha au shughuli za ajabu ambazo zingeweza kuvutia umakini na kuwaweka machoni pa mtu mwingine. Tukipitia maelezo machache kuhusu hali ya kifo chao kikatili tunapata mapadre waliokuwa wanakwenda kuadhimisha Misa au kufanya shughuli za kichungaji katika jumuiya fulani ya mbali; mashambulizi ya silaha yanayofanywa kwenye mitaa yenye shughuli nyingi; mashambulizi dhidi ya makanisa na nyumba za watawa ambako walijishughulisha na uinjilishaji, upendo na uhamasishaji wa watu. Walijikuta, bila kosa lao wenyewe, waathiriwa wa utekaji nyara, vitendo vya kigaidi, kuhusika katika ufyatuaji risasi au vurugu za aina mbalimbali. Katika maisha haya ya kawaida waliishi katika mazingira ya umaskini wa kiuchumi na kiutamaduni, uharibifu wa maadili na mazingira, ambapo hakuna heshima kwa maisha na haki za binadamu, lakini mara nyingi tu uonevu na unyanyasaji ni kawaida, pia waliunganishwa na kawaida nyingine ya  ile ya kuishi imani kwa kutoa ushuhuda wao rahisi wa kiinjili kama wachungaji, makatekista, wahudumu wa afya, wahuishaji wa liturujia, wa upendo...Wangeweza kwenda mahali pengine, kuhamia mahali salama zaidi, au kuacha ahadi zao za Kikristo, labda kuzipunguza, lakini hawakufanya hivyo, licha ya kujua hali hiyo na hatari zinazowakabili kila siku machoni pa ulimwengu. Lakini Kanisa, na hatimaye ulimwengu wenyewe, unasonga mbele shukrani kwao, ambao “sio maua yaliyochanua jangwani” na kwa wengi ambao, kama wao, wanashuhudia shukrani zao kwa upendo wa Kristo kwa kutafsiri katika matendo ya kila siku ya udugu na matumaini.

Wamisionari 20 waliouwawa mwaka 2023

Katika Sikukuu ya Mtakatifu Stefano, shahidi wa kwanza wa jumuiya ya Kikristo, Papa Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana alikumbuka kuwa: “Bado kuna wengi - wale wanaoteseka na kufa ili kushuhudia Yesu, kama vile walivyo kuadhibiwa katika viwango mbalimbali kwa ajili ya mwenendo unaopatana na Injili, na wale wanaohangaika kila siku kubaki waaminifu, bila mbwembwe, kwa kazi zao nzuri, huku ulimwengu ukiicheka na kuhubiri jambo lingine. Hata hawa kaka na dada wanaweza kuonekana kuwa wameshindwa, lakini leo hii tunaona kwamba sivyo. Sasa kama ilivyokuwa wakati huo, kiukweli, mbegu ya sadaka  zao, ambayo inaonekana kufa, ikichipuka na kuzaa matunda, kwa sababu Mungu anaendelea kutenda maajabu kupitia kwao (taz. Matendo 18:9-10), kubadilisha mioyo na kuokoa watu.”(Angelus, 26 decembre 2023).

Kwa mtazamo wa vifo vya wamisionari kila bara duniani: Bara la Afrika, Wamisionari 9 waliuawa. Hawa ni mapadre 5, mabruda 2, mseminari 1, na novisi 1. Hawa ni katika nchi ya Nigeria (4) Padre Isaac Achi,  kwa kuuawa na moto wakati wa shambulio kwenye parokia yake, katika Jimbo la Niger, lililofanywa na kikundi chenye silaha; Padre Charles Onomhoale Igechi, alishambuliwa na watu wenye silaha, kando ya Barabara ya Agbor, katika Jimbo la Edo; mseminari Na'aman Danlami, ambaye alichomwa moto akiwa hai katika shambulio la baadhi ya majambazi katika parokia aliyohudumu katika Jimbo la Kaduna; novisi Wabenediktini Godwin Eze, alitekwa nyara kutoka katika monasteri ya Eruku, Jimbo la Kwara, na kisha kuuawa na watekaji nyara.

Nchini Burkina Faso (2), Padre Jacques Yaro Zerbo alipoteza maisha kikatili, aliuawa na watu wasiojulikana wenye silaha, katika eneo la Boucle ya Mouhoun, wakati anakwenda kufanya shughuli za uchungaji, na Frateli Moses Simukonde Sens,aliyeuawa kwa risasi iliyofyatuliwa na maajenti waliokuwa wakisimamia kituo cha ukaguzi cha kijeshi katika mji mkuuOuagadougou, Burkina Faso, Nchini Tanzania (1) Padre Pamphili Nada alifariki dunia alipokuwa akipelekwa hospitali baada ya kushambuliwa katika parokia yake, mkoani Arusha. Huko Camerun (1) Ndugu Cyprian Ngeh alishambuliwa na kuchomwa kisu hadi kufa katika mtaa wa Bamenda. Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (1) Padre Léopold Feyen aliuawa kwa kuchomwa kisu katika eneo la Kinshasa, alipokuwa chumbani kwake parokiani ambako alitekeleza huduma yake ya kichungaji.

Barani AMERIKA wamisionari 6 waliuawa: Askofu 1, mapadri 3 na  walei 2. Hawa ni katika Nchi ya Mexico (4) Padre Juan Angulo Fonseca alipigwa risasi na kufa katika jimbo la Jalisco; Padre Javier García Villafaña aliuawa kwenye barabara inayounganisha manispaa ya Cuitzeo na Huandacareo, alipokuwa anakwenda kwa gari kuadhimisha Misa; Gertrudis Cruz de Jesús na Gliserina Cruz Merino, makatekista vijana, waliuawa wakati wa shambulio la kuvizia walipokuwa wakielekea kwenye maandamano ya Ekaristi katika jimbo la Oaxaca.

Nchini Marekani (2) Askofu David O'Connell, Askofu Msaidizi wa Los Angeles, aliuawa na mume wa mfanyakazi wa nyumbani ambaye alimtunza, na alikamatwa na kukiri mauaji hayo; Padre Stephen Gutgsell alikufa kufuatia shambulio la kisu lililotokea katika kanisa la Fort Cahloun, jumuiya ndogo ya Nebraska ambayo alikuwa ameiongoza kwa miaka 11.

Barani ASIA  ni watu 4 walei waliuawa. Hawa ni Nchini Ufilipino (2) kati ya waathirika  wa bomu lililolipuliwa wakati wa adhimisho la Ekaristi katika Chuo Kikuu cha Jimbo la Mindanao, katika jimbo la Lanao del Sur, kulikuwa na wanafunzi wawili wa Kikatoliki na watu waliojitolea kutoka jumuiya ya chaplaincy ya chuo kikuu, waliohusika katika uhuishaji wa kiliturujia: Junrey Barbante na Janine Arenas. Huko Palestina (2) Samar Kamal Anton, na mama yake, Nahida Khalil Anton, waliuawa na wavamizi walipokuwa wakitembea kuelekea kwenye nyumba ya watawa ya Mama Teresa huko Gaza. Mmoja aliuawa wakati akijaribu kumbeba mwingine kumpeleka salama. Wote wawili walikuwa wa kundi la wanawake, Wakatoliki na Waorthodox, walioshiriki katika safari ya imani na utume hasa kwa ajili ya maskini na walemavu.

Barani  ULAYA: Mlei 1 aliuawa. Ni huko Hispania ambaye Diego Valencia, mlei, aliyehusika katika Sakresitia ya parokia ya Mama wa Palma, huko Algeciras, katika jimbo la Cadiz, aliuawa na kijana wa Morocco aliyejihami kwa panga, ambaye alijeruhi hata watu wengine kando yake.

30 December 2023, 11:07