Tafuta

Mfuko wa Joseph Ratzinger, Benedikto XVI, ulianzishwa rasmi tarehe 1 Machi 2010 na Baba Mtakatifu Benedikto XVI. Mfuko wa Joseph Ratzinger, Benedikto XVI, ulianzishwa rasmi tarehe 1 Machi 2010 na Baba Mtakatifu Benedikto XVI.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Tuzo ya Mfuko wa Joseph Ratzinger Benedikto XVI Kwa Mwaka 2023

Kila mwaka, Mfuko huu unatoa tuzo kwa washindi katika nyanja mbalimbali za maisha na utume wa Kanisa na kwa mwaka 2023 Tuzo ya Mfuko wa Joseph Ratzinger, Benedikto XVI, imetolewa kwa Profesa Pablo Blanco Sarto na Francesc Torralba Rosellò na kwamba, hii ni mara ya kwanza tuzo hii kutolewa baada ya kifo cha Baba Mtakatifu Benedikto XVI kilichotokea tarehe 31 Desemba 2022 kwenye Monasteri ya “Mater Ecclesiae” na kuzikwa tarehe 5 Januari 2023.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mfuko wa Joseph Ratzinger, Benedikto XVI, ulianzishwa rasmi tarehe 1 Machi 2010 na Baba Mtakatifu Benedikto XVI. Mfuko huu unapania pamoja na mambo mengine: Kuibua na kukuza taalimungu ya Baba Mtakatifu Benedikto XVI kwa njia ya tafiti makini za kisayansi, mikutano, warsha na makongamano ya kitaifa na kimataifa, kwani unatambua kwamba, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu ni mahali muafaka pa kukuza na kuendeleza dhamana ya utamadunisho sanjari na uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo, ili kweli Injili iweze kuingia na kugusa mila, desturi na tamaduni za watu, dhamana inayoweza kutekelezwa kwa dhati kabisa kwa njia ya weledi wa kitaaluma, kisayansi na kielimu. Ni mfuko unaosaidia watafiti mbalimbali kuchapisha kazi zao pamoja na kutoa udhamini kwa wanafunzi wanaotaka kujizatiti zaidi katika taalimungu ya Baba Mtakatifu Benedikto XVI, ambaye katika maisha na utume wake wote alijipambanua kuwa ni shuhuda wa imani thabiti ya Kanisa Katoliki. Kila mwaka, Mfuko huu unatoa tuzo kwa washindi katika nyanja mbalimbali za maisha na utume wa Kanisa na kwa mwaka 2023 Tuzo ya Mfuko wa Joseph Ratzinger, Benedikto XVI, imetolewa kwa Profesa Pablo Blanco Sarto na Francesc Torralba Rosellò na kwamba, hii ni mara ya kwanza tuzo hii kutolewa baada ya kifo cha Baba Mtakatifu Benedikto XVI kilichotokea tarehe 31 Desemba 2022 kwenye Monasteri ya “Mater Ecclesiae” na kuzikwa tarehe 5 Januari 2023.

Tuzo ya Joseph Ratzinger imetolewa kwa mara ya kwanza tangu B16 afariki
Tuzo ya Joseph Ratzinger imetolewa kwa mara ya kwanza tangu B16 afariki

Haya ni maelezo yaliyotolewa na Padre Federico Lombardi, SJ., Rais wa Mfuko wa Joseph Ratzinger, Benedikto XVI kama sehemu ya utangulizi kabla ya kukabidhi Tuzo ya Mfuko wa Joseph Ratzinger, Benedikto XVI, iliyotolewa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican tarehe 30 Novemba 2023. Katika hotuba yake, Kardinali Pietro Parolin amekazia kuhusu: Amana, Utajiri na Urithi alioacha Baba Mtakatifu Benedikto XVI kama Khalifa wa Mtakatifu Petro: Shuhuda wa imani katika Fumbo la Utatu Mtakatifu; Kiongozi aliyeonesha ujasiri wa pekee katika kukuza na kudumisha majadiliano katika medani mbalimbali za maisha; Mchango wake katika maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican; Nyaraka za Kitume “Deus Caritas Est” yaani “Mungu ni upendo”, “Spe salvi” yaani “Matumaini yanayookoa”; Caritas in veritate yaani “Ukweli katika upendo” na Wosia wa kitume, ambao hakuumalizia kuuandika kama hitimisho la maadhimisho ya Mwaka wa Imani ni “Lumen fidei” yaani “Mwanga wa imani.

Mfuko wa Joseph Ratzinger: Majadiliano ya Kidini
Mfuko wa Joseph Ratzinger: Majadiliano ya Kidini

Kardinali Pietro Parolin anasema, Kanisa halina budi kusonga mbele baada ya kufariki kwa Papa Benedikto XVI aliyeacha amana na utajiri mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu Ukristo kwa kukazia zaidi: Utu, heshima na haki msingi za binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Benedikto XVI katika Waraka wake wa Kitume: Upendo katika Ukweli; “Caritas in veritate” anakazia kuhusu: Utu heshima na haki msingi za binadamu kuwa ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na wala si fedha na faida kubwa. Papa Benedikto XVI Shuhuda wa imani katika Fumbo la Utatu Mtakatifu na kwamba, Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu na kwamba, kwa hakika binadamu anatamani uwepo angavu wa Mungu katika maisha yake, ili kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Jumuiya ya binadamu inapaswa kusimikwa katika msingi wa haki na amani; mshikamano na maridhiano. Alikazia majadiliano katika ukweli na uwazi katika medani mbalimbali za maisha; majadiliano kati ya imani na uwezo wa mwanadamu kufiri na kutenda. Kwa hakika Baba Mtakatifu Benedikto XVI ni mfano bora wa kuigwa katika ujasiri mintarafu majadiliano na kwamba, ni kiongozi aliyekuwa na kipaji kikubwa cha usikivu, changamoto inayoendelezwa na Papa Francisko. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, lilikuwa ni tukio la matumaini ndani ya Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, walitambua dhamana, wajibu na changamoto iliyokuwa mbele yao, wakaamua kujadili vipengele mbalimbali na hatimaye, kuvipigia kura.

Padre Federico Lombard, Rais wa Mfuko
Padre Federico Lombard, Rais wa Mfuko

Ni Mtaguso uliowakusanya viongozi kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili kujadili maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, chini ya uongozi na usimamizi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, wakati huo akiwa ni Mtakatifu Yohane XXIII. Maaskofu na Makardinali wengi walishiriki kikamilifu katika kupembua na kujadili hali ya maisha na utume wa Kanisa. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walitaka kufanya marekebisho makubwa kwenye Liturujia kwa maana Kanisa kwa njia ya Liturujia, hasa Sadaka takatifu ya Ekaristi, latimizwa tendo la ukombozi wa mwanadamu. Liturujia inawasaidia kikamilifu waamini kushuhudia katika maisha yao na kuwadhihirishia wengine fumbo la Kristo Yesu na pia maumbile halisi ya Kanisa la kweli. Liturujia ya Kanisa ni chemchemi ya ibada ya kweli inayorutubishwa kwa njia ya sala binafsi. Waamini wanapokusanyika ili kusali kwa pamoja, Kristo Yesu yuko kati pamoja nao, hivyo anawasaidia kumwilisha kati yao ule upendo kwa Mungu na jirani. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walitaka kuleta mageuzi makubwa ndani ya Kanisa; Kuhusu Neno la Mungu, Ufunuo na Majadiliano ya Kidini na Kiekumene. Baadhi ya Mababa wa Mtaguso walitaka Kanisa lijadili kuhusu uhusiano kati ya Serikali na Kanisa. Mabadiliko ya Liturujia ya Kanisa yalipania kuhakikisha kwamba, waamini wanashiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, kwa kutumia lugha na maneno ambayo yaligusa undani wa mioyo ya watu, daima wakiwa na utambuzi makini wa Maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa. Mababa wa Kanisa walitamani kuona kwamba, maadhimisho yanayofanyika ndani ya Kanisa yanawagusa watu wote na hivyo kusaidia ushiriki mkamilifu wa mafumbo ya Kanisa.

Uchumi unaozingatia utu, heshima na haki msingi
Uchumi unaozingatia utu, heshima na haki msingi

Baba Mtakatifu Benedikto XVI katika Waraka wa kitume “Mungu ni upendo” “Deus caritas est”, uliandikwa wakati Jumuiya ya Kimataifa inapitia kipindi kigumu katika historia kutokana na mtikisiko wa uchumi kitaifa na kimataifa, vita, kinzani na mipasuko ya kidini; mambo ambayo yaliwakatisha wengi tamaa! Papa Benedikto XVI akaibuka na ujumbe wa matumaini na upendo kwa kukaza na kusema kwamba Mungu ni upendo, ndiye asili ya maisha, wema na utakatifu. Ni Mungu mwenye sura ya kibinadamu inayojifunua kwa njia ya Kristo Yesu! Baba Mtakatifu katika Waraka wa Mungu ni upendo anafafanua kwamba, Kanisa ni Jumuiya inayojikita katika upendo wa Kristo Yesu, mwaliko na changamoto ya kuhakikisha kwamba, Kanisa linatekeleza dhamana na wajibu wake kwa njia ya upendo unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Kwa namna ya pekee kabisa, upendo wa Mungu unajidhirisha katika kazi ya uumbaji inayofumbatwa katika historia ya wokovu. Waamini wanapaswa kumwilisha imani inayobubujika kutoka katika Maandiko Matakatifu katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku, hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Hii inatokana na ukweli kwamba, Kriso Yesu ni ushuhuda kamili wa pendo la Mungu katika maisha ya mwanadamu! Kwa kumpenda Mungu, waamini wajenge pia tabia ya kuwapenda na kuwathamini jirani zao!

Tuzo ya Joseph Ratzinger kwa Mwaka 2023
Tuzo ya Joseph Ratzinger kwa Mwaka 2023

Utekelezaji wa mikakati mbali mbali ya shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Mama Kanisa katika maisha na utume wake zinapaswa kuambata upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu na kwamba, upendo halisi ni wajibu na dhamana inayopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa katika shughuli zake za kichungaji kwa kuambata haki inayokamilishwa katika fadhila ya upendo. Upendo unapaswa kumwilishwa katika medani mbali mbali za maisha ya kijamii, binadamu akipewa kipaumbele cha kwanza. Huduma za upendo zinazotolewa na Mama Kanisa hazina budi kupata chimbuko na hitimisho lake kwa Kristo Yesu, Msamaria wa kwanza aliyethubutu kuganga madonda ya binadamu kwa kumwondolea dhambi na kumpatia mahitaji yake msingi. Viongozi wenye dhamana na madaraka katika Kanisa na Jamii katika ujumla wake, wanapaswa kutekeleza utume wao kwa kuambata: ukweli na uwazi; upendo, imani na matumaini. Kardinali Pietro Parolin anamkumbuka Papa Benedikto XVI kwa mahubiri yake ya kina, tasaufi na pamoja na taalimungu inayobubujika kutoka katika sala hata katika uzee wake.

Mfuko wa Joseph R.
14 December 2023, 15:25