Tafuta

Tamko la Mafundisho Tanzu ya Kanisa “Fiducia supplicans” Yaani “Kuomba Baraka kwa Imani” Maana ya Baraka Kichungaji” : Halitekelezeki! Tamko la Mafundisho Tanzu ya Kanisa “Fiducia supplicans” Yaani “Kuomba Baraka kwa Imani” Maana ya Baraka Kichungaji” : Halitekelezeki!  (Vatican Media)

Tamko la Kuomba Baraka Kwa Imani "Halitekelezeki" Kwa Baadhi ya Nchi Duniani

Kenya: Mapenzi ya watu wa jinsia moja hayakubaliki katika tamaduni za Kiafrika, kumbe huu ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, ili kuweza kuukumbatia na kuuambata wokovu. Malawi: vitendo vya ushoga na usagaji ni kinyume cha kanuni maadili na utu wema kumbe, havikubaliki. Baraka haziwezi kutolewa kwa wapenzi wa jinsia moja, kufanya hivyo ni kwenda kinyume cha Amri za Mungu, Mafundisho ya Kanisa na hisia za kitamaduni za watu wa Mungu Nigeria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tamko la Mafundisho Tanzu ya Kanisa “Fiducia supplicans” Yaani “Kuomba Baraka kwa Imani” Maana ya Baraka Kichungaji” lililotolewa na Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa tarehe 18 Desemba 2023 baada ya kuridhiwa na Baba Mtakatifu Francisko. Papa akijibu mashaka ya Makardinali “Dubia” waliomwandikia kuelezea wasiwasi wao kuhusu masuala makuu matano huku wakiomba tafsiri kuhusiana na: Ufunuo wa Kimungu, juu ya baraka kwa watu wa jinsia moja; Kuhusu Sinodi kama mwelekeo wa Kisheria wa Kanisa; Juu ya Upadrisho wa wanawake ndani ya Kanisa Katoliki na juu ya Toba kama sharti la lazima kwa ajili ya msamaha unaotolewa kwenye Sakramenti ya Upatanisho. Mashaka Kuhusu baraka za watu wa jinsia moja Baba Mtakatifu anasema, Ndoa ya Kikristo kama sura inayoakisi muungano kati ya Kristo Yesu na Kanisa lake, inatekelezwa kwa utimilifu katika muungano kati ya mwanaume na mwanamke wanaojitoa mmoja kwa mwenziye kwa upendo ulio huru, wenye uaminifu na wa kipekee, ambamo kila mmoja anakuwa ni mali ya mwenzake hadi kufa, na wanakuwa radhi kuendeleza uzao, tena wamewekwa wakfu kwa Sakramenti inayowaletea neema ya kuwa Kanisa la nyumbani na kuwa chachu ya maisha mapya kwa jamii. Hii ndio maana ya Ndoa ya Kikristo na wala si vinginevyo! Rej. Amoris laetitia 292. Pamoja na msimamo huu wa Kanisa, lakini pia upendo wa kichungaji unapaswa kuoneshwa kwa kujikita katika: uelewa, uvumilivu, huruma na ujasiri bila kuwahukumu waamini wengine kuwa ni wadhambi!

Tamko la Baraka la Kuomba Baraka Kwa Imani linakabiliwa na changamoto
Tamko la Baraka la Kuomba Baraka Kwa Imani linakabiliwa na changamoto

Tamko la Mafundisho Tanzu ya Kanisa “Fiducia supplicans” Yaani “Kuomba Baraka kwa Imani” Maana ya Baraka Kichungaji” lilijadiliwa katika mkutano wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, likapelekwa kwa Baba Mtakatifu na hatimaye, akaridhia lichapwe kwa kuweka saini yake tarehe 18 Desemba 2023. Tamko hili linajadili kwa kina na mapana kuhusu: Baraka katika Sakramenti ya Ndoa, Maana ya baraka katika Maandiko Matakatifu, Uelewa wa baraka kitaalimungu na kichungaji, na nani anaweza kuomba baraka. Baraka kwa watu wenye “ndoa tenge” pamoja na wapenzi wa jinsia moja. Kanisa ni Sakramenti ya upendo wa Mungu. Watu wa Mungu wenye imani thabiti wanaweza kupokea baraka za Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu na Kanisa na kwamba, Kristo Yesu ni kielelezo cha baraka kuu kutoka kwa Mungu, baraka ambayo ni chemchemi ya wokovu. Baraka katika Sakramenti ya Ndoa Takatifu: Kiini cha ndoa ya Kikristo ni maagano baina ya mume na mke au ukubaliano wao wa hiari usiotanguka. Muungano huo wa mume na mke na manufaa ya watoto wao huwataka wawe na uaminifu kamili kati yao. Kwa asili yake ndoa na mapendo ya wenye ndoa yamewekwa kwa ajili ya kuzaa watoto na kuwalea; nao ni taji yao. Kwa kweli watoto ni zawadi kuu ya Ndoa na tunu kubwa ya wazazi wenyewe. Haya ndiyo Mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu Ndoa na kamwe hayawezi kubadilishwa. Wakati wa kutoa baraka, Kanisa lina wajibu na dhamana ya kuhakikisha kwamba halichanganyi madhehebu ya kutoa baraka, ili kusitokee mkanganyiko na kwamba, Kanisa halina mamlaka ya kutoa baraka kwa wapenzi wa jinsia moja.

Mapenzi ya jinsia moja hayakubaliki katika tamaduni za Kiafrika
Mapenzi ya jinsia moja hayakubaliki katika tamaduni za Kiafrika

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, KCCB katika mjadala mintarafu Tamko la Mafundisho Tanzu ya Kanisa “Fiducia supplicans” Yaani “Kuomba Baraka kwa Imani” Maana ya Baraka Kichungaji” linasema kwamba, Tamko linatoa mchango mpya wa maana ya baraka kichungaji, kielelezo kwamba, Mwenyezi Mungu anawaangalia waja wake na hata mahitaji yao. Tamko linatoa angalisho la kutochanganya kuhusu baraka inayotolewa kwenye Liturujia ya Sakramenti ya Ndoa na baraka nyingine zinazotolewa na Mama Kanisa. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linakiri kwamba, mapenzi ya watu wa jinsia moja hayakubaliki katika tamaduni za Kiafrika, kumbe huu ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, ili kuweza kuukumbatia na kuuambata wokovu. Kazi ya Mama Kanisa ni kukusanya wale waliotawanyika, kuwatafuta waliopotea; kuwaongoza wadhambi kwenye njia ya wokouvu kwa kuondokana na nafasi sanjari na mazingira ya dhambi. Baraka zinapaswa kutambulikana kadiri ya mapenzi ya Mungu. Uinjilishaji ni safari ambayo kila mtu anaifanya kwa msaada wa neema na maombezi ya Kanisa.

Maaskofu wa Zambia na Malawi wanasema, Tamko halitekelezeki
Maaskofu wa Zambia na Malawi wanasema, Tamko halitekelezeki

Kwa upande wake, Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi, linaendelea kukazia kwamba, Tamko hili lina mwelekeo wa shughuli za kichungaji wala Baba Mtakatifu Francisko hajaruhusu  watu wa jinsia moja kuoana ingawa wanaweza kuomba baraka nje la maadhimisho ya Liturujia ya Sakramenti ya Ndoa wanasema Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi kwa kuzingatia maana ya baraka na sababu za kichungaji, linasema, hakuna baraka yoyote inayoweza kutolewa kwa wapenzi wa jinsia moja nchini Malawi. Nalo Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia, ZCCB linakazia kuhusu “Maana ya Baraka Kichungaji” na kwamba, vitendo vya ushoga na usagaji ni kinyume cha kanuni maadili na utu wema kumbe, havikubaliki. Kwa kuzingatia sheria za Zambia na urithi wa kitamaduni, Tamko la Mafundisho Tanzu ya Kanisa “Fiducia supplicans” Yaani “Kuomba Baraka kwa Imani” Maana ya Baraka Kichungaji” halitekelezeki nchini Zambia.

Maaskofu wa Nigeria wanasema hakuna mabadiliko katika Mafundisho ya Ndoa
Maaskofu wa Nigeria wanasema hakuna mabadiliko katika Mafundisho ya Ndoa

Nalo Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria, CBCN, linasema, Tamko linaonesha uwezekano wa kutoa baraka kwa wapenzi wa jinsia moja, linakazia maana ya Sakramenti ya Ndoa kadiri ya Mafundisho tanzu ya Kanisa Katoliki pamoja na huruma ya Mungu inayowahimiza wapenzi wa jinsia moja kutojikatia tamaa, bali wawe na matumaini kwa neema na baraka za Mungu zinazoweza kuwasaidia kutubu na kumwongokea Mungu. Maaskofu wanakaza kusema, Mafundisho ya Kanisa kuhusu Sakramenti ya Ndoa Takatifu yako pale pale na wala hakuna mabadiliko. Kumbe, nchini Nigeria, baraka haziwezi kutolewa kwa wapenzi wa jinsia moja, kufanya hivyo ni kwenda kinyume cha Amri za Mungu, Mafundisho ya Kanisa na hisia za kitamaduni za watu wa Mungu nchini Nigeria. Mapadre waendelee kuwasindikiza wanandoa kwa kuwahimiza kuchuchumlia na kuambata utakatifu wa ndoa.

Tamko linakabiliwa na changamoto za kitamaduni, kihisia na kimaadili
Tamko linakabiliwa na changamoto za kitamaduni, kihisia na kimaadili

Kwa upande wake, Askofu mkuu Socrates Buenaventura Villegas wa Jimbo kuu la Lingayen-Dagupan, nchini Ufilippin anakazia kuhusu huruma ya Mungu na mchakato wa utakatifushaji kadiri ya mapenzi ya Mungu, Nia na Mafundisho ya Kanisa. Kanisa Katoliki linaitwa na kutumwa kutangaza nguvu ya neema ya Mungu kwa njia ya sala, Ekaristi Takatifu na Sakramenti ya Upatanisho. Kristo Yesu ndiye mwenye nguvu za kuganga na kuponya moyo uliovunjika na kupondeka, ili kuonja upendo usiokuwa na masharti pamoja na urafiki wake.   Wakati huo huo Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi, OFM Cap., wa Jimbo kuu la Dar Es Salaam, Tanzania anasema kwa bahati mbaya mazingira ambamo Mafundisho ya Baraka ya Mahusiano ya Jinsia Moja yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko yametekwa na watu kwenye jamii na mitandao ambao hawalitakii mema Kanisa Katoliki. Anawataka watu wa Mungu wawe watulivu na kamwe “wasipaniki” wabaki katika uelewa na msingi wa Mafundisho sahihi ya Kanisa kuhusu Saramanti ya Ndoa.

Tamko Kuhusu Baraka
21 December 2023, 15:02