Tafuta

Ukanda wa Gaza wenye wakazi millioni mbili umeathirika vibaya na kwamba, watu hawana uhakika wa usalama wa maisha yao. Ukanda wa Gaza wenye wakazi millioni mbili umeathirika vibaya na kwamba, watu hawana uhakika wa usalama wa maisha yao.  

Sherehe ya Noeli Nchi Takatifu: Uchungu, Huzuni Na Masikitiko!

Watu wengi wamepoteza maisha na wengi zaidi wanateseka kutokana na vita, idadi ya wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum imeongezeka maradufu; kuna kilio kikuu cha maskini pamoja na uharibifu wa mazingira nyumba ya wote; zote hizi ni changamoto zinazoifanya Sherehe ya Noeli, 2023 iwe ni ya uchungu, huzuni na masikitiko makubwa! Kanisa ni chemchemi ya imani, matumaini na mapendo ya Mungu kwa watu wake; ujenzi wa amani ni muhimu sana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Pierbattista Pizzaballa, Patriaki wa Yerusalemu, tarehe 24 Desemba, ameongoza mkesha wa Noeli kwa mwaka 2023 mjini Yerusalemu. Katika mahubiri yake, amekazia kuhusu mazingira alimozaliwa Mtoto Yesu, Madhara ya Vita, leo hii Mtoto Yesu anazaliwa mahali gani? Dhamana na nafasi ya wachungaji wa kondeni sanjari na umuhimu wa kutangaza na kushuhudia Injili ya amani sehemu mbalimbali za dunia. Kardinali Pierbattista Pizzaballa anasema, Mtoto Yesu alizaliwa kwenye hori ya kulishia ng’ombe kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni. Anasema vita kati ya Israeli na Palestina imesababisha madhara makubwa kwa watu na mali zao.

Ukanda wa Gaza umeathirika sana kutokana na vita
Ukanda wa Gaza umeathirika sana kutokana na vita

Ukanda wa Gaza wenye wakazi milioni mbili umeathirika vibaya na kwamba, watu hawana uhakika wa usalama wa maisha yao. Wapalestina wamegeuka kuwa wageni katika nchi yao wenyewe na matokeo yake ni kwamba: chuki, uaminifu na tabia ya kutaka kulipizana kisasi imeongezeka maradufu. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu kutoa nafasi ili kweli Mtoto Yesu aweze kuzaliwa tena katika akili na nyoyo za waamini, sanjari na roho za viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa. Watu wengi wamepoteza maisha na wengi zaidi wanateseka kutokana na vita, idadi ya wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum imeongezeka maradufu; kuna kilio kikuu cha maskini pamoja na uharibifu wa mazingira nyumba ya wote; zote hizi ni changamoto zinazoifanya Sherehe ya Noeli kwa Mwaka 2023 iwe ni ya uchungu, huzuni na masikitiko makubwa.

Kanisa ni chemchemi ya imani, matumaini na mapendo ya Mungu kwa waja wake
Kanisa ni chemchemi ya imani, matumaini na mapendo ya Mungu kwa waja wake

Lakini, Kanisa la Mungu bado linaendelea kuwa ni chemchemi ya imani, matumaini na mapendo ya Mungu kwa watu wake. Kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, Mtakatifu Yosefu na wale wachungaji wa kondeni, waamini wanahamasishwa kutengeneza mazingira ambamo ataweza kuzaliwa Mtoto Yesu, kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Rej. Yn 3:16-17. Hii ni changamoto ya kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu na kwamba, wote ni watoto wa Mungu, licha ya tofauti zao msingi. Mtoto Yesu alipata makazi katika maisha ya Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu.

Waamini wajenga utamaduni wa haki, amani, msamaha na upatanisho
Waamini wajenga utamaduni wa haki, amani, msamaha na upatanisho

Hata katika kipindi hiki cha machafuko ya kisiasa na vita, kuna haja kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kukuza na kudumisha udugu wa kibinadamu, kwa kuombea na kuishi katika amani; kwa kuonesha ukarimu, kwa kujadiliana katika ukweli na uwazi; kwa kusameheana na kujenga upatanisho wa Kitaifa, tayari kukuza utamaduni wa haki, amani na maridhiano kati ya watu, kwani amani ni tunda la haki! Wachungaji wa kondeni, walibahatika kuwa ni mashuhuda wa Fumbo la Umwilisho, wakabahatika kuwa watu wa kwanza kumwona Mtoto mchanga, amevikwa nguo za kitoto, amelala katika hori ya kulishia ng’ombe, kielelezo cha unyonge na udhaifu wa binadamu, lakini huu ni mwaliko wa kupenda na kuhudumia; kwa kuendelea kutoa nafasi ya mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi; upatanisho na msamaha wa kweli, kama nguzo msingi za ujenzi wa amani ya kudumu. Hii ni changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujikita katika hija ya ujenzi wa amani duniani; kwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu pasi na makunyanzi. Waamini waendelee kusimama kidete kutafuta na kudumisha Injili ya amani, ukweli na haki kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Yerusalemu
26 December 2023, 15:08