Tafuta

2022.12.21 Yesu mtoto katika mikono ya mama yake Maria. 2022.12.21 Yesu mtoto katika mikono ya mama yake Maria. 

Noeli 2023,Kard.Farrell:Tukuze imani kwa Mungu na mapendo kwa kila mtu

Umwilisho ni wa bure kabisa ya wokovu.Kama Maria lazima kutambua kwamba tunahitaji msaada wa kuzaliwa upya kwa neema.Yesu ni Mungu aliyeumbwa mwanadamu ambaye anatufundisha maadili ya kweli ya maisha,huruma,msamaha na upendo.Tumtambue Mwokozi wetu katika Yesu.Ni tafakari Noeli ya Kardinali Farrell,Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei,Familia na Maisha.

Na Angella Rwezaula, - Vatican.

Tafakari ya Noeli Takatifu iliyotolewa na Kardinali Kevin Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha katika fursa ya Noeli ya 2023, alibainisha kuwa "siku chache zilizopita Baba Mtakatifu alitoa mwaliko kwetu: “tuthamini ukimya, kiasi na kusikiliza. Maria, Bikira wa ukimya, atusaidie kupenda jangwa, kuwa sauti za kuaminika zinazomtangaza Mwana wake ajaye”(Malaika wa Bwana 10 Desemba 2023). Ningependa, kwa maneno haya rahisi, kuukubali mwaliko wa Papa na kuchukua muda wa kutulia na kunyamaza nanyi ili kutafakari Noeli, tujitayarishe kuiishi ipasavyo, kurejesha maana na kina kwa imani yetu na kuwa sisi pia ni:  “sauti za kuaminika zikimtangaza Mwana wake”. Kwa kutazama mahali pote siku hizi tunaweza kuona kwamba karibu hakuna mahali ambapo tunaweza kupata ukimya, kiasi,na kusikiliza.

Hakika, kila mwaka kile kilichotokea wakati wa kuzaliwa Yesu  kihistoria kinaonekana kurudiwa: Mwokozi, Masiha aliyetangazwa na manabii, alizaliwa Bethlehemu, lakini watu hawakujua, hawakumtambua na walimtambua lakini si kumkaribisha. Kardinali Farrell anasisitiza kuwa "hata  leo hii inafanyika hivyo: Noeli inaadhimishwa, lakini karibu hakuna anayetambua uwepo wa Yesu kati yetu. Maana ya kidini ya sherehe hii inaonekana kuwa imepotea. Fumbo la Umwilisho linaonekana kutokuwa na umuhimu wowote, linawaacha watu wengi kutojali. Kwa sisi wakristo haiwezi kuwa hivyo! Hatuwezi kuruhusu kutojali kwa ujumla, kuvuruga, mtawanyiko na fadhaa ya ulimwengu, iliyomezwa na sherehe tupu na za juu juu, kuingia ndani ya roho zetu. Kwetu sisi, Noeli yaani kuzaliwa kwa Mwokozi  ni mwanzo wa ukombozi wetu! Ni tukio ambalo limebadilisha maisha yetu na ya dunia nzima milele!"

Umwilisho ni wa bure kabisa wa wokovu

Tangu tangazo la kwanza la kuzaliwa kwa Yesu, na kutokea kwa malaika Gabrieli kwa Bikira Maria, tunakabiliwa na kipengele kikuu cha fumbo la Umwilisho: uhuru kamili wa wokovu. Katika liturujia ya Majilio matamshi hayo yanalingana na ziara ya nabii Isaya kwa Mfalme Ahazi, aliyealikwa kuomba  ishara ya matumaini katika hali ngumu aliyokuwa akiipitia (rej Isa 7:10-17). Lakini katika pindi hicho, kwa visingizio vya kinafiki vya kidini, mfalme alikataa kuomba ishara. Hata hivyo, licha ya nia mbaya ya kibinadamu, Mungu alitoa ahadi: “Tazama, bikira atachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume, naye atamwita Imanueli” (Isa 7:14). Mwanadamu huendelea kufuata mipango yake midogo ya wokovu, hata hivyo, Mungu, mwingi wa huruma, huja kumsaidia kwa kumpatia wokovu wa kweli, ambao unapita zaidi ya matarajio yoyote ya kibinadamu. Tangazo la ajabu la Isaya la “mwana-Emanueli” lilitimizwa kwa kuzaliwa kwa Yesu: Bikira Maria alimzaa Yesu, Mwana wa Aliye Juu Sana, Yule ambaye kweli ni Emanueli, uwepo wa Mungu ulio hai pamoja nasi. Hata katika kipindi cha Kupashwa habari, kipengele cha  hiki kinaonekana mbele katika usemi "Umejaa neema": katika lugha ya asili, kihalisi, inamaanisha "yeye ambaye amejazwa neema". Ni Mungu aliyetenda, aliyejaza roho ya Maria neema, na ambaye kupitia kwake alitupatia Mwokozi, kwa njia isiyotarajiwa kabisa na isiyofikirika.

Sherehe ya Noeli  hutukumbusha sisi sote kwamba sikuzote Mungu anatutolea Mwana wake kuwa Mwokozi, na anafanya hivyo bila malipo kabisa, hata ikiwa sisi, kama Mfalme Ahazi, hatujali kuja kwake. Ni lazima tukubali, kiukweli, kwamba katika kila enzi watu hawatambui hitaji lao la wokovu. Katika siku zetu, kwa mfano, tunaona vurugu ikiongezeka kila mahali, hata katika familia na katika uhusiano wa karibu wa kihemko, tunashuhudia kuongezeka kwa vita, tunatambua kuchanganyikiwa na kuvunjika moyo kwa watu wengi, tunaona matokeo chungu ya maovu na kila maadili, ugonjwa unaopelekea maisha ya watu wengi kuharibika. Hata hivyo, pamoja na haya yote, tunaona pia kwamba watu hawatamani Mwokozi, hawana matumaini ya mtu ambaye anaweza kufanya upya maisha yao. Inaonekana kwamba hawataki kuponya, kwamba hawataki kuponywa, kukombolewa. Ingetosha kufungua mtazamo wetu ili kuona mwanadamu ni nani na kwa uhalisi unaotuzunguka kuinua kilio cha kuomba msaada kwa Mungu, ombi la wokovu kwa Yule aliyetuumba. Lakini ni wachache hufanya hivyo!

Kama Maria: kwa kutambua kwamba tunahitaji msaada, kuzaliwa upya, neema

Tukikabiliwa na ugumu huu wa moyo, ambao unaweza pia kutuambukiza, lakini kwa mfano wa Bikira Maria unatusaidia. Alipopokea tangazo la Malaika, Maria hakuonesha kiburi, hakujibu kama Mfalme Ahazi ambaye hahitaji chochote. Hata hivyo, alisikiliza kwa unyenyekevu, alielewa kwamba wakati huo Mungu anajifanya kuwa karibu na watu wote, kwamba ameangalia kwa huruma umaskini wao na kwa hiyo alikaribisha mpango wa Mungu bila madai ya kibinafsi zaidi ya kuwa mtumishi wa mipango ya ajabu ya Mungu: “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana, na nitendewe kam ulivyosema  ” (Lk 1:38). Kardinali Farrell aliendelea kusema kuwa sisi  pia leo hii, tukimtazama Maria na kujiandaa kwa Noeli, tunaalikwa kutambua kwamba tunahitaji Mwokozi. Tunahitaji msaada, wa kuzaliwa upya, neema ambayo haitoki kwetu, bali  inatoka kwa aliye juu".

Yesu ni Mungu aliyeumbwa mwanadamu ambaye anatufundisha maadili ya kweli ya maisha, ya  ni nini maana huruma, msamaha, upendo

Je, hii hutokeaje? Sakramenti za Kanisa zinatujulisha neema inayotoka juu, hutufanya kuwa washiriki katika asili ya kimungu, hutupatia Roho Mtakatifu. Na wakati sisi, kama Maria, tunakaribisha zawadi hizi za wokovu kila kitu kinabadilishwa. Uwepo wa mwanadamu daima unatishiwa na maumivu, kutokuwa na uhakika wa siku zijazo na kupoteza motisha wa kuishi. Lakini tunapomkaribisha Kristo Mwokozi inakuwa safari ya furaha kuelekea umilele,uliyojaa maana na yenye wingi wa mema, hata katikati ya majaribu. Uhusiano kati ya mwanamume na mwanamke daima unatishiwa na kutoelewana na unyanyasaji. Lakini unapomkaribisha Mwokozi, inakuwa mahali pa kukaribishwa na kusaidiana, kwa upendo usio na masharti na kutajirishana. Ushirika kati ya watu na watu daima unatishiwa na maslahi ya ubinafsi, kusongwa wengine na ukosefu wa haki, lakini wakati Kristo Mwokozi anapokaribishwa hutulia, unakuwa wa kibinadamu zaidi, zaidi ya amani, zaidi ya kidugu. Umwilisho hakika ni mwanzo wa maisha mapya! Mungu Baba, kwa kumtuma Mwana wake, anatupatia uwezekano wa kutobaki wafungwa wa taabu zetu. Yesu ni Mungu, mtu ambaye anatufundisha maadili ya kweli ya nini maana ya maisha, huruma, msamaha, upendo na kutupatia nguvu ya kuyaweka yote katika vitendo.

Tumtambue Mwokozi wetu katika Yesu na tumkaribishe bila upinzani katika maisha yetu

Tukiwa tumekusanyika katika Pango la  Kuzaliwa kwa Yesu, katika ukaribu wa familia zetu, katika mkusanyiko wa makanisa yetu, tumwombe Bikira Maria kwa unyenyekevu na hekima ya kumtambua Yesu kama Mwokozi wetu na kumkaribisha bila upinzani katika maisha yetu. Noeli hii itufanye kukua katika imani kwa Mungu na katika mapendo kwa kila mtu, hasa kwa wale ambao wameguswa zaidi na maumivu na mahitaji. Noeli Njema kwa wote!

23 December 2023, 17:51