Tafuta

Katika “Mafundisho ya kudumu ya Kikatoliki juu ya ndoa, Tamko linahimiza kuwa hayabadiliki: Ndoa ni ya mwanaume na mwanamke." Katika “Mafundisho ya kudumu ya Kikatoliki juu ya ndoa, Tamko linahimiza kuwa hayabadiliki: Ndoa ni ya mwanaume na mwanamke."  Tahariri

Moyo wa Mchungaji ambaye hafungi kamwe mlango

Katika tahariri ya Mwariri wetu Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano Vatican,Dk.Tornielli kuhusu Tamko la Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa la “Fiducia supplicans:”“Kuomba Baraka kwa Imani” kuhusu maana ya Baraka ya Kichungaji,lililoridhiwa na Papa na kuchapishwa Desemba 18 anasema:“Tamko linalofungua uwezekano wa baraka rahisi kwa watu wa jinsia moja ni kama tabia ya Yesu na Majisterio ya Francisko.”

ANDREA TORNIELLI

“Nemo venit nisi tractus,” hakuna mtu anayemkaribia Yesu ikiwa hajavutiwa, aliandika Mtakatifu Augustino, akifafanua maneno ya Mnazareti: “Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka.” Katika chimbuko la mvuto kuelekea kwa Yesu - kivutio hicho ambacho Benedikto wa kumi na sita alizungumzia wakati akikumbuka jinsi imani inavyoenea - daima kuna tendo la neema. Mungu daima hututangulia, hutuita, hutuvuta, hutufanya tupige hatua kuelekea kwake au angalau kuwasha ndani yetu hamu ya kuchukua hatua hiyo hata kama bado tunajiona kwamba hatuna nguvu na kujisikia kupooza. Moyo wa mchungaji hauwezi kubaki bila kujali watu wanaomkaribia kwa unyenyekevu wakiomba kubarikiwa, bila kujali hali zao, historia yao, njia yao ya maisha. Moyo wa mchungaji hauzimi nuru inayofukwa ya wale wanaohisi kutokamilika kwao wenyewe wakijua kwamba wanahitaji huruma na msaada kutoka Juu. Moyo wa mchungaji unaona katika ombi hilo la baraka ufa ukutani, mwanga mdogo ambao kupitia huo, neema inaweza kufanya kazi. Na kwa hiyo jambo lake la kuangaikia ni kutoziba ufa mdogo, kukaribisha na kuomba baraka na huruma ili watu walio mbele yake waanze kuelewa mpango wa Mungu kwa maisha yao.

Ufahamu huu wa kimsingi unaonekana katika “Fiducia supplicans yaani “Kuomba Baraka kwa Imani, ambalo ni Tamko la Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa juu ya maana ya Baraka ya Kichungaji, ambayo inafungua uwezekano wa kubariki wanandoa wasio wa kawaida, hata wa jinsia moja, likifafanua wazi baraka hiyo katika unyeti wa muktadha huo kwamba: "haimaanishi kuidhinisha uchaguzi wao wa maisha" na pia kusisitiza haja ya "kuepuka ibada yoyote au vipengele vingine ambavyo vinaweza hata kuiga harusi kwa mbali."  Ni hati inayojikita ndani ya fundisho la baraka, ikitofautisha kati ya zile za kiutamaduni na za kiliturujia na zile za hiari ambazo zinajulikana badala ya kuwa matendo ya ibada yanayohusishwa na ucha Mungu wa Watu. Ni maandishi yanayofanya uthabiti, miaka kumi baadaye, ya maneno yaliyoandikwa na Papa Francisko katika Waraka wa Kitume wa “Evangelii gaudium: “Kanisa si nyumba ya mpakani, ni nyumba ya kibaba ambapo kuna nafasi kwa kila mtu na maisha yake magumu.” 

Chimbuko la Tamko hilo ni la kiinjili. Karibu katika kila ukurasa wa Injili, Yesu anavunja mila na tamaduni na maagizo ya kidini, heshima na kanuni za kijamii. Na yeye anatimiza ishara ambazo zinakashifu fikra sahihi, kwa wanaojiita “safi”, wale wanaotumia kanuni na sheria kama ngao kusukuma mbali, kukataa, na kufunga milango. Karibu katika kila ukurasa wa Injili tunaona walimu wa sheria wakijaribu kumwaibisha na kumweka kwenye matatizo Mwalimu kwa maswali ya upendeleo na kisha kunung'unika kwa hasira mbele ya uhuru wake uliojaa huruma: “Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi na kula nao!” Yesu alikuwa tayari kukimbilia nyumba ya akida wa Kapernaumu ili kumponya mtumishi wake mpendwa, bila wasiwasi wa kujitia unajisi kwa kuingia katika nyumba ya mpagani. Alimruhusu mwenye dhambi kuosha miguu yake mbele ya sura za kuhukumu na za dharau za wageni, bila kuelewa kwa nini hakumfukuzia mbali.

Alitazama na kumwita Zakayo mtoza ushuru akiwa amekaa kwenye matawi ya mkuyu, bila kutarajia kwamba kabla ya kupata mtazamo huo wa huruma  angeongoka na kubadili maisha yake. Hakumshutumu mwanamke mzinzi ambaye, kulingana na sheria, angepigwa mawe, lakini alinyang'anya mikono ya wauaji wake kwa kuwakumbusha kwamba wao pia - kama kila mtu - walikuwa wenye dhambi. Alisema alikuja kwa ajili ya wagonjwa na si kwa wenye afya, alijifananisha na sura ya pekee ya mchungaji aliye tayari kuwaacha kondoo 99 bila uangalizi wa kwenda kumtafuta aliyepotea. Alimgusa mwenye ukoma, akimponya kutokana na ugonjwa huo na unyanyapaa wa kuwa “mtu asiyeweza kuguswa.” Hawa "waliokataliwa" walikutana na mtazamo wake na kuhisi kupendwa, wapokeaji wa kukumbatiwa kwa huruma bila masharti yoyote. Walipojikuta wanapendwa na kusamehewa, walitambua walivyokuwa: wenye dhambi maskini kama kila mtu mwingine, wanaohitaji uongofu, ombaomba wa kila kitu.

Baba Mtakatifu Francisko aliwaambia makardinali wapya mnamo  mwezi Februari 2015 kuwa: “Kwa Yesu, jambo la muhimu zaidi ni kufikia na kuokoa wale walio mbali, kuponya majeraha ya wagonjwa, kuwaunganisha tena kila mtu katika familia ya Mungu! Na Yesu haogopi kashfa ya aina hii!” Yeye hawafikirii watu wenye mawazo yaliyofungwa ambao hata wamekashifiwa na uponyaji, ambao wamekasirishwa na uwazi wowote, kwa hatua yoyote ambayo haiendani na mifumo yao ya kiakili na ya kiroho, kwa kubembeleza au huruma ambayo hailingani na tabia zao, wa mawazo na usafi wao wa kiibada.”

“Mafundisho ya kudumu ya Kikatoliki juu ya ndoa, Tamko linahimiza kuwa hayabadiliki: ni katika muktadha wa ndoa kati ya mwanamume na mwanamke ndipo “mahusiano ya ngono yanapata maana yao ya asili, ya kutosha na kamili ya kibinadamu.” Kwa hiyo ni lazima tuepuke kutambua kuwa ndoa ni “kitu ambacho siyo.” Bali kwa mtazamo wa kichungaji na kimisionari, sasa mlango haujafungwa kwa wanandoa “wasio wa kawaida” wanaokuja kuomba baraka rahisi, labda wakati wa kutembelea madhabahu au wakati wa hija.”  Msomi wa Kiyahudi Claude Montefiore alibainisha upekee wa Ukristo kwa usahihi katika hili kwamba: «Ijapokuwa dini zingine zinaelezea mwanadamu katika kumtafuta Mungu, Ukristo unatangaza Mungu anayemtafuta mwanadamu ... Yesu alifundisha kwamba Mungu hangojei toba ya mtenda-dhambi, anakwenda kumtafuta ili umwite kwake.” Mlango uliofunguliwa wa sala na baraka ndogo unaweza kuwa mwanzo, fursa na msaada.

Anahitimisha Tahariri yake Mwariri wetu Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano Vatican, Dk.  Andrea Tornielli kuhusu Tamko la Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa la “Fiducia supplicans:” “Kuomba Baraka kwa Imani” kuhusu maana ya Baraka ya Kichungaji.

Taariri ya Dk. Andrea Tornielli kuhusu Fiducia -Supplicans:Kuomba Baraka kwa Imana
19 December 2023, 14:54