Mahubiri ya Kardinali Cantalamessa Kipindi cha Majilio 2023: Njia ya Bwana!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kipindi cha Majilio ni muda muafaka wa kupyaisha: imani, matumaini, mapendo na amani. Ni kipindi kinachotoa dira, mwongozo, malezi na majiundo ya maisha ya kiroho kama sehemu ya maandalizi ya ujio wa Kristo Yesu katika maisha ya waamini katika maadhimisho ya Sherehe ya Noeli. Kardinali Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa nyumba ya Kipapa anasema, mahubiri yake katika Kipindi cha Majilio kwa Mwaka 2023 yanaongozwa na kauli mbiu: “Tayarisheni Njia ya Bwana: Kuelekea Maadhimisho ya Noeli Pamoja na Mtangulizi na Mama wa Kristo Yesu.” Kardinali Raniero Cantalamessa, katika mahubiri yake ya kwanza ya Kipindi cha Majilio, Ijumaa tarehe 15 Desemba 2023 amemtafakari Yohane Mbatizaji, Sauti ya mtu aliaye nyikani; kama mtu mwadilifu na Nabii aliyehubiri toba na wongofu wa ndani; Yohane Mbatizaji alikuwa ni zaidi ya Nabii aliyejikita katika mchakato wa uinjilishaji na kwamba, kila mwamini anaweza kuwa ni mwinjilishaji. Liturujia ya Kipindi cha Majilio inaanza kwa kumweka mbele ya macho ya imani Nabii Isaya anayetangaza ujio wa Masiha, Yohane Mbatizaji kama Mtangulizi wa Masiha na hatimaye, mkazo unawekwa kwa Bikira Maria.
Kiini cha mahubiri ya Yohane Mbatizaji kinachota utajiri na amana kutoka katika Injili ya Luka kuhusu tishio la hukumu sanjari na matunda yapatanayo na toba: “Yohana akawaambia wale waliokuja ili awabatize, “Enyi watoto wa nyoka! Ni nani aliyewaonya muepuke hukumu ya Mungu itakayokuja? Kama kweli mmetubu, basi onyesheni kwa matendo yenu. Wala msidhani kuwa mtasamehewa kwa kuwa ninyi ni uzao wa Ibrahimu. Nawaambia wazi, Mungu anaweza kabisa kumpa Ibrahimu watoto kutoka katika haya mawe! Na hivi sasa hukumu ya Mungu, kama shoka kwenye shina la mti, iko juu yenu. Kila mti usiozaa matunda mazuri utakatwa katwa na kutupwa motoni.” Watu wakamwuliza, “Inatupasa tufanyeje basi?” Akawaambia: “Aliye na nguo mbili amgawie asiye na nguo; kama una chakula wape wenye njaa.” Watoza kodi nao pia walikuja ili wabatizwe; wakamwuliza, “Bwana, na sisi inatupasa tufanyeje?” Akawajibu: “Msimdhulumu mtu kwa kudai kodi zaidi ya ile iliyoamriwa.” Na baadhi ya askari wakamwuliza, “Na sisi je, tufanye nini?” Akawajibu: “Msichukue fedha za watu kwa kutumia nguvu; msiwashtaki watu kwa kuwasingizia makosa; bali mtosheke na mishahara yenu!” Lk 3:7-14.
Yohane Mbatizaji alitangaza na kushuhudia uwepo wa Ufalme wa Mungu na watu wengi wakajibidiisha kutaka kuingia humo kwa kuzingatia Sheria na Manabii pamoja na Amri za Mungu, ili kujenga mahusiano mema na Mungu. Toba na wongofu wa ndani kilikuwa ni kiini cha ujumbe wa Kristo Yesu kama ilivyo pia kwa Yohane Mbatizaji, jambo ambalo liliwachukua muda ili kutubu na hatimaye, kumwongokea Mungu, kwa kuzingatia Amri kuu ya Upendo kwa Mungu na jirani, lakini watambue kwamba, Mungu Mwenyezi ndiye aliyeanza kuwapenda kwanza. Yohane Mbatizaji aliwashambulia sana wadhambi waliotubu na kumwongokea Mungu, lakini Kristo Yesu anatuhumiwa: “Mwana wa Adamu alikuja, akila na kunywa, wakasema, Mlafi huyu, na mlevi, rafiki yao watoza ushuru na wenye dhambi! Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa kazi zake.” Mt 11:19. Kristo Yesu alikula pamoja na Mafarisayo na Watoza Ushuru kama inavyosimuliwa katika Injili alipokwenda na kushinda nyumbani mwa Zakayo na Mathayo Mtoza Ushuru, bila kumsahau yule Mwanamke mdhambi aliyempaka Kristo manukato. Kwa hakika huruma ya Mungu haina mipaka, lakini ina matokeo yake ambayo ni toba na wongofu wa ndani. Hii ni changamoto kwa wazazi katika ulimwengu mamboleo, licha ya ushuhuda na malezi makini, lakini watoto wao wanakengeuka na kuwa ni “watu wa ajabu” kwa kuzama katika matumizi haramu ya dawa za kulevya, ulevi na ukahaba, changamoto kwa waamini ni kufanya maamuzi magumu, kwa kufuata sheria au kwa kujikita katika neema na huruma ya Mungu, lakini kwa pamoja waamini wanaalikwa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu.
Yohane Mbatizaji alikuwa ni zaidi ya Nabii aliyejikita katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha, kwa kufungua kipindi kipya cha unabii wa Kikristo, kwa kumtambulisha Kristo katika hali yake ya unyenyekevu kuwa ndiye Mwanakondoo wa Mungu. Rej Yn 1:15; 19, 29-51. Hiki ni kielelezo cha imani kubwa aliyokuwa nayo Yohane Mbatizaji. Licha ya miujiza, mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu, bado Waisraeli waliona ugumu kumwamini. Hii ndiyo kashfa ya Fumbo la Umwilisho inayofumbatwa katika ufukara wa Kristo Yesu, changamoto na mwaliko kwa waamini kuwasaidia watu kumwona Kristo Yesu katika ufukara wa Kanisa na ule wa watoto wa Kanisa na kwamba, Kristo Yesu ni mwanga wa Mataifa. Yohane Mbatizaji hakuwa mahiri sana katika taalimungu kiasi cha kumfahamu Kristo Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu, Neno wa Mungu au Mwana wa Mtu, lakini maneno na maisha yake yaliwavuta wengi kumtambua Kristo Yesu katika maisha yake. Kwa kufuata mfano wa maisha na maneno ya Yohane Mbatizaji, kwa hakika kila mwamini anaweza kuwa ni mwinjilishaji lakini kwa kutumia msingi uleule wa Injili.
Neno la Mungu linakuwa na kukomaa, ikiwa kama waamini watalitafakari na kulimwilisha katika vipaumbele kwa maisha na utume wao. Mtakatifu Gregori mkuu anasema “Scriptura cum legentibus” yaani Neno la Mungu linakuwa na kukomaa kadiri linavyo somwa na hivyo linakuwa ni chemchemi ya maisha matakatifu. Mambo makuu matatu yanategemeana na kukamilishana: Ufunuo, Maandiko Matakatifu pamoja na Mapokeo hai ya Kanisa. Kristo Yesu ni yule anayebatiza kwa Maji na Roho Mtakatifu. Kumbe wokovu wa Kikristo si tu kwa ajili ya maondoleo ya dhambi, bali unamwezesha mwamini kupata maisha mapya katika Roho Mtakatifu. Huu anasema Mtakatifu Paulo ni uhuru katika Roho. “Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu. Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti.” Rum 8:1-2. Huu ni mwaliko kwa waamini kulisoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika maisha yao ya kila siku. Watakatifu huko mbinguni bado wanaendeleza utume walioutekeleza wakiwa hapa duniani. Mama Kanisa mwaka 2023 anaadhimisha Jubilei ya Miaka 150 tangu alipozaliwa Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu. Yohane Mbatizaji alibahatika kuwa Mtangulizi wa Kristo Yesu, changamoto na mwaliko kwa waamini katika ulimwengu mamboleo kuwapatia sauti katika maisha yao, chemchemi ya furaha ya ushuhuda wa Yohane Mbatizaji, Mtu mwadilifu na Nabii aliyebahatika kumwona Roho Mtakatifu, akimshukia Kristo Yesu kwa mfano wa njiwa wakati wa Ubatizo.