Tafuta

Jumatano tarehe 4 Oktoba 2023 jioni wajumbe walikusanyika na kuanza kusikiliza hotuba za ufunguzi na ujumbe kutoka kwa wawakilishi mbalimbali. Jumatano tarehe 4 Oktoba 2023 jioni wajumbe walikusanyika na kuanza kusikiliza hotuba za ufunguzi na ujumbe kutoka kwa wawakilishi mbalimbali.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Maadhimisho ya Sinodi XVI ya Maaskofu: Hotuba za Wajumbe Mbalimbali

Mara baada ya Baba Mtakatifu Francisko kufungua rasmi Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu kwa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, jioni wajumbe walikusanyika na kuanza kusikiliza hotuba za ufunguzi na ujumbe kutoka kwa wawakilishi mbalimbali. Kardinali Jean Claude Holleric, Sr. Maria Ignazia Angellin, Patriaki Ibrahim I Sedrak: Mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi mwelekeo mpya katika utume!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yananogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume” na yanahudhuriwa na wajumbe 464. Hati ya Kutendea Kazi “Instrumentum laboris” kwa Maadhimisho ya Awamu ya Kwanza ya Sinodi kuanzia tarehe 4 hadi 29 Oktoba 2023 inagusia kuhusu: Kanisa la Kisinodi Uzoefu Muhimu: Sifa za Kanisa la Kisinodi; Mwelekeo wa Maadhimisho ya Kanisa la Kisinodi: Majadiliano na Roho Mtakatifu. Sehemu ya Pili ni: Umoja, Ushiriki na Utume: Vipaumbele vitatu vya Kanisa la Kisinodi. Huu ni umoja unaong’ara, alama na chombo cha ushirika na Mwenyezi Mungu na alama ya umoja kati ya binadamu. Uwajibikaji katika utume na jinsi ya kushirikishana karama katika huduma ya Injili. Ushiriki, utawala na madaraja: Je, ni mchakato, miundombinu na taasisi gani zinapaswa kushiriki katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi? Hati ya Kutendea Kazi: “Instrumentum laboris” ni matunda ya ushiriki mkamilifu wa watu wa Mungu kutoka katika: Majimbo, Mabaraza ya Maaskofu na katika maadhimisho ngazi ya Kimabara, sanjari na maadhimisho yaliyokuwa yakiendeshwa kwa njia ya mitandao ya kijamii na hivyo kubainisha vipaumbele vya Makanisa mahalia vinavyopaswa kufanyiwa kazi kuanzia tarehe 4 – 29 Oktoba 2023. Lengo kuu ni kutekeleza utume wa Mama Kanisa wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Huu ni muda wa kusikiliza kwa makini jinsi ambavyo limeishi na kutekeleza dhamana na utume wake; matatizo na changamoto zinazojitokeza.

Kwa ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume
Kwa ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume

Changamoto kubwa katika maadhimisho ya Sinodi ni uwezo wa kuratibu kinzani ili ziweze kuwa ni chemchemi ya nguvu mpya ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Huu ni wakati ambapo utambulisho na wito wa Kanisa unajikita katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi pamoja na kuhakikisha kwamba, matunda yaliyojitokeza yanamwilishwa katika uhalisia wa maisha ya Jumuiya za waamini sehemu mbalimbali za dunia. Mara baada ya Baba Mtakatifu Francisko kufungua rasmi Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu kwa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, jioni wajumbe walikusanyika na kuanza kusikiliza hotuba za ufunguzi na ujumbe kutoka kwa wawakilishi mbalimbali. Kardinali Jean-Claude Holleric, Mwezeshaji mkuu wakati wa Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu amezungumzia juu ya mwenendo mzima wa maadhimisho ya Sinodi ambao umegawanyika katika sehemu kuu mbili, kazi ya mkutano mkuu utakaofanyika kwenye Ukumbi wa Sinodi pamoja na kazi za makundi maarufu kama “Circuli Minores” ili kuwawezesha Mababa wa Sinodi kujadiliana pamoja na kumsikiliza Roho Mtakatifu tayari kukutana na Kristo Mfufuka kama ilivyokuwa kwa wafuasi wa Emau.

Sr. Maria Ignazia Angelini OSB
Sr. Maria Ignazia Angelini OSB

Kwa upande wake Sr Maria Ignazia Angelini, OSB katika salam zake amekazia umuhimu wa Injili ambao ni kiini cha maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa, tayari kuanza maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Francisko wa Assis, tayari kulijenga Kanisa la Kristo. Ujumbe mzito kutoka kwa Mtakatifu Francisko wa Assis ni unyenyekevu, upendo mkamilifu na huduma kwa jirani pamoja na maisha ya sala. Ni mwaliko kwa Mababa wa Sinodi kusikiliza kwa makini Neno la Mungu, tayari kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili.

Patriaki Ibrahim I Sedrak wa Kanisa Katoliki la Kikoptik la Alexandria
Patriaki Ibrahim I Sedrak wa Kanisa Katoliki la Kikoptik la Alexandria

Wakati huo huo, Patriaki Ibrahim I Sedrak wa Kanisa Katoliki la Kikoptik la Alexandria, amemshukuru Mwenyezi Mungu anayewawezesha watu wake kutembea kwa pamoja na kuendelea kupata mang’amuzi juu ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, jambo ambalo si rahisi sana. Maadhimisho ya Sinodi hii yamebeba uzito wa pekee kwani yamewashirikisha watu wote wa Mungu, ili kuweza kutembea kwa pamoja, kusikilizana na hatimaye, kufanya mang’amuzi ya pamoja kila mtu kadiri yak arama na mapaji aliyokirimiwa na Roho Mtakatifu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa zima. Maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi hii yamekuwa ni changamoto kubwa na mwanzo wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi hata kabla ya kuadhimisha Sinodi yenyewe. Jambo la muhimu ni toba na wongofu wa ndani tayari kuandamana na Kristo Yesu anayewaokoa waamini kutokana kwenye vifungo vyao vya utumwa, woga na wasiwasi pamoja na upweke hasi na hivyo kuwakirimia neema ya kuweza kuishi katika utimilifu na mapendo kamili. Huu ni mwaliko kwa Mababa wa Sinodi kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu; Kristo Yesu ndiye kiini cha maadhimisho ya Sinodi, Yeye ni mwanzo na mwisho; Alfa na Omega. Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa ni njia itakayowawezesha Mababa wa Sinodi kuweza kufikia malengo ya Sinodi ya Maaskofu.

Hotuba za ufunguzi
04 October 2023, 15:45