Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu: Ujumbe kwa Watu wa Mungu Unaandaliwa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican
Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yananogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Lengo kuu la Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ni kuliwezesha Kanisa kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza na kuwashirikisha waamini walei katika maisha na utume wake. Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu yanapania pamoja na mambo mengine: kujenga na kudumisha urika wa Maaskofu, tayari kumsikiliza Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha. Hati ya Kutendea Kazi: Instrumentum laboris ni matunda ya ushiriki mkamilifu wa watu wa Mungu. Mababa wa Sinodi wametekeleza dhamana hii kwa mikutano pamoja na majadiliano yaliyofanyika kwenye makundi madogo madogo kadiri ya lugha, yanayojulikana kama “Circoli minori” ili kujenga utamaduni wa kusikiliza na kusikilizana ili kwa pamoja waweze kumsikiliza Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 29 Oktoba 2023, Majira ya Saa 4:00 za Asubuhi kwa Saa za Ulaya, anatarajia kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ili kufunga rasmi Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu katika awamu ya kwanza, ngazi ya Kanisa la Kiulimwengu. Kwa sasa Mababa wa Sinodi wanaendelea kuandika Ujumbe kwa Watu wa Mungu mara baada ya Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu katika ngazi ya Kiulimwengu. Mababa wa Sinodi wanaonja mateso mahangaiko ya watu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia wanaoteseka kutokana na baa la njaa, umaskini, vita pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Wameendelea kujadiliana kuhusu mang’amuzi kati ya uongozi wa Kanisa na uwajibikaji unaofumbatwa katika majadiliano katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu kutoa nafasi kwa Roho Mtakatifu ili kugeuza nyoyo za waamini kutoka katika hali ya mapambano ya uchu wa madaraka hadi kufikia ujenzi wa haki na amani; umoja na ushirika; kwa kujenga utamaduni wa kuwasikiliza wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya maisha na utume wa Kanisa. Hawa ni wakimbizi na wahamiaji wanaoendelea kutoa changamoto ya majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamadunini; watu wenye ulemavu, bila kuwasahau hata wale waamini wenye mielekeo ya mapenzi ya jinsia moja. Katekisimu ya Kanisa Katoliki, muhtasari wa: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili na Sala kuhusu makosa dhidi ya usafi wa moyo inasema: “Shauku ya jinsia ya aina moja inamaanisha uhusiano kati ya wanaume au kati ya wanawake wanaoonja mvuto wa kijinsia kuelekea kwa watu wa jinsia ileile tu au wanaooonja mvuto zaidi kwa watu wa jinsia ileile. Shauku hii imechukua sura mbalimbali katika mwenendo wa karne na katika tamaduni mbalimbali. Mwanzo wake kisaikolojia unabaki kwa vikubwa hauelezeki. Yakijitegemeza katika Maandiko Matakatifu yanayaonesha matendo ya kujamiana ya jinsia moja kama matendo yenye uovu mkubwa, mapokeo yametamka daima kwamba “matendo ya kujamiana ya jinsia moja ni maovu kwa yenyewe.” Ni matendo dhidi ya sheria ya maumbile. Yanatenga paji la uhai na tendo la kijinsia. Kwa namna yoyote ile hayawezi kuidhinishwa. Idadi ya wanaume na wanawake waliozama katika maelekeo ya shauku ya jinsia ya aina ileile sio ya kupuuzia.
Hawayachagui maelekeo haya na kwa walio wengi ni swala la kujaribu. Uhusiano nao wapaswa kuwa wa heshima, huruma, na uangalifu. Kila ishara ya ubaguzi usio wa haki iepukwe. Watu hawa wanaitwa kutimiza mapenzi ya Mungu katika maisha yao, na kama Wakristo, kuunganisha magumu wanayoweza kukutana nayo kutokana na hali yao na sadaka ya Msalaba wa Bwana. Watu wa shauku ya jinsia moja wanaitwa kuwa na usafi wa moyo. Kwa fadhila za kujitawala zinazowafundisha uhuru wa ndani na mara nyingine kwa kushikizwa na urafiki usiojitafuta, kwa sala na neema ya Sakramenti, wanaweza, na wanatakiwa polepole na kwa uthabiti kukaribia ukamilifu wa Kikristo.” KKK 2357-2359. Mama Kanisa anapaswa kuendelea kuonesha upendeleo wa pekee kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu Francisko anasema, nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndani ya Kanisa ni kashfa ambayo imechafua maisha na utume wa Kanisa kiasi kwamba, haiwezi kamwe kufichwa, kuikataa wala kuibeza kwani ni ukweli usioweza kufumbiwa macho. Ukweli huu unapaswa kupokelewa na hatimaye, kumwilishwa katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, wema na utakatifu wa maisha; kwa kuganga na kutibu madonda ya kashfa ya nyanyaso za kijinsia, tayari kuambata upendo na huruma ya Mungu, ili kuanza upya kwa kuchuchumilia: kanuni maadili, utu wema na utakatifu wa maisha. Lengo kuu ni kuzuia kashfa ya nyanyaso za kijinsia isijitokeze tena ndani ya Kanisa. Siku za mwisho, waamini watahukumiwa kwa jinsi walivyowatendea jirani zao walio wadogo!
Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu pamoja na mambo mengine inapania kukuza na kujenga umoja na ushirika wa watu wa Mungu unaofumbatwa katika tofauti zao msingi. Hii ni Sinodi ya Maaskofu inayowahusisha watu wa Mungu katika tofauti zao msingi yaani: Maaskofu, Mapadre, Matawa na Waamini walei. Tofauti hizi zinajionesha pia mahali wanapotoka waamini, rangi, lugha na tamaduni zao, lakini wote hawa wanaunganishwa pamoja chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu. Ikumbukwe kwamba, Fumbo la Utatu Mtakatifu ni kiini cha umoja, ushirika na ushirikishwaji wa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa. Lengo la Kanisa ni kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu sanjari na huduma kwa binadamu. Kumbe, maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ni mchakato wa toba na wongofu wa ndani, tayari kujikita katika utakatifu wa maisha unaopata chimbuko lake katika Maandiko Matakatifu, Mapokeo hai ya Kanisa sanjari na Mafundisho Jamii ya Kanisa. Hili ni Kanisa linalopaswa kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, Kristo Yesu akiwa ni kiini cha imani ya Kanisa. Wajumbe, katika “Tamko la Belèm la Mwaka 2023” kutoka Ukanda wa Amazonia wanataka watu wa Mungu Ukanda huo, kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira. Kusitisha uvunaji na unyonyaji wa mali asili kwa sababu nchi zinazoendelea zimeshindwa kugharimia miradi ya maendeleo kiuchumi iliyokuwa inagharimu kiasi cha dola bilioni 100. Wajumbe wanasema, umaskini ni kikwazo kikubwa cha ustawi na maendeleo ya wengi. Uchimbaji wa madini na uvunaji wa rasilimali za Ukanda wa Amazonia unafanywa kwa kasi ya kutisha. Uwajibikaji wa pamoja ni sehemu ya mang’amuzi ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yanayopania pia kutoa nafasi ya ushiriki mkamilifu wa wanawake katika maisha na utume wa Kanisa. Mababa wa Sinodi wanasema watawa wamekuwa mstari wa mbele kuombea maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu.
Baraza la Makanisa Ukanda wa Amazonia, “Conferência Eclesial da Amazônia” yaani: CEAMA” ni matunda ya mchakato wa maadhimisho ya Sinodi Ukanda wa Amazonia, changamoto kwa Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, anatangaza na kushuhudia Ujumbe wa Matumaini kwa watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia, kwa kuinua utu, heshima na haki zao msingi; tayari kujikita katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili sanjari na ushiriki mkamilifu wa waamini walei. Baraza la Makanisa Ukanda wa Amazonia, CEAMA linao wajibu wa kuragibisha umuhimu wa Ukanda wa Amazonia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wote wa Mungu katika ujumla wao. Sera na mikakati ya shughuli za kichungaji haina budi kutoa kipaumbele cha kwanza katika mapambano dhidi ya umaskini kwa kujikita katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kanisa Ukanda wa Amazonia halina budi kuendelea kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa kujikita katika malezi na majiundo ya Mapadre wake na kwamba, CEAMA inapaswa kuwa ni chombo cha maendeleo ya watu wa Mungu, daima kwa kusoma alama za nyakati. Uhaba wa miito ya Kipadre na Kitawa ni changamoto endelevu katika maisha na utume wa Kanisa. Mashemasi wa kudumu wanao mchango mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa, huu ni wito na wajibu wa waamini walei. Kumbe, bado Kanisa linapaswa kuendelea kusoma alama za nyakati, kujikita katika mchakato wa utamadunisho, ili kuhakikisha kwamba, waamini wanajitahidi kuishi kikamilifu tunu msingi za maisha ya Kiinjili.