Tafuta

Kardinali Protase Rugambwa ni kielelezo cha umoja, ushirikiano na utengemano wenye tija na mashiko kwa Taifa la Tanzania anasema, Askofu Benson Bagonza wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Tanzania, Dayosisi ya Karagwe, iliyoko mkoani Kagera Kardinali Protase Rugambwa ni kielelezo cha umoja, ushirikiano na utengemano wenye tija na mashiko kwa Taifa la Tanzania anasema, Askofu Benson Bagonza wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Tanzania, Dayosisi ya Karagwe, iliyoko mkoani Kagera 

Kardinali Protase Rugambwa: Ushuhuda wa Askofu Bagonza! Maajabu ya Njia za Mungu

Askofu Dr. Benson Bagonza wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Karagwe iliyoko mkoani Kagera amefurahi sana kushirikiana na Maaskofu Katoliki katika maadhimisho ya kusimikwa kwa Kardinali Protase Rugambwa, kielelezo cha umoja, ushirikiano na utengamano wenye tija na mashiko kwa Taifa la Tanzania. Kuteuliwa na hatimaye kusimikwa kwake kuwa ni Kardinali ni kati ya mambo ambayo yamegusa undani wa moyo wake kama jirani na ndugu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 9 Julai 2023 aliwateuwa Makardinali wapya 21 na kusimikwa rasmi katika mkutano wa kawaida wa Makardinali tarehe 30 Septemba 2023 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amekazia zaidi uwakilishi wa Makardinali toka sehemu mbalimbali za dunia, kama ilivyokuwa siku ile ya Pentekoste ya kwanza, hawa ni Makardinali na Maaskofu wa nyakati hizi, ili kugundua kwa mshangao zawadi ya Injili waliyoipokea katika lugha zao wenyewe, tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu; tayari pia kusimama kidete na kuwa ni wainjilishaji, huku wakimwilisha ndani mwao, ujenzi wa Kanisa la Kisinodi pamoja na kuendelea kumwaminia Roho Mtakatifu anayetengeneza utofauti na umoja; kiongozi mpole na thabiti. Kardinali Protase Rugambwa katika hotuba yake kwenye hafla ya kumpongeza, aliwashukuru wote waliobahatika kujumuika kumpongeza pamoja na kumtakia heri na fanaka katika maisha na utume wake, tangu siku ile Baba Mtakatifu Francisko alipotia nia ya kuwatangaza Makardinali wapya ishirini na moja. Kwa hakika, wamekuwa ni msaada mkubwa kwake: kiroho, kimwili na ki-hali. Kardinali Protase Rugambwa, anamshukuru Mwenyezi Mungu pamoja na Baba Mtakatifu kwa yote anayomtendea katika maisha yake. Anawashukuru wale wote waliofika mjini Vatican kuhudhuria tukio hili kubwa katika historia ya maisha na utume wake na hivyo kuongeza nguvu katika Kanisa kwa kuwa ni wasaidizi na washauri wa karibu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Makardinali wapya 21 waliosimikwa tarehe 30 Septemba 2023
Makardinali wapya 21 waliosimikwa tarehe 30 Septemba 2023

Kardinali Protase Rugambwa, anawaomba watu wa Mungu kuendelea kumkumbuka na kumwombea, ili sala zao ziendelee kumsindikiza katika maisha na utume wake kama Askofu mkuu mwandamizi wa Jimbo kuu la Tabora na kama Kardinali. Ameishukuru na kuipongeza Jumuiya ya Watanzania wanaoishi nchini Italia na kuwataka watanzania kujenga na kudumisha: umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa, mambo msingi yanayowatambulisha watanzania, licha ya tofauti zao msingi. Wawe tayari kujenga na kudumisha utamaduni wa upendo na mshikamano na watu wengine hata ambao si watanzania kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Huu ni mwaliko wa kuendelea kujifunza kujenga umoja, ushiriki na utume wa Kanisa, ili watu wote waweze kufurahia maisha na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani.

Kardinali Protase Rugambwa ameandika historia mpya kwa Kanisa la Tanzania
Kardinali Protase Rugambwa ameandika historia mpya kwa Kanisa la Tanzania

Ibada kwa ajili ya kuwasimika Makardinali wapya ilihudhuriwa na viongozi wakuu wa Makanisa mbalimbali akiwemo Askofu Dr. Benson Bagonza wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Karagwe iliyoko mkoani Kagera. Amefurahi kuunganika na watanzania wengine kushiriki katika tukio hili kama jirani mwema wa Kardinali Protase Rugambwa, anayeshirikiana naye pia katika ujamaa wa kidugu na kikristo. Anamkaribisha katika urika wa Maaskofu na kumtakia heri na baraka tele katika maisha na utume wake kama Kardinali na Askofu mkuu Mwandamizi wa Jimbo kuu la Tabora. Hii ni fahari kubwa ya Tanzania kupata Kardinali wa tatu ndani ya Kanisa Katoliki. Anamwombea baraka na mapendo ili aweze kudumu katika wito alioitiwa. Kuteuliwa kwake na hatimaye kusimikwa kuwa ni Kardinali ni kati ya mambo yaliyomgusa kutoka katika undani wa moyo wake kuona ni jinsi gani Mwenyezi Mungu anaweza kuchagua watu wake kwa kazi maalum kwa njia isiyoweza kuelezeka. Amefurahi sana kushirikiana na Maaskofu Katoliki katika maadhimisho haya, kielelezo cha umoja, ushirikiano na utengemano wenye tija na mashiko kwa Taifa la Tanzania. Kwa upande wake Askofu Msaidizi Methodius Kilaini anasema, Kardinali Protase Rugambwa ni tunu ya Tanzania na Afrika katika ujumla wake, changamoto kwa watanzania ni kuendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili, kwani Kanisa linalitambua na kulithamini Kanisa la Tanzania.

Kardinali Protase Rugambwa: Shuhuda
05 October 2023, 15:48