Tafuta

Kardinali Protse Rugambwa ni matunda ya kazi ya umisionari na uinjilishaji ndani ya Kanisa. Kardinali Protse Rugambwa ni matunda ya kazi ya umisionari na uinjilishaji ndani ya Kanisa.  

Kardinali Protase Rugambwa Ni Tunda la Mchakato wa Uinjilishaji

Mapokezi makubwa yaliyooneshwa na watu wa Mungu ni dalili za upendo mkuu anaomrudishia Mwenyezi Mungu na kwa watu wote wa Mungu, ili kukoleza imani, majadiliano ya kidini na kiekumene na kwamba, kimsingi Kardinali Protase Rugambwa ni matunda ya Jimbo kuu la Tabora. Katika mahubiri yake, Kardinali Protase Rugambwa alikazia kuhusu: Uaminifu na utii kwa Mungu; Uvumilivu wa Mungu kwetu sisi wanadamu na kwamba, Uvumilivu wa Mungu una kikomo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwadhama Kardinali Protase Rugambwa ni kati ya Makardinali 21 walioteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 9 Julai 2023 na kusimikwa rasmi tarehe 30 Septemba 2023 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Tarehe 4 Oktoba 2023 Baba Mtakatifu Francisko akashirikiana na Makardinali wapya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya ufunguzi wa Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu inayonogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume” na yanahudhuriwa na wajumbe 464 kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Tarehe 6 Oktoba, Kardinali Protase Rugambwa, alilakiwa na watu wa Mungu nchini Tanzania, wakiongozwa na Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, pamoja na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar Es Salaam. Kardinali Protase Rugambwa, aliwapatia watu wa Mungu baraka zake za Kikardinali, waamini waliohudhuria hafla ya kumpokea pale Makao makuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki, TEC, Kurasini, Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Drt. Philip Isdor Mpango aliwaongoza watanzania katika mapokezi ya Kardinali
Drt. Philip Isdor Mpango aliwaongoza watanzania katika mapokezi ya Kardinali

Na tarehe 7 Oktoba 2023, familia ya Mungu, Jimbo kuu la Tabora ilimpokea Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu Mwandamizi wa Jimbo kuu la Tabora na Dominika tarehe 8 Oktoba 2023 akaadhimisha Ibada ya shukrani kwa kuteuliwa na hatimaye kusimikwa kuwa Kardinali na hivyo kuandika historia mpya kwa Jimbo kuu la Tabora kwa kuwa ni Kardinali wa tatu kwa Kanisa la Tanzania, mwenye makao yake Jimbo kuu la Tabora. Kardinali Protase Rugambwa amewashukuru watu wote wa Mungu kutoka ndani na nje ya Jimbo kuu la Tabora kwa sala na matashi mema yaliyomsindikiza tangu siku ile Baba Mtakatifu Francisko alipotangaza nia ya kuwasimika Makardinali wapya 21 na hatimaye, wale wote waliomsindikiza katika tukio hili kubwa katika historia ya maisha na wito wake, pamoja na watu wote wanaoendelea kumwombea katika majukumu haya mapya. Mapokezi makubwa yaliyooneshwa na watu wa Mungu ni dalili za upendo mkuu anaomrudishia Mwenyezi Mungu na kwa watu wote wa Mungu, ili kukoleza imani, majadiliano ya kidini na kiekumene na kwamba, kimsingi Kardinali Protase Rugambwa ni matunda ya Jimbo kuu la Tabora. Katika mahubiri yake, Kardinali Protase Rugambwa alikazia kuhusu: Uaminifu na utii kwa Mungu; Uvumilivu wa Mungu kwetu sisi wanadamu na kwamba, Uvumilivu wa Mungu una kikomo chake. Askofu mkuu Paulo Runangaza Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora ambaye “Maaskofu wenzake wanamvulia kofia” kwa ubobezi wa historia ya Kanisa, amewakumbusha watu wa Mungu waliohudhuria Ibada ya Misa Takatifu kwamba, mahali palipoadhimishwa Ibada ya Misa Takatifu paliitwa “Unyanyembe” Tabora, mahali ambapo tarehe 25 Septemba 1960, Askofu Mkuu Marko Mihayo wa Jimbo kuu la Tabora alipopewa Daraja Takatifu ya Uaskofu na kusimikwa rasmi kuwa Askofu mkuu wa kwanza nchini Tanzania na Afrika Mashariki katika ujumla wake.

Kardinali Protase Rugambwa ni matunda ya mchakato wa uinjilishaji wa kina.
Kardinali Protase Rugambwa ni matunda ya mchakato wa uinjilishaji wa kina.

Hili ni tukio la kihistoria lililohudhuriwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, wakati ule akiwa Waziri mkuu wa Tanganyika. Hili ni tukio ambalo pia lilimkutanisha na Kardinali Laurian Rugambwa, Kardinali wa kwanza Tanzania na Afrika katika ujumla wake. Kumbe, Kardinali Protase Rugambwa ni matunda ya malezi na makuzi, tangu Shule ya Msingi, Seminari ya Ndogo ya Itaga na hatimaye, Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 2 Septemba 1990 wakati wa hija ya kitume ya Mtakatifu Yohane Paulo II nchini Tanzania. Baada ya miaka 63 Uwanja wa Unyanyembe Tabora, unashuhudia tena tukio kubwa la kihistoria la Kardinali Protase Rugambwa, kuadhimisha Ibada ya Misa ya Shukrani kwa zawadi ya Ukardinali. Watu wa Mungu Jimbo kuu la Tabora wanamshukuru Mungu kwa uweza na nguvu ndani ya maisha ya watu wake; maisha yanayopambwa kwa matukio mbalimbali. Kardinali Protase Rugambwa, Dominika tarehe 8 Oktoba 2023 ameandika historia mpya kwa Jimbo kuu la Tabora, kwa kuwa na kiti cha Ukardinali, changamoto na mwaliko kwa watu wa Mungu ndani na nje ya Jimbo kuu la Tabora kujenga na kudumisha umoja na ushirika wa watu wa Mungu.

Mapokezi ya "kufa mtu" ni dalili za upendo na mshikamano wa watu wa Mungu.
Mapokezi ya "kufa mtu" ni dalili za upendo na mshikamano wa watu wa Mungu.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Damian Denis Dallu wa Jimbo kuu la Songea ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Uinjilishaji, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania amesema, Kardinali Protase Rugambwa ni matunda ya Baraza la Kipapa la Uinjilishaji ambalo tarehe 14 Novemba 2022 limeadhimisha Jubilei ya Miaka 400 tangu kuanzishwa kwake na Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara sanjari na Miaka 100 ya Daraja Takatifu ya Upadre nchini Tanzania. Kumbe, Kardinali Protse Rugambwa ni matunda ya kazi ya umisionari na uinjilishaji ndani ya Kanisa. Itakumbukwa kwamba, Nembo ya Kardinali Protase Rugambwa inanogeshwa na maneno “Euntes in mundum universum", yaani “Enendeni Ulimwenguni kote" Mk 16:15. Naye Askofu Isaac Laizer wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Magharibi Kati na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania ametumia fursa hii, kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuipamba Dominika ya tarehe 8 Oktoba 2023, kwa Ibada ya shukrani kwa kupokelewa kwa Kardinali Protase Rugambwa, Jimbo kuu la Tabora. Amempatia pongezi nyingi Kardinali Protase Rugambwa kwa kuteuliwa na hatimaye kusimikwa kuwa ni Kardinali na Askofu mkuu mwandamizi wa Jimbo kuu la Tabora, na Mshauri wa Baba Mtakatifu. Amempongeza pia Askofu mkuu Paulo Runangaza Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora kwa wema, maisha na utume wake na kwa baraka ya kumpata Kardinali Protase Rugambwa. Anamwombea utumishi mwema na afya njema pamoja na kuendeleza majadiliano ya kiekumene ili Kristo Yesu aweze kuinuliwa!

Kardinali Rugambwa
10 October 2023, 14:07