Tafuta

Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu mwandamizi wa Jimbo kuu la Tabora, Tanzania anaandika historia mpya ya Jimbo kuu la Tabora. Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu mwandamizi wa Jimbo kuu la Tabora, Tanzania anaandika historia mpya ya Jimbo kuu la Tabora. 

Kardinali Protase Rugambwa Anaandika Historia ya Jimbo kuu la Tabora, Tanzania

Askofu mkuu Paul Runangaza Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora, Tanzania anaelezea furaha ya watu wa Mungu kwa kuteuliwa na hatimaye kusimikwa kwa Kardinali Protase Rugambwa, historia ya majimbo makuu ya Dar es Salaam na Jimbo kuu la Tabora na kwamba sasa Kardinali Protase Rugambwa anaandika historia mpya kwa maisha na utume wa Kanisa la Tanzania, kwa Jimbo kuu la Tabora kuwa ni Makao makuu ya Kardinali wa tatu nchini Tanzania. Tabora Kumenoga!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 9 Julai 2023 aliwateuwa Makardinali wapya 21 kati yao Makardinali watatu ni wale ambao wamejipambanua katika huduma kwa Kanisa na watu wa Mungu katika ujumla wao. Makardinali wapya wamesimikwa rasmi katika mkutano wa kawaida wa Makardinali tarehe 30 Septemba 2023 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Na tarehe 4 Oktoba Makardinali wapya wakashiriki katika Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya ufunguzi rasmi wa Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu inayonogeshwa na kauli mbiu: “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Makardinali kimsingi ndio walinzi wa imani na washauri wakuu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro ili kukoleza juhudi za toba, haki, amani na maridhiano; kwa kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu, ili watu waweze kuishi katika mazingira bora zaidi. Ukardinali umegawanyika katika ngazi kuu tatu: Kardinali Askofu, Kardinali Padre na Kardinali Shemasi. Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu mkuu Paul Runangaza Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora, Tanzania anaelezea furaha ya watu wa Mungu kwa kuteuliwa na hatimaye kusimikwa kwa Kardinali Protase Rugambwa, historia ya majimbo makuu ya Dar es Salaam na Jimbo kuu la Tabora na kwamba sasa Kardinali Protase Rugambwa anaandika historia mpya kwa maisha na utume wa Kanisa la Tanzania, kwa Jimbo kuu la Tabora kuwa ni Makao makuu ya Kardinali wa tatu nchini Tanzania, sifa na utukufu apewe Mwenyezi Mungu.

Kardinali Protase Rugambwa anaandika historia mpya ya Jimbo kuu la Tabora.
Kardinali Protase Rugambwa anaandika historia mpya ya Jimbo kuu la Tabora.

Askofu mkuu Paul Runangaza Ruzoka anapenda kuchukua fursa hii kuwaalika watu wa Mungu ndani na nje ya Tanzania kuungana na familia ya Mungu Jimbo kuu la Tabora, Jumamosi tarehe 7 Oktoba 2023 kumpokea na kumkaribisha Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu Mwandamizi wa Jimbo kuu la Tabora anayerejea kutoka mjini Vatican ambako amehudhuria Ibada ya Kusimikwa kuwa ni Kardinali. Kardinali Protase Rugambwa, Dominika tarehe 8 Oktoba 2023 anatarajia kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya Ukardinali. Hii ni siku maalum kwa ajili ya kuyashangilia makuu ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya Kanisa la Tanzania, lakini zaidi kwa ajili ya Jimbo kuu la Tabora, ambalo limebahatika kushuhudia Baba Mtakatifu Francisko akiwasimika Makardinali wapya ishirini na moja kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, tarehe 30 Septemba 2023. Makardinali hawa sasa ni sehemu ya walinzi wa imani na washauri wakuu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kati yao watatu ni wale wanaotoka Barani Afrika. Furaha ya watu wa Mungu Jimbo kuu la Tabora ni kubwa zaidi kwa sababu ya uwepo wa Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu mwandamizi wa Jimbo kuu la Tabora.

Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu mwandamizi wa Jimbo kuu la Tabora
Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu mwandamizi wa Jimbo kuu la Tabora

Huu ni muda wa shukrani na shangwe kwa watu wa Mungu Jimbo kuu la Tabora, kwani tangu sasa Kardinali Protase Rugambwa anaandika historia mpya katika maisha na utume wa Kanisa la Tanzania kwa Tabora kuwa ni Makao makuu ya Kikardinali. Itakumbukwa kwamba, tarehe 25 Machi 1953 Papa Pio wa Kumi na Mbili aliyatangaza Majimbo ya Dar Es Salaam na Tabora kuwa ni Majimbo makuu. Na kunako mwaka 1968 Kardinali Laurian Rugambwa akahamia rasmi na kuchukua nafasi ya kuwa ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, nafasi iliyokuwa imeachwa wazi baada ya Askofu mkuu Edgar Maranta, OFMcap., kung’atuka kutoka madarakani. Kardinali Laurian Rugambwa akang’atuka kutoka madarakani kunako mwaka 1992 na kumwachia madaraka Askofu mkuu mwandamizi Polycarp Pengo. Tarehe 8 Desemba 1997 Kardinali Laurian Rugambwa, akafariki dunia na baada ya siku 40 tu za maombolezo, Mtakatifu Yohane Paulo II akamtangaza Askofu mkuu Polycarp Pengo kuwa Kardinali wa pili kutoka Tanzania na kusimikwa rasmi tarehe 21 Februari 1998 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Tarehe 30 Septemba 2023 Kardinali Protase Rugambwa ameandika ukurasa mpya wa historia ya Kanisa la Tanzania, kuwa ni Kardinali wa watu kutoka Tanzania na makao makuu yake yakiwa ni Jimbo kuu la Tabora ambalo kwa sasa linakuwa ni Jimbo kuu la Kikardinali. Shukrani, sifa na utukufu vinamwendea Mwenyezi Mungu na Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwatunuku watanzania, lakini hasa Jimbo kuu la Tabora lililo chini ya ulinzi na usimamizi wa Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu, Bikira na Mwalimu wa Kanisa, ambaye ni miongoni mwa wanawake wanne hadi sasa waliotangazwa na Mama Kanisa kuwa ni Walimu wa Kanisa.

Jimbo kuu la Tabora

 

06 October 2023, 15:59