Tafuta

Msalaba wake Kardinali VanThuan alioutengeneza wakati yuko kwenye magerezea Msalaba wake Kardinali VanThuan alioutengeneza wakati yuko kwenye magerezea 

Septemba 16 ni Kumbukumbu ya kifo cha Kardinali Xavier Nguyên Van Thuân

Kila tarehe 16 Septemba ni kumbukizi la kifo cha Mtumishi wa Mungu Kardinali François Xavier Nguyên Van Thuân,rais mstaafu wa Baraza la Kipapa la Haki na Amani.Mtu asiye wa kawaida wa ushuhuda wakati wa kifungo chake.Mnamo tarehe 4 Mei 2017,Papa Francisko aliidhinisha kutangazwa kwa amri ya mchakato wa kutangazwa kuwa Mtukufu.

Na Angella Rwezaukla, - Vatican.

Tarehe 16 Septemba ya kila mwaka ni kumbu kumbu ya kifo cha Kardinali  François Xavier Nguyên Van Thuân aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Haki na Amani kwa wakati ule. Ni mwanaume shuhuda maalumu wakati wa kufungwa kwake gerezani. Mnamo tarehe 4 Mei 2027 Baba Mtakatifu Francisko alitoa idhini ya kuendeleza mchakato wa utakatifu na kutangaza kuwa Mtumishi wa Mungu.  Kardinali François Xavier Nguyên Van Thuân, alizaliwa mnamo tarehe 17 Aprili 1928 huko Huê nchini  Viêtnam. Alitoka katika familia ambayo inaweza kuhesabu mashahidi wengi: mnamo 1885 wakaaji wote wa kijiji cha mama yake walichomwa moto katika kanisa la parokia, isipokuwa babu yake, ambaye alikuwa akisoma huko Malaysia wakati huo. Babu zake wa baba walikuwa waathiriwa wa mateso mengi kati ya 1698 na 1885.

Babu wa bibi yake, pamoja na washiriki wengine wa familia, walikuwa wametumwa kwa lazima kwa familia isiyo ya Kikristo ili apoteze imani yake. Na alisimulia historia  hiyo kwa kijana François Xavier. Walimwambia kwamba kila siku, akiwa na umri wa miaka 15, alitembea kilomita 30 kummpelekea baba yake mchele na chumvi kwa baba yake ambaye alikuwa gerezani kwa sababu ya kuwa Mkristo. Bibi yake, kila jioni, baada ya sala ya familia, bado alisali rozari kwa ajili ya makuhani. Hakujua kusoma wala kuandika. Mama yake Elisabeti alimlea Kikristo tangu alipokuwa mtoto mchanga. Kila jioni alimfundisha historia za Biblia na kumwambia shuhuda za wafia imani, hasa mababu zake. Alizungumza naye mengi kuhusu Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu. Mtoto wake alipokamatwa, mama yake aliendelea kusali kwamba daima aendelee kuwa mwaminifu kwa Kanisa, tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu, akiwasamehe watesi wake. Alipewa daraja la Upadre tarehe 11 Juni 1953.

Alimaliza masomo yake jijini  Roma, na kuhitimu katika Sheria ya Kanisa mnamo 1959. Baada ya kupata digrii yake Roma, alirudi Viêt Nam kama profesa na kisha mkuu wa seminari, Padre  na Askofu wa  Nha Trang (iliyechaguliwa tarehe 13 Aprili 1967 na kuwekwa wakfu tarehe 24 Juni iliyofuata). Kujitolea kwake huko Nha Trang kulikuwa na nguvu sana. Waseminari wakuu wametoka  idadi ya 42 hadi kufikia 147 katika miaka 8. Wale  wa seminari ndao kutoka 200 hadi 500. Zaidi ya hayo, alijitolea kuimarisha uwepo wa walei, vijana, na mabaraza ya wachungaji. Kisha akateuliwa kuwa Askofu Mkuu wa Vadesi na Mwandamizi wa Saigon (Thành-Phô Chi Minh, Hôchiminh Ville) na Papa Paulo VI tarehe 24 Aprili 1975. Kauli mbiu yake ya kiaskofu ilikuwa ni : ‘Gaudium et spes.’ Kwa hiyo mpango wake wa kichungaji ni: “Kanisa katika ulimwengu wa kisasa.” Baada ya miezi michache, hata hivyo, pamoja na ujio wa utawala wa kikomunisti alikamatwa na kuwekwa gerezani. Aliishi gerezani kwa miaka kumi na tatu, hadi tarehe 21 Novemba 1988, bila kesi au hukumu, akitumia miaka tisa katika kifungo cha upweke.

Wakomunisti walipofika Saigon walimshtaki mara moja kwa ukweli kwamba kuteuliwa kwake kuwa Askofu Mkuu kulitokana na njama kati ya Vatican na mabeberu. Baada ya miezi mitatu ya mvutano aliitwa kwenye Ikulu ya Rais, Ikulu ya Uhuru, ili akamatwe. Ilikuwa saa mbili usiku tarehe 15 Agosti 1975, katika Sherehe ya Kupalizwa Bikira Maria Mbinguni. Alikuwa na kasoksi na rozari tu mfukoni. Hakukubali kamwe kuzidiwa na kujiuzulu. Hakika, alijaribu kuishi kifungo chake kwa "kujaza kwa upendo", kama asemavyo. Tayari mnamo Oktoba alianza kuandika mfululizo wa ujumbe kwa jumuiya ya Kikristo. Quang, mvulana mwenye umri wa miaka 7, alimletea karatasi hizo kwa siri kisha akapeleka ujumbe huo nyumbani ili kaka  na dada zake waweze kunakili maandishi hayo na kuyaeneza. Hivvyo ndivyo kitabu kiitwacho: ‘Njia ya matumaini’ kilivyozaliwa. Hali hiyohiyo ilitokea mnamo mwaka 1980, katika makazi ya lazima huko Giangxà, Kaskazini mwa Vietnam, alipoandika, tena usiku na kwa siri, kitabu chake cha pili: ‘Njia ya matumaini katika mwanga wa Neno la Mungu na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na kisha kitabu cha tatu: ‘Mahujaji kwenye njia ya matumaini.’

Kwa minyororo alirudishwa kwenye eneo la Jimbo lake la kwanza , huko Nha Trang. Gereza halikuwa mbali na uaskofuni, kwa hiyo kwake ilikuwa tukio la kushangaza. Alipata nyakati ngumu sana kama vile kusafiri kwa meli na wafungwa 1500 wenye njaa na waliokata tamaa. Kisha katika kambi ya Vinh-Quang, katika milima, na  wafungwa wengine 250. Kisha kutengwa kwa muda mrefu, ambao ulidumu miaka tisa. Kulikuwa na walinzi wawili tu. Akiwa gerezani hakuweza kuchukua Biblia pamoja naye. Kwa hiyo, alikusanya vipande vyote vya karatasi alivyopata na kutengeneza shajara ndogo ambayo aliandika zaidi ya sentensi 300 kutoka katika Injili. Injili hii ilikuwa kitabu chake cha kila siku, kasha lake la hazina la thamani ambalo angeweza kupata nguvu. Adhimisho la Ekaristi lilikuwa wakati muhimu wa siku zake. Aliadhimisha Misa Takatifu katika kiganja cha mkono wake, kwa matone matatu ya divai na tone moja la maji. Alipokamatwa aliruhusiwa kuandika barua kuwauliza jamaa zake mambo muhimu zaidi. Kisha akaomba mvinyo kidogo kama dawa ya maumivu ya tumbo. Waamini walielewa maana ya kweli ya ombi hilo na mara moja wakampelekea chupa ndogo na divai ya Misa na kwa lebo: “dawa dhidi ya maumivu ya tumbo”. Ili kuhifadhi Sakramenti Takatifu hata alitumia karatasi kutoka katika pakiti za sigara. Akiwa gerezani pia aliweza kuunda jumuiya ndogo ndogo za Kikristo zilizokutana kusali pamoja na zaidi ya yote kuadhimisha Ekaristi. Usiku, ilipowezekana, alipanga zamu za kuabudu kabla ya Ekaristi.

Alikuwa katika kifungo cha upweke huko Hanoi wakati mwanamke polisi alipomletea samaki mdogo ambaye alipaswa kupika. Samaki alikuwa amefungwa katika kurasa mbili za  Gazeti la “Osservatore Romano”. Ilipofika Hanoi kwa njia ya posta, gazeti hilo liliombwa na kisha kuuzwa sokoni kama karatasi. Na hizo kurasa mbili zilikuwa zimetumika kufunga samaki kwa ajili ya Askofu Van Thuân. Bila kutambuliwa, aliosha hizo kurasa   mbili vizuri na kuziacha zikauke kwenye jua, na kuzihifadhi karibu kama masalio. Katika kutengwa kwake jela, kurasa hizo mbili zilikuwa ishara ya umoja  na Petro. Wakati wa kutengwa alizoea kusali Misa Takatifu karibu saa 9 alasiri wakati wa Yesu alikufa Msalabani. Akiwa peke yake, aliimba Misa kwa Kilatini, Kifaransa na Kivietinamu. Pia aliimba nyimbo za kikanisa na Ekaristi kama vile Te Deum, Pange Lingua, Veni Creator Spiritus. Mtazamo wake wa upendo uliwavutia sana walinzi. Kiasi kwamba wakuu wa polisi walimtaka kuwafundisha maafisa lugha. Hivyo watekaji wake pia wakawa wanafunzi wake. Katika milima ya Vinh Phù, katika gereza la Vinh Quang, alimwomba mlinzi ruhusa ya kukata kipande cha mbao katika umbo la msalaba.

Naye akamkubalia. Katika gereza jingine alimwomba mlinzi kipande cha waya wa umeme. Akiogopa kwamba alitaka kujiua, afisa huyo aliogopa. Askofu Van Thuân alimweleza kwamba alitaka kutengeneza mnyororo wa kubeba msalaba wake. Baada ya siku tatu mlinzi naye akapatatia kifaa na kwa pamoja wakatengeneza cheni. Daima alibeba msalaba huo na mnyororo huo pamoja, shingoni mwake. Aliachiliwa mnamo  tarehe 21 Novemba  1988, katika Sikukuu ya Uwasilishaji wa Maria Hekaluni. Akiwa anaandaa chakula cha mchana aliitwa na kupelekwa kwa gari hadi kwenye jengo ili kuonana na Waziri wa Mambo ya Ndani, yaani wa polisi. Waziri alimuuliza kama ana matakwa. Askofu Van Thuân alijibu kwamba alitaka kuachiliwa mara moja: “Nimekuwa gerezani kwa muda wa kutosha, chini ya Mapapa watatu: Paulo VI, Yohane  Paul I na Yohane  Paulo II. Na pia chini ya makatibu wakuu wanne wa Chama cha Kikomunisti cha Kisoviet: Brezhnev, Andropov, Chernenko na Gorbachev! Mara baada ya kuachiliwa, huko Geneva, mnamo mwaka wa 1992, aliteuliwa kuwa mjumbe wa Tume ya Kimataifa ya Kikatoliki ya Uhamiaji. Tarehe 24 Novemba 1994, kwa kuteuliwa kuwa Askofu Mkuu Mwandamizi wa Thành-Phô Chi Minh (Saigon), aliteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Baraza la Kipapa la Haki na Amani. Tarehe 24 Juni 1998 akawa Rais wa Baraza hilo hilo la Kipapa.

Alihubiri mafungo  ya kiroho ya Kwaresima kwa JPapa Yohane  Paul II na Curia Romana katika mwaka wa 2000. “Katika mwaka wa kwanza wa milenia ya tatu Mvietnamu utahubiri mafungo ya  kiroho kwa Curia Romana “ Mtakatifu Yohane Paulo II alimwambia mnamo tarehe 15 Desemba 1999. Papa alimtazama kwa makini akamuuliza: “Je, una wazo lolote akilini”.  Yeye alijibu “Baba Mtakatifu, nimepigwa na butwaa, nashangaa. Labda ningeweza kuzungumza juu ya matumaini” alijibu Van Thuân. Na Papa akasema “ Toa ushuhuda wako!” Mafungo  ya Kiroho ya Kwaresima yalianza  mnamo tarehe 12 Machi  katika Kikanisa cha  Redemptoris Mater mjini Vatican , na kumalizika tarehe 18 Machi 2000.

Siku hiyo hiyo, miaka 24  iliyokuwa imepita, alikuwa amechukuliwa kutoka katika makao ya kulazimishwa ya Cay-vong na kutengwa kwa ukali. katika gereza la Phu-Khanh. Katika hitimisho la Mfungo ya Kiroho,  Papa Yohane Paulo II alisema: “Namshukuru Monsinyo mpendwa François Xavier Nguyên Van Thuân ambaye kwa urahisi na uvuvio wa kiroho alituongoza katika kuimarisha wito wetu kama mashahidi wa matumaini ya Kiinjili mwanzoni mwa milenia ya tatu. Yeye mwenyewe akiwa shahidi wa msalaba wakati wa miaka mingi ya kifungo huko Viêt Nam, alituambia mara kwa mara ukweli na matukio ya kifungo chake chenye uchungu, na hivyo kututia nguvu katika uhakika wa kufariji kwamba wakati kila kitu kinapoanguka karibu nasi na labda hata ndani yetu, Kristo anabaki kuwa wetu. msaada usio na kikomo.”

16 September 2023, 13:47