Tafuta

Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii tarehe 29 Mei 2023 limechapisha Waraka unaojulikana kama: “Kuelekea Uwepo Kamili. Tafakari ya Kichungaji juu ya Ushirikiano na Mitandao ya Kijamii” Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii tarehe 29 Mei 2023 limechapisha Waraka unaojulikana kama: “Kuelekea Uwepo Kamili. Tafakari ya Kichungaji juu ya Ushirikiano na Mitandao ya Kijamii”  (ANSA)

Waraka: Kuelekea Uwepo Kamili. Tafakari ya Kichungaji Juu ya Ushirikiano na Mitandao ya Kijamii

Mama Kanisa anakazia umuhimu wa mawasiliano ya jamii, siyo tu yale yanayowaunganisha watu, bali mawasiliano yasaidie kunogesha utamaduni wa kuheshimiana na kuthaminiana, majadiliano katika ukweli na uwazi pamoja na ujenzi wa urafiki wa kijamii. Baba Mtakatifu Francisko anasema, mitandao ya kijamii ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya mwanadamu kila kukicha! Mitandao ya kijamii ni kielelezo cha umoja na ushirika wa watu wa Mungu katika ujumla wao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii tarehe 29 Mei 2023 limechapisha Waraka unaojulikana kama: “Kuelekea Uwepo Kamili. Tafakari ya Kichungaji juu ya Ushirikiano na Mitandao ya Kijamii” "Towards Full Presence. A Pastoral Reflection on Engagement with Social Media.” Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano yamewezesha watu kujisikia kuwa ni majirani wanaopendana. Maendeleo haya yamewezesha pia kuibuka kwa matumizi ya akili bandia na kwamba mitandao ya kijamii imekuwa ni mahali muafaka pa vijana wa kizazi kipya kukutana. Kimsingi, watu wengi wanajipambanua katika ulimwengu wa kidigitali. Ni katika muktadha huu, waamini wengi wanaomba mwongozo wa matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii kwa sababu matumizi yake yana athari kubwa katika jamii ya waamini na hata katika ngazi ya mtu mmoja mmoja katika safari ya maisha yake ya kiroho. Makanisa na taasisi mbalimbali zinazoendeshwa na Mama Kanisa zimejitahidi kuandaa miongozo kwa ajili ya matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii. Mama Kanisa anakazia umuhimu wa mawasiliano ya jamii, siyo tu yale yanayowaunganisha watu, bali mawasiliano yasaidie kunogesha utamaduni wa kuheshimiana na kuthaminiana, majadiliano katika ukweli na uwazi pamoja na ujenzi wa urafiki wa kijamii. Baba Mtakatifu Francisko anasema, mitandao ya kijamii ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya mwanadamu kila kukicha! Wakati wa maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko uliweza kuwafikia mamilioni ya watu wa Mungu kwa njia ya mitandao ya kijamii, hiki ni kielelezo cha umoja na ushirika wa watu wa Mungu katika ujumla wao. Kumbe, kusudi mahususi la Waraka huu wa kichungaji wa “Kuelekea Uwepo Kamili. Tafakari ya Kichungaji juu ya Ushirikiano na Mitandao ya Kijamii” "Towards Full Presence. A Pastoral Reflection on Engagement with Social Media” unapania pamoja na mambo mengine kutoa tafakari ya jumla mintarafu mang’amuzi yanayoibuliwa katika ulimwengu wa kidigitali, ili kuwahamasisha watu binafsi na jumuiya za waamini kujenga utamaduni wa ujirani mwema, amani na maana halisi ya maisha kwa kumtambua jirani yako ni nani katika mitandao ya kijamii, ili hatimaye, uweze kuurithi ufalme wa Mbinguni.

Mawasiliano yajenge utamaduni wa kuheshimiana na kutaminiana
Mawasiliano yajenge utamaduni wa kuheshimiana na kutaminiana

Mitandao ya kijamii ni sehemu tu ya ulimwengu wa kidigitali ambao umeendelea kuboresha medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu na sasa kuna mageuzi makubwa yanayofanyika hata katika masuala ya kisiasa na kiuchumi kwa mashine kuchukua nafasi ya nguvu kazi ya binadamu katika uzalishaji na huduma. Mitandao ya kijamii inaendelea kutoa maana na utambulisho wa kijamii na mahali ambapo tunu msingi za kijamii zinatangazwa na kushuhudiwa. Miaka kadhaa iliyopita, watu walipoanza kutumia internet kwa mawasiliano, matumaini yalianza kuibuka na hivyo kuleta furaha ya kwamba hapa pangekuwa ni mahali pa uelewa wa kawaida, upatikanaji huru wa habari na kwamba, matumizi ya Internet yalikuwa ni kama kufikia “Nchi ya Ahadi.” Mahali ambapo watu wengi wangetegemea kupata na kushirikishana habari kwa msingi wa ukweli na uwazi; uaminifu na kitaaluma. Kwa bahati mbaya kuna makosa yanayopaswa kuepukwa katika matumizi ya mitandao ya kijamii, kwani bado kuna ukosefu mkubwa wa usawa katika matumizi ya ulimwengu wa kidigitali. Kuna watu wanakosa mahitaji msingi, wanakosa teknolojia na mawasiliano na hivyo mitandao ya kijamii kuonekana kuwa inaendelea kuwagawa watu badala ya kuwa ni watumiaji wa mitandao ya kijamii, sasa wamegeuka na kuwa ni walaji wa kutupwa wa mitandao ya kijamii na kwamba, takwimu za walaji zimekuwa zikitumika kwa ajili ya faida ya wamiliki wa mitandao ya kijamii. Watumiaji wa mitandao ya kijamii wamekuwa wakishirikisha taarifa zao na hata pengine kuimarisha utambuzi wao wa kiimani. Kuna hatari kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii kukutana na wale wanaofikiri tofauti na wao; watu wengi wanaathirika kwa chuki na uhasama, migawanyiko pamoja na mipasuko ya kijamii na kwamba, kuna idadi kubwa sana ya watu wa Mungu wanaoachwa nyuma ya maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano.

Mitandao ya kijamii isaidie kujenga urafiki wa kijamii
Mitandao ya kijamii isaidie kujenga urafiki wa kijamii

Mitandao ya kijamii isaidie kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kijamii, kwa kujenga ujirani mwema, kama ilivyokuwa kwa mfano wa Msamaria mwema, ili kweli jukwaa la mitandao ya kijamii liweze kuwa ni mahali pa kushirikishana habari, kushirikiana, kwa kujisikia kuwa ni sehemu muhimu sana ya mawasiliano na kwamba, mitandao hii iwe ni mahali pa kuaminiana. Mitandao ya kijamii iwe ni jukwaa la kujenga mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala na maisha ya Kisakramenti. Huu ni mwaliko wa kujenga utambuzi na hatimaye, kujenga makutano ya kweli, kwa kujenga wasikilizaji wa kweli, kwa kukazia usikivu mwanana, ili kuweza kusikiliza kwa sikio la moyo, tayari kufanya mang’amuzi ya uwepo mwanana kwenye mitandao ya kijamii. Huu ni mwaliko wa kutoka katika mwelekeo wa watu kukutana na kuanza ujenzi wa jumuiya ya watu wanaowasiliana uso kwa uso kama ilivyokuwa kwa yule Msamaria mwema na kwa Zakayo mtoza ushuru tayari kuganga na kuponya madonda yanayosababishwa na mitandao ya kijamii, tayari kujenga udugu wa kijamii na kuendelea kuwa ni Wasamaria wema tayari kuwainua wale walioteleza na kuanguka kwa njia ya: ushuhuda, majadiliano katika ukweli na uwazi; upatanisho na mafungamano ya kijamii, bila kusahau ukarimu, ili kuondokana na upweke hasi unaojengwa kwa njia ya mitandao ya kijamii. Huu ni mwaliko wa kujenga mitandao ya kijamii yenye afya na mazingira bora zaidi ya mawasiliano ya kijamii. Kanisa ni jumuiya ya kiimani inayosafiri hapa duniani kuelekea kwenye Ufalme wa mbinguni. Inasikitisha kuona kwamba, wakati mwingine matangazo ya Ibada ya Misa Takatifu yanatumiwa kama sehemu ya biashara! Hapa kuna haja ya kutafakari kwa kina kuhusu ushiriki mkamilifu wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, kwa kujenga uelewa mzuri kuhusu umuhumu wa kupokea Ekaristi Takatifu tayari kujenga ushirika wa waamini kila mara waamini wanapokusanyika kwa ajili ya Ibada ya Misa Takatifu.

Mitandao ya kijamii isaidie mchakato wa uinjilishaji mpya.
Mitandao ya kijamii isaidie mchakato wa uinjilishaji mpya.

Mwanadamu anawasiliana kwa njia ya roho na mwilI, akili na moyo wake na kila kitu alicho nacho! Kumbe, kipaji cha ubunifu wa upendo kiwe ni kielelezo cha mawasiliano ya kweli na mazuri yanayojikita katika ubora wa maudhui yanayopania kujenga na wala si kubomoa; kwa kuwajengea watu uwezo wa kutangaza na kushuhudia nguvu ya mawasiliano ya pamoja, tayari kujenga na kudumisha ushirika. Simulizi la historia ya maisha ya mtu lina mvuto na mashiko katika mchakato wa ujenzi wa jumuiya ambayo kimsingi inajengwa kwa njia ya mawasiliano; kwa kurejesha mahusiano na mafungamano ya kijamii kama majirani wema na kwa njia hii, kushiriki pia katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaosimikwa katika ushuhuda wa maisha unaochochea toba na wongofu wa ndani. Waraka huu wa kichungaji wa “Kuelekea Uwepo Kamili.Tafakari ya Kichungaji juu ya Ushirikiano na Mitandao ya Kijamii” unakazia umuhimu wa ujenzi wa jumuiya katika ulimwengu wenye kinzani na mipasuko mbalimbali, mahali pa kukuza na kudumisha mawasiliano mema na hivyo kuepuka mashambulio. Mwamini atambue umuhimu wake kwenye mitandao ya kijamii ili iwe ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wake na wala si kwa ajili ya kujimwambafai. Waamini wajenge tabia ya kufanya tafakari ya kina na ushiriki mkamilifu tayari kujenga Kanisa la Kisinodi. Waamini kwenye vyombo na mitandao ya kijamii wawe ni mashuhuda wa Kristo Yesu na Kanisa lake, wawe ni mashuhuda wa imani tendaji, yenye mvuto na mashiko, ili watu wawe na maisha tele! Bikira Maria katika maisha na utume wake, amejipatia umaarufu mkubwa kwa kukubali mpango wa Mungu katika maisha yake.

Mawasiliano

 

10 August 2023, 16:50