Sudan Kusini:Askofu wa Malakal amesema Kard.Parolin ameleta matumaini
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Tangu tarehe 14 Agosti, Katibu wa Vatican, Kardinali Pietro Parolin yuko Nchini Sudan Kusini hadi tarehe 17 Agosti 2023. Katika ziara yake ya tarehe 15 Agosti alikwenda katika Jimbo la Malakal . Katika fursa hiyo Askofu Stephen Nyodho Ador Maiwok wa Jimbo Katoliki la Malakal, amefafanua juu ya matumaini ambayo anafikiri yanabaki kwa waamini na watu wenye mapenzi mema ambao walifika na kumwona Kardinali Pietro Parolin. Hayo yamethibitishwa wakati akizungumza na mwandishi wa habari wa Radio Vatican/Vatican news ambapo Askofu Stephen alisema: “Uwepo wa Kardinali Parolin huko Malakal kwa hakika ni muhimu sana, ni ziara inayotoa matumaini, inayoleta upendo wa Kanisa, ziara inayodhihirisha ukaribu na mshikamano wa Kanisa Katoliki kwa watu wanaoteseka".
Askofu wa Jimbo la Malakal aidha alisema "Ziara ya Kardinali itawasaidia watu kuelewa kwamba kufanya kazi kwa pamoja, kwa umoja kati ya jumuiya mbalimbali, kutawapa nguvu kubwa ya kwenda mbele, kujenga nchi yao na jimbo lao.” Kardinali Parolin akiwa huko asubuhi tarehe 16 Agosti 2023 aliwakaribisha wakimbizi waliokimbia vita nchini Sudan na ambao walifika kwa mtumbwi na kuongozana nao kwenye mtumbwi huo hadi kituo cha mapokezi.
Katika siku kuu ya Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni tarehe 15 Agosti, Kardinali Parolin akiwa huko Malakal, aliongoza misa Takatifu katika Kanisa kuu na baadaye alikutana na wakimbizi katika kituo cha mapokezi. Hadi sasa huko Malakal, kaskazini mashariki mwa Sudan Kusini ambapo Jimbo la Malakal linajumuishwa ndani ya Wilaya ya Upper Nile, Jonglei na Unity, zaidi ya watu 42,000 wamewasili, na takriban 35,000 wamehamishwa, na mara nyingi katika maeneo ambayo kuna baadhi ya wanafamilia. Wakimbizi wengi ni raia wa Sudan Kusini ambao wamehamia Khartoum kwa miaka mingi. Kwa ujumla kuna Wasudan Kusini milioni 1.5 ambao wamewasili Sudan, na wengi wao sasa wanarejea kutokana na kutoroka vita vinavyoendelea vya wenyewe kwa wenyewe.
Nchini Sudan Kusini yote inakadiriwa kuwa karibu watu 200,000 wamewasili. Wakimbizi hao wanapowasili, karibu kila mara wameibiwa kila kitu, wengi huchukuliwa kutoka mpakani hadi Malakal kwa mtumbwi wa mizigo ya Jimbo ambao kwa kawaida husafirisha nafaka, lakini ambayo sasa inatumika kwa ajili ya watu, kati ya 400 na 800 kwa safari moja. Na hivyo takriban siku 2-3. Mtumbwi huo huo ambao Kadinali Parolin alipanda tarehe 16 Agosti 2023. Na kufika hadi sasa ni watu 3,000 ambao wamesafirishwa na mfumo huo. Kwa mujibu wa Askofu Nyodho Ador Maiwok katika maelezo kwa Vatican New, amethibitisha kuwa Jimbo hilo ni mojawapo ya walioathirika zaidi na majanga ya asili na pia imeharibiwa na vita. Jimbo hilo sasa linapokea maelfu ya watu wanaokimbia vita nchini Sudan. Kwa hiyo Jimbo la Malakal, lilikuwa moja ya kuanza kuingilia kati na kuunda daraja la kuwaleta wakimbizi kutoka mpaka na Sudan hadi Malakal.
“Watu hapa wanahitaji amani na upatanisho, wanahitaji umoja, kama Papa alivyoonesha alipokuja mwezi Februari uliopita. Na ziara ya Kardinali sasa ina maana kubwa sana kwetu, itasaidia watu kuelewa kwamba ni lazima tuwe wamoja, tuwe na nguvu ya kusonga mbele, hata kama si rahisi, maana ni wale wale waliogombana wenyewe kwa wenyewe ambao waliua kila mmoja, na hivyo inachukua muda mrefu kuwaleta pamoja. Ilikuwa ni ziara ya Papa ambayo ilitupatia nguvu kubwa na matumaini makubwa ya upatanisho kati ya watu wa Nile, ambayo ni muhimu sana,” alisema Askofu wa Malakal.
Askofu Nyodho Ador Maiwok, akiendelea alisema “Vita vilileta uharibifu na uporaji, na hakuna chochote kilichosalia hapa, watu wanaokuja nyumbani kwako wanawezaje kusaidiwa katika hali hii? Mfano anaoufanya Kardinali ni wa huruma kwani safari moja ya kuleta watu kutoka mpaka hadi Malakal inagharimu dola elfu 7 hadi nane, kwa ajili ya mafuta tu, baada ya hapo unapaswa kutoa chakula, makazi, na sasa magonjwa pia yanalipuka.” Kwa kuongeza amesema “Hatuwezi kubaki tumeketi, ndiyo maana tunajaribu kusonga mbele, ili kufanya kile tunachoweza, kulingana na uwezo wetu. Wito ni kwa jumuiya ya kimataifa, kwa washirika, kwa watu wenye mapenzi mema, kwa sababu hali hapa inahitaji watu wenye mapenzi mema, inahitaji ubinadamu, ili tuweze kusaidia.
Kwa kuhitimisha Askofu wa Malakal maelezo yake ni ya kusikitisha kwamba, “kumekuwa na mateso na wanaendelea kuteseka sana. Mvua inanyesha siku hizi, ni msimu wa mvua, na watu hawana chochote cha kujifunika, na watoto na wazee wanahitaji msaada mkubwa.”