Papa Francisko amekutana na Rais Rajoelina wa Madagascar
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko tarehe 17 Agosti 2023, amekutana na Bwana Andry Nirina Rajoelina, Rais wa Jamhuri ya Madagascar ambaye mara baada ya mkutano huo amekutana na Monsinyo Miroslaw Wachowski, Katibu msaidizi wa Vatican kwa ajili ya Mahusiano na Nchi.
Kwa mujibu wa Taarifa kutoka Ofisi ya Vyombo vya habari vatican imeeleza kuwa Rais wa Madagascar alifika saa 5.00 kamili na kuhitimisha mazungumzo saa 5.20, wakati huo huo mkutano wote umemalizika saa 5.30. Katika mazunguzmo yao na Katibu Msaidizi wa Vatican viongozi hawa, wamepongezana kuhusu uhuasiano wao chanya uliopo kati ya nchi hizi mbili, ikiwa ni pamoja na mchango wa Kanisa Katoliki katika sekta nyingi za jamii ya Madagascar.
Katika mwendelezo wa mazungumzo hayo, walijikita pia juu ya masuala mbalimbali ya kitaifa na kimataifa, ikiwa ni pamoja na vita vya Ukraine na matokeo yake ya kimataifa, hali ya mgogoro inayoathiri bara la Afrika na uwezekano wa kuendelea na utafiti wa kuandaa rasimu ya makubaliano baina ya nchi hizo mbili kama ishara zaidi ya ushirikiano wa heshima.
Kama kawaida ya ugeni huo na mkutano huo wa faragha kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Rais wa Madagascar, mara baadaye Baba Mtakatifu amekaribisha ujumbe uliomsindikiza Rais na kupiga picha pamoja wakiwa mbele ya picha ya Meli ambayo Papa alizawadiwa wakati wa Hija yake ya Kitume nchini Madagascar. Baadaye wamesali pamoja mbele ya picha ya Maria aliyozawadiwa na Maaskofu wa Madagascar, na kuhitimisha akiwabariki.
Katika kupeana zawadi, Baba Mtakatifu ametoa Hati za kipapa ambazo ni: Ujumbe wa Amani kwa mwaka 2023, Hati za kipapa na Kitabu cha Statio Orbis kunachelezea Njia ya Msalaba ya tarehe 27 Machi 2020,katikati ya Janga la Uviko, kilichaoandaliwa na nyumba ya vitabu ya Vatican(LEV). Na zawadi ya Sanamu ya shaba yenye ujumbe: “Kuweni Wajumbe wa Amani”
Kwa upande wake Rais wa Madagascar, Bwana Andry Rajoelina amemzawadia Papa Mchoro unaoonesha mandhari ya maisha ya wakulima wa Malagashi na Mchezo wa 'Solitaire', wenye marumaru yaliyotengenezwa kwa mawe mahalia.