Tafuta

15 Agosti Kupalizwa mbinguni Mama Maria 15 Agosti Kupalizwa mbinguni Mama Maria  (©e55evu - stock.adobe.com)

Agosti 15:Siku Kuu ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni Mwili na Roho

Kupalizwa kwa Bikira Maria mbinguni huadhimishwa kila ifikapo Agosti 15.Kwa kuwa Mama wa Yesu,Mwana wa Pekee wa Mungu na kwa kukingiwa na doa la dhambi,Maria,kama Yesu,alifufuliwa na Mungu.Hii ni kutaka kukumbuka kuwa mnamo tarehe Mosi Novemba 1950,Papa Pio XII alianzisha siku hii kwa hati ya Munificentissimus Deus, yaani,“Mungu Mkarimu".

Na Angella Rwezaula, - Vatican

Kila tarehe tarehe 15 Agosti ya kila mwaka kadiri ya kalenda ya kiliturujia ya Kanisa Katoliki, Mama Kanisa anaadhimisha Siku kuu ya kupalizwa mbinguni kwa Mama Bikira Maria. Hii ni kutaka kukumbuka kuwa Mama Kanisa mnamo tarehe Mosi Novemba 1950 katika mamlaka aliyokabidhiwa na Kristo, Baba Mtakatifu Pio XII kwa andiko lake la  hati ya Munificentissimus Deus, yaani, “Mungu Mkarimu”. alifundisha wazi wazi na kwa milele kuwa Mama Bikira Maria aliyekingiwa dhambi ya asili ili amzae Mwana wa Mungu, aliyempatia Jina  Yesu Kristo damu yake ya kibinadamu, akamsindikiza mwanae  mpaka chini ya msalaba, alipalizwa mbinguni mwili na roho. Makanisa ya Kiorthodox huadhimisha sikukuu ya kulala kwa  Bikira siku hiyo hiyo. Kwa hiyo kupalizwa mbinguni mwili na roho ni tuzo kubwa kutoka kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Kila mwaka, kwa njia hiyo ni kukumbushwa fundisho hili la kupalizwa mbinguni mwili na roho. Na  Kanisa ambalo linainua maombi yake kwa Mungu, kwa njia ya Roho Mtakatifu wa ukweli, katika unyenyekevu na udumifu ilifunuliwa wazi  na Mungu mwenyewe kuwa Bikira Maria amepalizwa mbinguni.

Katika maadhimisho haya tufurahi kushirikishwa kwa Mama Bikira Maria katika utukufu wa mwanaye, Yesu Kristo ambaye ni Mkombozi pekee wa ulimwengu. Utukufu ambao mama huyu ameushiriki tangu mwanzo wa fumbo la umwilisho, yaani Yesu Kristo kutwaa mwili wa kibinadamu kwa njia yake. Ni Pale tu alipotikia “Tazama mimi hapa”. Lakini si hilo tu bali kupalizwa mbinguni kunaambatana na fumbo la Pasaka ambapo tunakiri wazi Bikira Maria alimsindikiza mwanae mpaka chini ya msalaba huku akishuhudia mateso. Kwa namna hiyo basi Mwana asingeweza kumwacha mamaye aoze kaburini, lazima amtuze zawadi hiyo ya kupalizwa mbinguni. Kumbe Kanisa linapiga vigelegele kwa sababu ya kutukuzwa kwa Mama wa Mungu  tunda la ufufuko.

Katika kitabu cha Mwanzo, tunaona madhaifu ya wazazi wa kwanza, Adamu na Eva, ambao kwa njia yao kifo kiliingia duniani, daima  na mara moja tangazo la upendo kutoka kwa Mungu likatolewa kwa mwanadamu ambapo tunasoma: “Nitaweka uadui kati yako wewe na huyo mwanamke” (Mw 3:15), kwa sababu joka lile  lililoleta anguko kwa wazazi wa kwanza na ndiyo maana Mungu anaeleza kwamba atawekwa uadui huo kwa njia ya mwanamke. Kwa vyovyote vile mwanamke huyu asingeweza kuwa Eva kwa maana Eva na nyoka walifanya urafiki. Ni lazima awe mwanamke mwingine mpya hasa.

Na kwa kadiri ya Mafundisho ya mababa na walimu wa Kanisa Mwanamke huyo ni Mama Bikira Maria, yaani ni Eva mpya; ni yule ambaye wokovu utaingia duniani kwa njia ya utii  wake kwa Mungu.  Kwa sababu, Mama Maria alipotembelewa na Malaika Gabrieli akimpashwa habari,  Maria aliitikia: “Tazama Mimi ni mtumishi wake Bwana na nitendewe kama ulivyonena.” Na katika hilo, tunampata hata Adamu mpya ambaye ni Yesu Kristu Masiya atakayetangaza uadui dhidi ya kifo yaani utawala wa shetani. Kristu mshindi wa kifo, aliye Adamu mpya hakuacha kumshirikisha mama kwa karibu katika vita dhidi ya kifo na kwa namna hiyo, kiukweli  Yesu na Maria wako pamoja katika uadui dhidi ya nyoka kielelezo cha mwovu shetani.

Kwa upande wa Agano Jipya, Bikira Maria alipokea salamu  ya kipekee kutoka kwa Malaika Gabrieli alimwambia: “salaamu Maria ewe uliyebarikiwa na Mungu na  Bwana yuko nawe” (Rej. Lk 1:28).  Ni salamu ya heshima kubwa kabisa yenye kuonesha kuwa tangu mwanzo wa maisha yake na hata mwisho hana doa la dhambi. Na hivyo hayuko chini ya utawala wa kifo kilicho na tabia ya dhambi. Ni mkingiwa dhambi ya asili na kwa namna yoyote angepalizwa mbinguni mwili na roho yake. Kwa kuambiwa kubarikiwa zaidi ya wanawake wote alipatata baraka ya kipekee, yaani amejaa neema tangu kuumbwa kwake na kwa sababu hiyo,  uwepo wa Bwana ni mkamilifu katika Yeye. Na Baraka aliyoipokea mama Bikira Maria ikawa ni kinyume na laana ya kale ya kurudi mavumbini kwa wazazi wetu wa kwanza (Rej. Mw 3:19). Ni dhahiri kabisa kuwa  kama ilivyokuwa wa Kristo kushinda mauti ya kifo kilicholewa na Adamu ndivyo sasa Maria anakuwa mshindi  kabisa dhidi ya kifo kilicholetwa na Eva.

Kwa ushindi huu wa Bikira husingekosa  zawadi ya kushiriki utukufu wa Mwanae kabla ya wanadamu wengine wote, na ndiyo maana kupalizwa mbinguni. Kupalizwa Mbinguni ni kuendeleza ushindi na ni mlango wa kumfuasa Kristo katika kuingia mbinguni kwetu sisi tuliokabidhiwa kwake pale chini ya msalaba. Yesu Mwenyewe alisema kwa Mwanafunzi wake Yohane: “Mama tazama huyu ndiye mwanao.” Na kumbe Yeye ni Mama hawezi kutuacha katika shimo la machozi na mahangaiko ya ulimwengu huu. Hatuna budi kufurahi sana, katika siku ya leo ambapo Mama anapalizwa Mbinguni. Tushangilie katika nafasi kubwa ya maisha ya akina mama wote kwa kutazama mshindi na mfano bora kwa mama wote, Mama Maria,  mama yetu mtukuka, ambaye ni tunda la kwanza la ukombozi ni ushindi wa akina mama wote, na ni ushindi wa familia zote hasa zile ambazo zinafanya kweli mapenzi ya Mungu.

Ninawatakia heri ya Siku kuu njema ya Bikira Maria Kupalizwa Mbingini Mwili na Roho!

Siku Kuu ya Kupalizwa Mbinguni Bikira Maria
14 August 2023, 16:28