Ujumbe wa Utume wa Bahari Kwa Mwaka 2023: Mchango wa Mabaharia na Wavuvi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Utume wa Bahari, “Apostolatus Maris” unaojulikana na wengi kama “Stella Maris” ulianzishwa tarehe 4 Oktoba 1920 na waamini walei wanaoshiriki: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo Yesu. Ni jukumu na wito wa waamini walei kuutafuta Ufalme wa Mungu wakiyashughulikia mambo ya dunia na kuyaelekeza kadiri ya mpango wa Mungu. Wanaitwa kuyatimiza majukumu yao wenyewe wakiongozwa na roho ya Kiinjili, ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa imani, matumaini na mapendo thabiti! Ili kuonesha na kushuhudia ukaribu wa Kanisa kwa mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao, Papa Pio XI tarehe 17 Aprili 1922 aliridhia kuanzishwa kwa Utume wa Bahari. Leo hii kuna jeshi kubwa la watu wanaojisadaka zaidi kuwadumia mabaharia na wavuvi katika bandari 300 kwa kutembelea meli zisizopungua 70,000 kwa mwaka. Mama Kanisa anawashukuru kwa dhati Mitume hawa wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma makini kwa mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao. Wadau wa Utume wa Bahari wamekuwa ni mashuhuda na vyombo vya uinjilishaji wa kina kwa kuwafunulia watu wa Mungu ile sura pendelevu ya Mama Kanisa: kwa kuonesha ukaribu wake kwa watu watakatifu wa Mungu na hivyo kuwahamasisha kujisikia kuwa ni sehemu hai ya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Takribani miaka 100 iliyopita, imekuwa ni kipindi muafaka cha ujenzi wa misingi ya majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni kutokana na mwingiliano wa watu kutoka katika dini, tamaduni na mataifa mbalimbali duniani.
Mama Kanisa tarehe 9 Julai 2023 anaadhimisha Dominika ya Utume wa Bahari, fursa kwa Familia ya Mungu sehemu mbalimbali za dunia, kumshukuru Mungu kwa huduma na mchango mkubwa unaotolewa na mabaharia pamoja na wavuvi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni siku maalum ya kutambua na kuthamini sadaka ya watu hawa ambao wakati mwingine: haki, utu na heshima yao vinahatarishwa kutokana na changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wakati wa kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa jamii. Hii ni siku maalum ambayo Kanisa linatambua mchango mkubwa unaotolewa na Mabaharia katika ustawi na maendeleo ya binadamu katika nyanja mbalimbali za maisha. Maadhimisho haya pia yana mwelekeo wa kiekumene, kwani yanawashirikisha Wakristo kutoka katika Makanisa na madhehebu mbalimbali ya Kikristo, ili kuonesha moyo wa upendo na mshikamano na mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao. Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu katika ujumbe wake kwa mwaka 2023, linajikita zaidi kubainisha umuhimu wa Dominika ya Utume wa Bahari, mchango wa mabaharia na wavuvi katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi sehemu mbalimbali za dunia pamoja na kuonesha ukaribu wa Mama Kanisa kwa mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi.
Kardinali Michael Czerny, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu, katika ujumbe wake kwa Dominika ya Utume wa Bahari kwa Mwaka 2023 anasema, tangu mwanzo wa Kanisa, mabaharia wamekuwa ni wahudumu wakuu wa Habari Njema ya Wokovu, waliobahatika kushiriki maisha na wafuasi wa Kristo Yesu, kiasi cha kufungua akili na nyoyo zao kwa imani. Dominika ya Utume wa Bahari inatoa fursa kwa jumuiya za waamini sehemu mbalimbali za dunia kujizatiti katika kukuza na kudumisha asili yao pamoja na kusali kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao, wanaojihusisha na usafirishaji wa bidhaa sehemu mbalimbali za dunia, ambao ni zaidi ya mabaharia milioni moja, hao ndio wanaosaidia kuendesha gurudumu la uchumi wa dunia. Hawa ni watu ambao ni vigumu sana kutambua imani, matumaini na mapendo yao. Dominika kimsingi ni siku ya Mungu, Siku ya Kristo Yesu, Siku ya Kanisa, ni Siku ya Binadamu kupumzika na hivyo kushiriki katika maadhimisho ya Pasaka ya Bwana, kila juma, lakini waamini wengi wanashindwa kuhudhuri Ibada ya Misa Takatifu kwa sababu ya umbali na kwamba, wanalazimika kuwemo kazini. Mama Kanisa katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu anasali na kuwakumbuka wote hawa, ili hatimaye, waweze kupata wokovu, kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki zao msingi kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Katika maisha na utume wao, Mitume wa Yesu walimkaribisha Kristo Yesu mashuani mwao na hivyo kujenga jumuiya ya wavuvi baharini. Huu ni ulimwengu ambao bado umefichama sana na hivyo kukosa usawa. Kumbe, huu ni mwaliko kwa kila Jumuiya ya Kikristo kujikita katika maboresho ya maisha ya roho zao kwa kumshukuru Mungu kwa zawadi ya huduma ya mabaharia pamoja na wavuvi, wanaowasaidia kuboreshsa maisha kwa bidhaa wanaozasafirisha kila kukicha. Kardinali Michael Czerny anapenda kuwatangazia mabaharia na wavuvi kwamba, Mama Kanisa yuko karibu sana nao na anataka kuwatangazia furaha ya Injili na kwamba, anataka kujitahidi kutatua changamoto zinazowasibu mabaharia pamoja na wavuvi katika maisha na utume wao. Kama Jumuiya ya waamini, Kanisa liko tayari kusikiliza na kupokea: historia na shuhuda zao za maisha; mtazamo wao kuhusu kazi, uchumi, kukoleza majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni. Mama Kanisa anataka kufahamu hali halisi ya maisha yao wakiwa baharini na nchi kavu, lakini zaidi Kanisa linataka kufahamu imani yao. Uzoefu na mang’amuzi yao yanaweza kuwafikia na hatimaye, kuwachangamotisha waamini na kwa njia yao, changamoto hizi zinaifikia jamii nzima. Hii ni sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi kwa kutembea kwa pamoja, bila kumwacha mtu awaye yote, ili kutajirishana, kwa kutambua kwamba, kila mtu analo jambo la kuwashirikisha wengine. Huu ni mwaliko kwa mabahari na wavuvi kushikamana, ili kazi, majukumu na imani yao viweze kuwa ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko.