Tafuta

Ijumaa tarehe 7 Julai 2023 Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu imechapisha orodha ya majina 363 ya wajumbe wa Sinodi ya ya XVI ya Maaskofu, kati yao kuna wanawake 54 wenye haki ya kupiga kura. Ijumaa tarehe 7 Julai 2023 Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu imechapisha orodha ya majina 363 ya wajumbe wa Sinodi ya ya XVI ya Maaskofu, kati yao kuna wanawake 54 wenye haki ya kupiga kura.   (Vatican Media)

Orodha ya Majina ya Wajumbe wa Sinodi ya XVI ya Maaskofu Kutoka Afrika Mashariki na Kati

Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu imechapisha orodha ya majina 363 ya wajumbe wa Sinodi ya ya XVI ya Maaskofu, kati yao kuna wanawake 54 wenye haki ya kupiga kura. Wajumbe kutoka katika Makanisa ya Mashariki ni 20, Kanisa Barani Afrika ni 43, Amerika ni 47, Barani Asia ni 25, Ulaya 48, Oceania 5. Maaskofu wasiokuwa na Baraza la Maaskofu ni mmoja ambaye ameteuliwa. Wamo pia Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi na Askofu Flavian Matindi Kassala!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yananogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Lengo kuu la Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ni kuliwezesha Kanisa kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza na kuwashirikisha waamini walei katika maisha na utume wake. Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu yanapania pia kujenga na kudumisha urika wa Maaskofu, tayari kumsikiliza Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha. Huu ni utamaduni wa watu wa Mungu kusikilizana kwa makini! Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yamegawanywa sasa katika awamu kuu mbili. Awamu ya kwanza ni kuanzia tarehe 4 hadi 29 Oktoba 2023 na Awamu ya Pili itaadhimishwa Mwezi Oktoba 2024. Lengo ni kuendelea kufanya mang’amuzi ya kina kuhusu dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, chombo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa watu wa Mungu katika ujumla wao kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili. Ijumaa tarehe 7 Julai 2023 Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu imechapisha orodha ya majina 363 ya wajumbe wa Sinodi ya ya XVI ya Maaskofu, kati yao kuna wanawake 54 wenye haki ya kupiga kura. Wajumbe kutoka katika Makanisa ya Mashariki ni 20, Kanisa Barani Afrika ni 43, Amerika ni 47, Barani Asia ni 25, Ulaya 48, Oceania 5. Maaskofu wasiokuwa na Baraza la Maaskofu ni mmoja ambaye ameteuliwa. Katika Orodha hii, kuna Marais wa Mashirikisho ya Mabaraza ya Maaskofu Ulimwenguni, kama vile SECAM, hawa ni 5. Kuna wakuu wa Mabaraza ya Kipapa “Curia Romana” 20. Katika Orodha hii, kuna wajumbe 50 wameteuliwa moja kwa moja na Baba Mtakatifu Francisko; wajumbe kutoka katika Baraza la Kawaida ni 16. Kuna watu 8 ambao wamepewa mialiko maalum na wajumbe wengine wanaoshiriki ni 75, wataalamu na wawezeshaji ni 75. Kumbe, idadi ya wanawake katika maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu jumla ni 54.

Orodha ya washiriki wa Sinodi kutoka Afrika Mashariki na Kati
Orodha ya washiriki wa Sinodi kutoka Afrika Mashariki na Kati

Orodha ya Majina ya Washiriki wa Sinodi kutoka Afrika Mashariki na Kati ni kama ifuatavyo: Askofu Georges Bizimana kutoka Jimbo Katoliki la Ngozi, Burundi; Askofu mkuu Martin Kivuva Musonde wa Jimbo kuu la Mombasa na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, Askofu mkuu Anthony Muheria wa Jimbo kuu la Nyeri, Kenya; Askofu mkuu George Desmond Tambala, O.C.D, kutoka Jimbo kuu la Lilongwe, Malawi; Askofu Edouard Sinayobye wa Jimbo  Katoliki Kyangungu, Rwanda; Askofu mkuu Stephen Ameyu Martin Mulla wa Jimbo kuu la Juba, kutoka Sudan ya Kusini. Kutoka Tanzania ni Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi wa Jimbo kuu la Dar Es Salaam pamoja na Askofu Flavian Matindi Kassala wa Jimbo Katoliki la Geita ambaye pia ni Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC. Kutoka Uganda, ameteuliwa Askofu Sanctus Lino Wanok wa Jimbo Katoliki la Lira na hatimaye ni Zambia ambayo itawakilishwa na Askofu mkuu Ignatius Chama, wa Jimbo kuu la Kasama. Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, linawakilishwa na Kardinali Fridolin Ambongo Besungu, O.F.M. Cap., Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Kinshasa, DRC.; Wengine ni Mheshimiwa sana Padre Gebresilasie Tadese Tesfaye, M.C.C. J Mkuu wa la Wamisionari wa Comboni wa Moyo Mtakatifu wa Yesu; Askofu Lucio Andrice Muandula wa Jimbo la Xai Xai, Msumbiji, Rais mwakilishi. Wakati huo huo Padre Anthony Makunde, Katibu mkuu wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati AMECEA, anashiriki katika Sinodi kama mtaalam na mwezeshaji katika maadhimisho ya Sinodi.

Papa Francisko anatarajiwa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Sinodi
Papa Francisko anatarajiwa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Sinodi

Ni katika muktadha huu, Jumanne tarehe 20 Juni 2023 Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu imechapisha Hati ya Kutendea Kazi “Instrumentum laboris” kwa Maadhimisho ya Awamu ya Kwanza ya Sinodi kuanzia tarehe 4 hadi 29 Oktoba 2023. Hati hii inagusia kuhusu: Kanisa la Kisinodi Uzoefu Muhimu: Sifa za Kanisa la Kisinodi; Mwelekeo wa Maadhimisho ya Kanisa la Kisinodi: Majadiliano na Roho Mtakatifu. Sehemu ya Pili ni: Umoja, Ushiriki na Utume: Vipaumbele vitatu vya Kanisa la Kisinodi. Huu ni umoja unaong’ara, alama na chombo cha ushirika na Mwenyezi Mungu na alama ya umoja kati ya binadamu. Uwajibikaji katika utume na jinsi ya kushirikishana karama katika huduma ya Injili. Ushiriki, utawala na madaraja: Je ni mchakato, miundombinu na taasisi gani zinapaswa kushiriki katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi? Hati ya Kutendea Kazi: Instrumentum laboris ni matunda ya ushiriki mkamilifu wa watu wa Mungu kutoka katika: Majimbo, Mabaraza ya Maaskofu na katika maadhimisho ngazi ya Kimabara, sanjari na maadhimisho yaliyokuwa yakiendeshwa kwa njia ya mitandao ya kijamii na hivyo kubainisha vipaumbele vya Makanisa mahalia vinavyopaswa kufanyiwa kazi kuanzia tarehe 4 – 29 Oktoba 2023. Lengo kuu ni kutekeleza utume wa Mama Kanisa wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Huu ni muda wa kusikiliza kwa makini jinsi ambavyo limeishi na kutekeleza dhamana na utume wake; matatizo na changamoto zinazojitokeza. Changamoto kubwa katika maadhimisho ya Sinodi ni uwezo wa kuratibu kinzani ili ziweze kuwa ni chemchemi ya nguvu mpya ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Huu ni wakati ambapo utambulisho na wito wa Kanisa unajikita katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi pamoja na kuhakikisha kwamba, matunda yaliyojitokeza yanamwilishwa katika uhalisia wa maisha ya Jumuiya za waamini sehemu mbalimbali za dunia.

Oorodha Sinodi 2023
08 July 2023, 16:03