Tafuta

Kumbukumbu ya Miaka 60 tangu Mtakatifu Yohane XXII achapishe Waraka wa Kichungaji wa “Pacem in terris." Kumbukumbu ya Miaka 60 tangu Mtakatifu Yohane XXII achapishe Waraka wa Kichungaji wa “Pacem in terris."  (AFP or licensors)

Mahojiano Kati ya Kardinali Parolin na Kituo cha Televishen cha Televisheni-RAI-TG1

Kardinali Pietro Parolin katika mahojiano maalum na RAI-TG1 amegusia kuhusu: Umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika ujenzi wa matumaini na umoja miongoni mwa watu wa Mataifa; ziara ya Kardinali Matteo Maria Zuppi nchini Ukraine na Urusi, Kumbukumbu ya Miaka 60 tangu Mtakatifu Yohane XXII achapishe Waraka wa Kichungaji wa “Pacem in terris”, pamoja na kumbukizi ya Miaka 75 ya Tamko la Haki Msingi za Binadamu; Injili ya uhai dhidi ya kifo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Kituo cha Televisheni chaTaofa la Italia, RAI: TG1 amegusia kuhusu: Umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika ujenzi wa matumaini na umoja miongoni mwa watu wa Mataifa; ziara ya Kardinali Matteo Maria Zuppi nchini Ukraine na Urusi, Kumbukumbu ya Miaka 60 tangu Mtakatifu Yohane XXII achapishe Waraka wa Kitume wa “Pacem in terris”, pamoja na kumbukizi ya Miaka 75 ya Tamko la Haki Msingi za Binadamu. Tamko la Haki Msingi za Binadamu, lililotiwa mkwaju na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 10 Desemba 1948, miaka sabini na tano iliyopita ni changamoto endelevu kwa Jumuiya ya Kimataifa kwa wakati huu. Kipaumbele cha kwanza kinapaswa kuwa ni utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; uhai unaopaswa kulindwa na kuendelezwa, sanjari na kujikita katika mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu: kiroho na kimwili. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuheshimu haki msingi za binadamu dhidi ya kile kinachodaiwa kuwa ni “Haki Mpya” ambazo kimsingi zinasigana na tamaduni, mila na desturi za mataifa mengi. Hiki ni kielelezo cha ukoloni wa kiitikadi. Uhuru wa kweli hauna budi kudumishwa dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba na kifo laini; biashara haramu ya binadamu na viungo vyake sanjari na utumwa mamboleo; mambo yanayokwenda kinyume cha Injili ya uhai. Kumbe, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuhakikisha kwamba, watu wengi zaidi wanapata huduma bora ya afya na dawa muhimu katika mapambano dhidi ya magonjwa duniani. Ili kudumisha uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, kuna haja pia ya kujikita katika ujenzi wa amani kama chachu ya maendeleo endelevu ya binadamu.

Utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za nyuklia ni hatari
Utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za nyuklia ni hatari

Utengenezaji, ulimbikizaji, usambazaji, uuzaji na matumizi ya silaha za atomiki kwa ajili ya vita ni kinyume cha maadili na utu wema. Mkataba wa Kimataifa wa Kupinga Matumizi ya Silaha za Nyuklia, TPNW unalenga kujenga mazingira ya usalama, amani na utulivu bila ya kuwa na hofu ya mashambulizi ya silaha za maangamizi. Amani ya kweli inajengwa kwa njia ya majadiliano na mshikamano! Kuna hatari kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa kumegeka na kutumbukia katika vita na ubaridi wa moyo. Ujenzi wa matumaini mapya ndicho kilichokuwa kilio baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia na matokeo yake ni Tamko la Helsinki kuhusu Haki Msingi za Binadamu sanjari na ujenzi wa mshikamano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kanisa Katoliki kwa upande wake, litaendelea kuhimiza umuhimu wa watu wa Mataifa kudumisha amani. Kanisa linaunga mkono Kanuni ya Sheria ya Kimataifa kuhusu Silaha za Nyuklia, ikiwa ni pamoja na Mkataba wa Kimataifa wa kupiga rufuku utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za kinyuklia duniani. Amani ni kazi ya haki na matunda ya upendo! Amani inatishiwa sana na mashindano ya silaha; utengenezaji na biashara ya silaha pamoja na mchakato wa ulimbikizaji wa silaha duniani! Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha amani ambalo ni jina jipya la maendeleo fungamani ya binadamu!

Silaha za nyuklia zinatishia usalama wa Kimataifa
Silaha za nyuklia zinatishia usalama wa Kimataifa

Baba Mtakatifu anasema, dunia bila kuwa na silaha za kinyuklia inawezekana kabisa na ni muhimu sana na kwamba, silaha hizi za maangamizi kamwe haziwezi kuwasaidia viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuwa na uhakika wa usalama wa raia na mali zao kitaifa na kimataifa. Kuna haja ya kufanya upembuzi yakinifu kuhusu madhara yake katika maisha ya watu sanjari na mazingira; kwa kuondoa hofu, mazingira ya kutoaminiana, chuki na uhasama vinavyozungumza “dhana ya silaha za nyuklia.” Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujielekeza zaidi katika kubuni sera na mikakati itakayosaidia utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030. Kuhusu ziara ya Kardinali Matteo Maria Zuppi, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia nchini Ukraine na Urusi kwa niaba ya Baba Mtakatifu ilipania pamoja na mambo mengine: kuhusu hali ya mateka na wafungwa wa kijeshi; urejeshwaji wa watoto waliochukuliwa nchini Ukraine na kupelekwa nchini Urusi anasema kwa sasa Vatican inatafuta mbinu za utekelezaji wa ziara hii ya Kardinali Matteo Maria Zuppi kwa vitendo pengine hata kwa msaada wa Mashirika ya Kimataifa. Mtakatifu Yohane XXIII tarehe 11 Aprili 1963 alichapisha Waraka wake wa Kitume “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” kumbe Mama Kanisa anafanya kumbukizi ya Miaka 60 tangu kuchapishwa kwake. Mtakatifu Yohane XXIII anasema, amani inasimikwa katika misingi ya ukweli, haki, upendo na uhuru kamili. Kila mwanadamu ni nafsi yenye haki na wajibu. Hii ni haki ya kuishi na kuwa na maisha na haki za tunu za kimaadili na kiutamaduni. Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, mashindano ya utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha, zikiwemo silaha za nyuklia yanaendelea kukomba rasilimali za dunia ambazo zingeweza kutumika vyema zaidi kwa ajili ya kunogesha mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote!

Vita kati ya Palestina na Israeli ni matumizi mabaya ya rasilimali.
Vita kati ya Palestina na Israeli ni matumizi mabaya ya rasilimali.

Kunahitajika mkakati wa Kimataifa ili kusitisha hatari inayoweza kusababishwa na mashindano ya silaha kwani madhara yake ni makubwa kama inavyojionesha huko nchini Ukraine. Kuna Vita Kuu ya Tatu ya Dunia inayopiganwa sehemu mbalimbali za dunia na madhara yake ni makubwa kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha na kuchechemea kwa hali ya maisha; kukosekana kwa uhakika na usalama wa chakula duniani hasa Barani Afrika na Mashariki ya Kati. Vita imeendelea kuwatumbukiza watu wengi katika umaskini wa hali na kipato kama inavyojionesha nchini Siria. Kardinali Parolin anakazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kuheshimu sheria za Kimataifa; kwa kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi. Wakuu wa Kanisa Katoliki daima wameendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Umoja wa Mataifa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Umoja wa Mataifa ni familia kubwa ya Mungu ambapo nchi wanachama zinaheshimiwa na kwamba, Umoja wa Mataifa unapaswa kujengewa uwezo wa kuingilia kati machafuko, vita na kinzani. Ni katika muktadha huu, Umoja wa Mataifa unapaswa kufanyia marekebisho makubwa, ili kuweza kurejea katika asili yake, jambo ambalo si lelemama! Baba Mtakatifu Francisko anasema, sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi na usalama wa maisha! Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni changamoto pevu anasema Kardinali Pietro Parolin, lakini inaweza kupatiwa ufumbuzi kwa kujikita katika mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaosimamiwa na kanuni auni. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujizatiti kikamilifu katika kulinda utu, heshima na haki msingi za binadamu tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mapenzi ya Mungu. Kimsingi, Kanisa linahimiza huduma kwa binadamu kwa kuzingatia kanuni msingi za Kiinjili. Pili tunu msingi za maisha ya ndoa na familia zinapaswa kulindwa na kudumishwa na wote.  

Kardinali Parolin Mahojiano
07 July 2023, 15:20