Tafuta

Shirikisho la Mashirika ya Misaada kwa Makanisa ya Mashariki, ROACO kuanzia tarehe 19 - 22 Juni 2023 limekuwa likiadhimisha Mkutano wake wa 96. Shirikisho la Mashirika ya Misaada kwa Makanisa ya Mashariki, ROACO kuanzia tarehe 19 - 22 Juni 2023 limekuwa likiadhimisha Mkutano wake wa 96.  (AFP or licensors)

Mkutano Mkuu wa 96 wa ROACO 19-22 Juni 2023: Amani, Diplomasia na Vijana

Hiki ni kipindi cha kusali na kuwaombea wafadhili wa ROACO ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuchangia huduma mbalimbali za huruma na upendo zinazotolewa na ROACO kwa Makanisa ya Mashariki. Ni nafasi pia kwa ajili ya kuendelea kumlilia Mwenyezi Mungu ili aweze kuingilia kati na kuwakirimia waja wake amani, utulivu wa kisiasa, kijamii na kidini; mambo ambayo pia yamechangiwa kwa kiasi kikubwa kwa kuenea kwa athari za Ugonjwa wa UVIKO-19.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Mashirika ya Misaada kwa Makanisa ya Mashariki, ROACO, (R.O.A.C.O. Riunione Opere Aiuto Chiese Orientali), kuanzia tarehe 19 - 22 Juni 2023 limekuwa likiadhimisha Mkutano wake wa 96. Hiki ni kipindi cha kusali na kuwaombea wafadhili wa ROACO ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuchangia huduma mbalimbali za huruma na upendo zinazotolewa na ROACO kwa Makanisa ya Mashariki. Ni nafasi pia kwa ajili ya kuendelea kumlilia Mwenyezi Mungu ili aweze kuingilia kati na kuwakirimia waja wake amani, utulivu wa kisiasa, kijamii na kidini; mambo ambayo pia yamechangiwa kwa kiasi kikubwa kwa kuenea kwa athari za Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Mkutano huu wa 96 umefunguliwa kwa ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu mkuu Claudio Gugerotti, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa Ajili ya Makanisa ya Mashariki. Nia ya Ibada hii ya Misa imekuwa ni kwa ajili ya kuombea amani huko Mashariki ya Kati.

Shirikisho la Mashirika ya Misaada kwa Makanisa ya Mashariki, ROACO
Shirikisho la Mashirika ya Misaada kwa Makanisa ya Mashariki, ROACO

Wajumbe wa ROACO pamoja na mambo mengine, wamekuwa wakijadili kwa kina na mapana madhara ya vita, kinzani na machafuko ya kidini na kisiasa huko Mashariki. kwa kuwasikiliza viongozi wakuu wa Makanisa mjini Yerusalemu. Wajumbe wamepata fursa ya kujadili kuhusu Sadaka na Mchango wa Ijumaa kuu kwa ajili ya Nchi Takatifu: "Pro Terra Sancta" kwa Mwaka 2023 pamoja na hali ya Makanisa mahalia ambayo yako chini ya Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican amewashirikisha wajumbe wa ROACO kuhusu mpango mkakati wa diplomasia ya Vatican kuhusu: Vita kati ya Ukraine na Urusi; Hali tete huko Mashariki ya Kati pamoja na machafuko ya kisiasa nchini Ethiopia. Mabalozi wa Vatican nchini Uturuki na Iran wamewashirikisha wajumbe wa ROACO hali halisi ya huko wanakotoka pamoja na hali ya kisiasa, kijamii na kidini ilivyo nchini Eritrea, taarifa iliyotolewa na Askofu mkuu Menghesteab Tesfamariam, M.C.C.I wa Jimbo kuu la Asmara.

ROACO imesikiliza taarifa kutoka Eritrea
ROACO imesikiliza taarifa kutoka Eritrea

Jumatano tarehe 21 Juni 2023 ni siku ambayo ROACO imetenga kwa ajili ya kuwasikiliza vijana wa kizazi kipya kutoka katika nchi 13 za Makanisa ya Mashariki ambazo ziko chini ya uongozi na usimamizi wa Baraza la Kipapa kwa Ajili ya Makanisa ya Mashariki. Vijana hawa wamekuwepo mjini Roma kuanzia tarehe 16 na wataendelea kuwepo hadi tarehe 23 Juni 2023 ili kujadili tema inayohusu “Kanisa Likishirikiana Safari na Vijana wa Kizazi Kipya: Vijana Watendaji Wakuu wa Mafao ya Wengi.” Hii imekuwa ni fursa kwa vijana wa kizazi kipya kufahamiana, kusali kwa pamoja, kutafakari pamoja na kutembelea mji wa Roma ambao umesheheni amana na utajiri mkubwa wa Kanisa na hatimaye, kushirikishana na wajumbe wa ROACO jinsi ya kusongesha mbele ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, vijana wakiwa ni wadau katika mchakato huu.

ROACO 96
21 June 2023, 14:38