Tafuta

Kardinali Michael Czerny Jubilei ya Miaka 50 ya Maisha na Utume wa Kipadre na kitawa ndani ya Shirika la Wayesuit na Kanisa katika ujumla wake. Kardinali Michael Czerny Jubilei ya Miaka 50 ya Maisha na Utume wa Kipadre na kitawa ndani ya Shirika la Wayesuit na Kanisa katika ujumla wake.  (ANSA)

Kardinali Michael Czerny Jubilei ya Miaka 50 ya Maisha na Utume wa Kipadre

Kardinali Michael Czerny, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu, tarehe 15 Juni 2023 amemwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya Maisha na Utume wa Kipadre ndani ya Shirika la Wayesuit na Kanisa katika ujumla wake. Katika kipindi hiki cha miaka 50 amepata, fursa na kupitia changamoto nyingi, lakini Mungu amemwiimarisha katika: imani, matumaini na mapendo

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Jubilei ni kipindi cha kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Ni wakati muafaka wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka anazowakirimia waja wake hata bila mastahili yao. Ni muda wa kufanya toba na kuomba msamaha kwa mapungufu yote yaliyojitokeza katika maisha na utume, tayari kuomba tena neema na baraka ya kusonga mbele kwa imani na matumaini zaidi. Ni katika muktadha huu, Kardinali Michael Czerny, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu, tarehe 15 Juni 2023 amemwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya Maisha na Utume wa Kipadre ndani ya Shirika la Wayesuit na Kanisa katika ujumla wake. Katika kipindi cha miaka 50 ya maisha na utume wake kama Padre na Mtawa amepata fursa na kukumbana na changamoto mbalimbali, lakini kwa huruma, nguvu na msaada wa Mwenyezi Mungu hadi leo hii bado amesimama na anaendelea kumtumikia kwa ari, moyo na nguvu mpya. Mwenyezi Mungu amemwimarisha katika imani, matumaini na mapendo thabiti.

Kardinali Michael Czerny wakati wa kusimikwa kwake kama Kardinali
Kardinali Michael Czerny wakati wa kusimikwa kwake kama Kardinali

Injili kama ilivyoandikwa na Marko imekuwa ni sehemu ya rejea katika maisha na utume wake kama Padre kwa jinsi ile Kristo Yesu alivyowaita aliowataka mwenyewe wakamwendea, kielelezo cha ufunuo wa siri kubwa ya wito wa Mungu katika maisha ya mwanadamu mintarafu kazi ya ukombozi. Mitume kumi na wawili walitofautiana sana katika maisha yao mpaka akina Yuda Iskarioti, ili kuwaonjesha huruma na upendo wake usiokuwa na kifani. Kardinali Michael Czerny, katika maisha na utume wake, daima alifarijika kwa maneno ya Kristo Yesu anayesema “Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni. Haya nawaamuru ninyi, mpate kupendana.” Yn 15:16-17. Mitume kumi na wawili wanayo dhamana na nafasi ya pekee katika maisha na utume wa Kristo Yesu, katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Hiki ni kielelezo cha Agano kati ya Mwenyezi Mungu na watu wake, ili kuwakirimia wokovu. Kristo Yesu aliamua kuunda Kundi la Mitume kumi na wawili, ili waweze kuwa ni msingi wa Agano Jipya na la milele na mwanzo wa Kanisa linalopata utimilifu wake kwa ujio wa Roho Mtakatifu siku ile ya Pentekoste ya kwanza!

Kanisa halina budi kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi.
Kanisa halina budi kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi.

Kumbe, kila wito ni tendo la uumbaji ambalo kwalo Mwenyezi Mungu anaumba upya sura ya nchi, na hivyo kuwasha moto wa imani unaosimikwa katika “Ndiyo” ya mhusika, kuonesha utayari wake wa kushiriki katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, huku akitambua kwamba, amejengwa juu ya msingi wa Mitume na Manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni. Rej. Ef 2:20. Huu ni mwaliko wa kujitaabisha kumfahamu, kumpenda na kumtumikia Kristo Yesu; tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; huku wakisimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hii ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo, ili watu wawe na uzima, kisha wawe nao tele, kwani imani na haki ni sawa na chanda na pete, vinakumbatiana na kukamilishana. Kama wafuasi wa Kristo Yesu, wabatizwa wote wanaitwa kukaa na Kristo, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Huu ndio utume ambao Kristo Yesu alipenda kuwakabidhi Mitume wake baada ya mateso, kifo na ufufuko wake. Imani ya Kikristo imejengwa juu ya msingi wa Mitume na inaendelea kutangazwa na kushuhudiwa sehemu mbalimbali za dunia, changamoto na mwaliko kwa waamini kuwa ni mashuhuda waaminifu wa Injili na walinzi waaminifu wa Mapokeo ya Kanisa.

Jubilei ya Miaka 50 ya Upadre
15 June 2023, 16:06