Tafuta

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Dominika tarehe 18 Juni 2023 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Jimbo la Koper. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Dominika tarehe 18 Juni 2023 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Jimbo la Koper. 

Kardinali Pietro Parolin: Huruma ni Chemchemi ya Furaha, Utulivu na Amani ya Ndani

Katika mahubiri yake amekazia ushirika unaobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo; Huruma na upendo wa Kristo kwa waja wake, Uinjilishaji unasimikwa katika matendo ya huruma yaliyowasukuma wamisionari wengi kutoka Slovenia kwenda kuinjilisha na kwamba, Baba Mtakatifu Francisko analihamasisha Kanisa kujizatiti katika mchakato wa uinjilishaji unaofumbatwa katika ushuhuda makini. unaobubujika katika huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kati ya tarehe 17 na 18 Juni 2023, Jimbo la Koper limekuwa ni mwenyeji wa matukio muhimu sana katika Kanisa Katoliki nchini Slovenia kwa mwaka 2023. Kimsingi Slovenia imekuwa ni mwenyeji wa Jukwaa la Majadiliano na Amani huko Bulkan, tukio ambalo limehudhuriwa na wawakilishi wa ngazi za juu wa dini zote kuu duniani yaani: Ukristo, Uislam na Uyahudi. Jukwaa hili limehudhuriwa na wawakilishi kutoka katika nchi 15 za Balkan na kutoka katika Rasi ya Asia Ndogo. Majadiliano haya yananogeshwa na kauli mbiu: “Amani kwako, Ulaya! Amani iwe kwenu, watu wa Balkan!” Huu ni mwitikio wa Kanisa mahalia la Slovenia linaloendelea kujikita katika majadiliano ya kidini yanayohimiza wadau mbalimbali kujikita katika ujenzi wa misingi ya amani duniani. Slovenia ina utajiri na urithi mkubwa wa tunu msingi za maisha ya Kikristo. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Dominika tarehe 18 Juni 2023 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Jimbo la Koper. Katika mahubiri yake amekazia ushirika unaobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo; Huruma na upendo wa Kristo kwa waja wake, Uinjilishaji unasimikwa katika matendo ya huruma yaliyowasukuma wamisionari wengi kutoka Slovenia kwenda kuinjilisha na kwamba, Baba Mtakatifu Francisko analihamasisha Kanisa kujizatiti katika mchakato wa uinjilishaji unaofumbatwa katika ushuhuda makini.

Uinjilishaji unaosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko
Uinjilishaji unaosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko

Kardinali Pietro Parolin katika mahubiri yake amewataka watu wa Mungu nchini Slovenia kujikita katika ushirika na utakatifu unaopata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo, tayari kumwilisha ushirika huu unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kristo Yesu ni Uso wa huruma ya Baba wa milele. Huruma ni chemchemi ya furaha, utulivu na amani ya ndani. Hili ni sharti la wokovu wa binadamu. Huruma ni tendo la juu na kuu kabisa ambalo kwa njia yake Mwenyezi Mungu anamwendea mwanadamu. Huruma ni njia inayowaunganisha Mungu na binadamu, na kuufungulia moyo mlango wa matumaini ya kupendwa daima, licha ya hali ya dhambi inayomwandama mwanadamu. Huruma ndiyo msingi thabiti wa uhai wa Kanisa. Kazi zake zote za kichungaji zinapaswa kufungamanishwa katika upole linalouonesha kwa waamini; hakuna chochote katika mahubiri na ushuhuda wake kwa ulimwengu kinachoweza kukosa huruma. Umahiri wa Kanisa unaonekana kwa namna linavyoonyesha huruma na upendo. Rej. Misericordiae vultus, Uso wa huruma namba 10.

Ushuhuda wa imani ni nyenzo msingi katika uinjilishaji
Ushuhuda wa imani ni nyenzo msingi katika uinjilishaji

Dhamana, wito na utume wa uinjilishaji unawaambata Wakristo wote kama ilivyokuwa kwa Askofu Frederick Baraga na wamisionari wenzake, waliosimama kidete kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu nchini Slovenia. Akathubutu kuwa ni Muasisi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Slovenia. Waamini wanatumwa Kuinjilisha na kuinjilishwa, ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Huu ni ushuhuda wa upendo wa Kristo Yesu unaoganga na kuokoa; kumbe, kila mwamini anaitwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu ni kiini cha mtume mmisionari, ambaye anatambua kwamba, ameitwa, akapewa madaraka na hatimaye kutumwa na Kristo Yesu kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! Kumbe, Kristo Yesu ni kiini cha mitume wamisionari ambao wanapaswa kumtangaza na kumshuhudia Kristo kwani wao ni wajumbe wake! Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, amehitimisha mahubiri yake kwa kuwatia shime watu wa Mungu nchini Slovenia wasife moyo wala kukata tamaa kutokana na changamoto wanazopitia katika maisha, bali wamtazame Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu; waendelee kujizatiti katika maisha ya sala, watubu na kumwongokea Mungu na hivyo kuendelea kujibidiisha kujenga ushirika na Fumbo la Utatu Mtakatifu, nguvu thabiti katika mchakato wa uinjilishaji.

slovenia
19 June 2023, 14:49