Tafuta

Majadiliano haya yananogeshwa na kauli mbiu: “Amani kwako, Ulaya! Amani iwe kwenu, watu wa Balkan!” Majadiliano haya yananogeshwa na kauli mbiu: “Amani kwako, Ulaya! Amani iwe kwenu, watu wa Balkan!”  

Jukwaa la Majadiliano ya Amani Huko Balkan: Heri Wapatanishi

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika hotuba yake amekazia kuhusu Heri za Mlimani, Msimamo wa Vatican kwenye vita ya Balkan; Majadiliano ya kidini ni nyenzo muhimu katika ujenzi wa amani duniani na kwamba, kesho la Bara la Ulaya inasimikwa katika njia ya udugu wa kibinadamu. Majadiliano ya kidini ni nyenzo muhimu katika mchakato wa ujenzi wa msingi wa haki, amani na maridhiano duniani na haswa miongoni mwa Wakristo, Waislam na Wayahudi

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kati ya tarehe 17 na 18 Juni 2023, Koper imekuwa ni mwenyeji wa matukio muhimu sana katika Kanisa Katoliki nchini Slovenia kwa mwaka 2023. Kimsingi Slovenia imekuwa ni mwenyeji wa Jukwaa la Majadiliano na Amani huko Bulkan na kuhudhuriwa na wawakilishi wa ngazi za juu wa dini zote kuu duniani yaani: Ukristo, Uislam na Uyahudi. Jukwaa hili linahudhuriwa na wawakilishi kutoka katika nchi 15 za Balkan na kutoka katika Rasi ya Asia Ndogo. Majadiliano haya yananogeshwa na kauli mbiu: “Amani kwako, Ulaya! Amani iwe kwenu, watu wa Balkan!” Huu ni mwitikio wa Kanisa mahalia la Slovenia linaloendelea kujikita katika majadiliano ya kidini yanayohimiza wadau mbalimbali kujikita katika ujenzi wa misingi ya amani duniani. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika hotuba yake amekazia kuhusu Heri za Mlimani, Msimamo wa Vatican kwenye vita ya Balkan; Majadiliano ya kidini ni nyenzo muhimu katika ujenzi wa amani duniani na kwamba, kesho la Bara la Ulaya inasimikwa katika njia ya udugu wa kibinadamu. Ukanda wa Balkan umeendelea kuwa aminifu kwa wito na mwingiliano wa watu, tamaduni na historia yao, kiasi kwamba, Ukanda huu umeendelea kuwa ni mfano bora wa kuigwa kwa watu kutoka katika makabila, tamaduni na dini mbalimbali kuweza kuishi kwa amani na maridhiano. “Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu.” Mt.5:9.

Jukwaa la majadiliano ya kidini huko Balkan
Jukwaa la majadiliano ya kidini huko Balkan

Vatican katika maisha na utume wake, imeendelea kujipambanua katika kutafuta suluhu ya amani katika migogoro mbalimbali ya Kimataifa bila ya kufungwa na masilahi ya kisiasa, kiuchumi na kijeshi, ili hatimaye kusaidia kunogesha mchakato wa haki, amani na upatanisho. Vatican katika Ukanda wa Balkan imeendelea kuwa aminifu kwa maisha na utume wa Kanisa. Vatican ikashuhudia katika kipindi cha miaka ya 1990 machafuko ya kisiasa na tabia ya Mataifa kutaka kujitenga, kama ilivyooneshwa na Croatia pamoja na Slovenia. Vatican ikapaaza sauti kulinda na kutetea haki msingi za wananchi husika; ikakazia majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kukuza na kudumisha maridhiano kati ya watu wa Mungu nchini Yugoslavia. Tarehe 25 Juni 1991 Slovenia ikagawanyika, Croatia ikatambulika Kimataifa na uhuru wa Solovenia ukawa mashakani. Vatican ikatambua uwepo wa nchi zote mbili. Mtakatifu Yohane Paulo II aliwataka waamini wa Kanisa Katoliki, Waorthodox na Waislam kushirikiana na kushikamana pamoja kwa ajili ya ustawi , maendeleo na mafao ya wengi na hivyo kuendelea kujikita katika majadiliano ya ukweli na uwazi. Hata leo hii, Ukanda wa Balkan unapaswa kuendelea kujikita katika ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana, ili kujadiliana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Majadiliano ya kidini ni muhimu katika kudumisha amani duniani.
Majadiliano ya kidini ni muhimu katika kudumisha amani duniani.

Kardinali Pietro Parolin anakaza kusema, majadiliano ya kidini ni nyenzo muhimu katika ujenzi wa amani duniani. Majadiliano ni muhimu sana katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya mawasiliano ya kijamii; ukuaji na udumishaji wa amani katika Ukanda wa Balkan. Majadiliano ya kidini ni muhimu sana kwa waamini wa Kanisa Katoliki, Kanisa la Kiorthodox na Kiislam ili kukuza na kudumisha misingi ya amani. Majadiliano ya kidini ni wajibu na dhamana ya wananchi wote. Hii inatokana na ukweli kwamba, majadiliano ni njia inayojenga na kudumisha udugu wa kibinadamu, amani duniani na ushirika kati ya watu wa Mungu. Leo na kesho ya Bara la Ulaya inasimikwa katika njia ya udugu wa kibinadamu mintarafu fursa iliyotolewa na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya katika kukoleza mageuzi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na demokrasia ya kweli Barani Ulaya. Vatican inaunga mkono na kutumaini kwamba, Umoja wa Ulaya utazisaidia nchi za Balkan kuendelea kukua na kushamiri katika medani mbalimbali za maisha kwa kuzingatia umoja na utofauti wa nchi hizi, kama sehemu ya haki zao msingi. Njia ya udugu wa kibinadamu iliweka msingi wa amani kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Vatican itaendelea kuwa karibu na watu wa Mungu katika nchi za Balkan na kwamba, majadiliano katika ukweli na uwazi, yatasaidia ujenzi na miundo mbinu ya kudumisha amani.

Jukwaa la amani

 

 

17 June 2023, 16:07