Askofu Mkuu Protase Rugambwa Mapokezi Jimbo Kuu la Tabora 25 Juni 2023, Aagwa Kigoma!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Askofu mkuu Protase Rugambwa, Askofu mkuu mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo kuu la Tabora, Tanzania, Ijumaa tarehe 23 Juni 2023 ameagwa rasmi na watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Kigoma. Jumamosi tarehe 24 Juni 2023 watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Kigoma wanamsindikiza kuelekea Jimbo kuu la Tabora ambako atapokelewa rasmi Usinge mpakani mwa Tabora na Kigoma na jioni anatarajia kushiriki katika Masifu ya Jioni na Dominika tarehe 25 Juni 2023 maadhimisho ya Ibada ya Misa takatifu yanayofanyika kwenye Kituo cha hija cha Ifucha nghoro kilichoko Jimbo Kuu Katoliki Tabora. Katika makala haya, Askofu mkuu Protase Rugambwa, Askofu mkuu mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo kuu la Tabora, anaelezea hisia zake tangu alipopashwa habari juu ya nia ya Baba Mtakatifu Benedikto XVI kumteuwa kushiriki katika huduma za kichungaji kwa Kanisa la Kiulimwengu hapo tarehe 7 Juni 2012 wakati Maaskofu walipokuwa Jimboni Iringa, tarehe 26 Juni 2012 alipotangazwa rasmi. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC., kuanzia Dominika 14 Mei hadi tarehe 21 Mei 2023 limefanya Hija ya Kitume “Ad Limina Apostolorum Visitatio,” kwa kifupi, “Ad Limina” inayofanyika kila baada ya miaka mitano na hiyo imekuwa ni fursa ya kuungana na watanzania wanaoishi Italia kumwaga Askofu mkuu Protase Rugambwa, tayari kumpokea anapoanza utume wake kama Askofu mkuu mwandamizi wa Jimbo kuu la Tabora. Askofu mkuu Protase Rugambwa alitumia fursa hii kuwashuruku Maaskofu, Watanzania wanaoishi Italia na kwa namna ya pekee Mapadre wanafunzi kutoka “Colleggio San Pietro” alioshiriki nao katika maisha. Jambo la msingi aliwaomba watanzania ni kumsindikiza katika sala anapoanza utume wake Jimbo kuu la Tabora.
Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko tarehe 13 Aprili 2023 alimteuwa Askofu mkuu Protase Rugambwa kuwa Askofu mkuu mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo kuu la Tabora, Tanzania. Itakumbukwa kwamba, Askofu Mkuu Rugambwa alizaliwa tarehe 31 Mei 1960 huko Bunena-Bukoba nchini Tanzania, akapata Daraja Takatifu ya Upadri kutoka mikononi mwa Mtakatifu Yohane wa Pili alipotembelea Tanzania tarehe 2 Septemba 1990 na kuwa Padri wa Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara. Kuanzia mwaka 2002 hadi mwaka 2008 alifanya utume wake kwenye Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu mjini Vatican. Baba Mtakatifu Benedikto XVI, tarehe 18 Januari 2008 akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Kigoma, na tarehe 26 Juni 2012 akateuliwa kuwa Katibu Mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu na Rais wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari na wakati huo huo kumpandisha hadhi na kuwa ni Askofu mkuu. Tarehe 9 Novemba 2017 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu. Baada ya kulitumikia Baraza kwa vipindi viwili na muda wake ulipogota ukomo, kadiri ya Katiba mpya ya Kitume inayojulikana kama “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu” tarehe 13 Aprili 2023, Baba Mtakatifu amemteuwa Askofu Mkuu Protase Rugambwa kuwa Askofu mkuu wenye haki ya kurithi Jimbo kuu la Tabora, Tanzania.
Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu Flavian Matindi Kassala wa Jimbo Katoliki la Geita ambaye pia ni Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, baada ya uteuzi huu anasema, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linapenda kumkaribisha Askofu mkuu Protase Rugambwa miongoni mwao kwa mikono miwili! Hili ni Jembe la uhakika! Katika kipindi cha utume wake kwenye Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu amejipatia uzoefu, mang’amuzi na utajiri mkubwa ambao sasa anakuja kuufanyia kazi kwa watu wa Mungu nchini Tanzania. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania lina matumaini makubwa kwa Askofu mkuu Protase Rugambwa katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda sanjari na ujenzi wa Kanisa la Kisinodi linalosimikwa katika: Umoja, Ushiriki na Utume wa Kanisa. Askofu mkuu Rugambwa kwa sasa ni “Jembe machachari” ambalo limenolewa tayari kukabiliana na changamoto mamboleo katika mchakato wa uinjilishaji unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Askofu mkuu Rugambwa atakuwa ni msaada mkubwa kwa Askofu mkuu Paulo Runangaza Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora, wanayefahamiana kwa miaka mingi katika huduma kwa watu wa Mungu Jimbo kuu la Tabora, kwani Askofu mkuu Protase Rugambwa alikuwa ni mrithi wake Jimbo Katoliki la Kigoma, na sasa amemrithi pia Jimbo kuu la Tabora, matendo makuu ya Mungu, si bure! Jumuiya ya watanzania wanaoishi na kufanya shughuli zao hapa Italia, watakosa sana uwepo wake, kwani kwao alikuwa ni Baba, Kaka na Mlezi, daima walifurahia uwepo na ushiriki wake katika matukio mbalimbali ya watanzania!