Askofu Mkuu Germano Penemote Balozi wa Vatican nchini Pakistan
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amemteuwa Monsinyo Germano Penemote kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Pakistan na kumpandisha hadhi na hivyo kuwa ni Askofu mkuu. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu mteule Germano Penemote alizaliwa tarehe 24 Oktoba 1969 mjini Ondobe nchini Angola. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 6 Desemba 1998 akapewa daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Ondijiva, lililoko nchini Angola.
Askofu mkuu mteule Germano Penemote alijiendeleza na hatimaye kufaulu kujipatia Shahada ya Uzamivu kwenye Sheria na Taratibu za Uendeshaji wa Kesi Mahakamani, “Utroque Iure.” Tarehe 1 Julai 2003 akaanza utume wa diplomasia ya Kanisa na kufanikiwa kutumwa nchini; Benin, Uruguay, Slovakia, Thailand, Hungaria, Perù na Romania. Tarehe 16 Juni 2023, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa ni Balozi wa Vatican nchini Pakistan.