Tafuta

Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima: atokaye kwa Baba na Mwana. Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima: atokaye kwa Baba na Mwana.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Sherehe ya Pentekoste: Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana Mleta Uzima

Huyu ni Roho Mtakatifu amedhihirishwa, ametolewa na kushirikishwa kama Nafsi ya Tatu katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima: atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana: Aliyenena kwa vinywa vya Manabii. Hii ni sehemu ya Kanuni ya Imani kuhusu Roho Mtakatifu Nafsi ya Tatu katika Fumbo la Utatu Mtakatifu: Anatambulika kama: Mwanga, Moto, Upepo, Maji na Njiwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sherehe ya Pentekoste “Πεντηκοστή (Pentēkostē)” inahitimisha kipindi cha Siku 50 za Sherehe ya Pasaka ya Kristo Yesu, kwa kummimina Roho Mtakatifu. Huyu ni Roho Mtakatifu ambaye amedhihirishwa, ametolewa na kushirikishwa kama Nafsi ya Tatu katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima: atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana: Aliyenena kwa vinywa vya Manabii. Hii ni sehemu ya Kanuni ya Imani. Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima ni kipengele kinachofafanua asili ya Nafsi ya Tatu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu anayetenda kazi zake kwa njia ya: Imani, Neno, Sakramenti na Sala za Kanisa. Roho Mtakatifu anawakirimia waamini uzima unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Anawapatia waamini maisha mapya kwa kufisha matendo ya mwili yanayoleta kifo! Atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa na Baba na Mwana ni imani inayoonesha Nafsi ya tatu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kardinali Raniero Cantalamessa, Mhubiri ya Nyumba ya Kipapa anakumbushia kwamba, sehemu hii ya Kanuni ya Imani yaani “Filioque” ndicho chanzo cha mpasuko kati ya Kanisa la Mashariki na Kanisa la Magharibi. Hii ni imani ya Kanisa katika Umungu Mmoja wenye Nafsi tatu. Roho Mtakatifu hata katika kujificha kwake bado anapendwa katika Fumbo zima la Utatu Mtakatifu na kutambulika kwa alama ya: Mwanga, Moto, Upepo, Maji na Njiwa. Roho Mtakatifu alinena kwa vinywa vya Manabii, akazungumza kwa njia ya Yesu na sasa anaendelea kuzungumza kwa njia ya Kanisa. Roho Mtakatifu amezungumza katika Sheria, Manabii na kwenye Agano Jipya. Akamshuhudia Kristo alipokuwa anabatizwa Mtoni Yordani kwa alama ya Njiwa, akawashukia Mitume kwa alama ya ndimi za moto!

Roho Mtakatifu ni mhimili wa uinjilishaji, maisha na utume wa Kanisa.
Roho Mtakatifu ni mhimili wa uinjilishaji, maisha na utume wa Kanisa.

Kardinali Raniero Cantalamessa anasema “Sekwensia ya Roho Mtakatifu” inabeba utajiri mkubwa wa mahusiano kati ya Roho Mtakatifu na mwamini kama “Baba wa maskini, mwanga wa nyoyo za watu na faraja kwa watu.” Sekwensia ya Roho Mtakatifu ni kwa ajili ya kuzima kiu ya mahitaji ya binadamu! Pentekoste ni Sherehe ya waamini walei ndani ya Kanisa. Hawa ni wale waliokusanyika katika Taifa la Mungu na kuwekwa katika Mwili mmoja wa Kristo chini ya kichwa kimoja, wawao wote waitwa, kama viungo vyenye uhai, kutolea nguvu zao zote walizopewa na ufadhili wa Muumbaji na neema ya Mkombozi, ili kulikuza Kanisa na kulitakatifuza daima. Utume wa walei ndio kushiriki utume wa Kanisa lenyewe uletao wokovu; na kuutimiza utume huo ni agizo ambalo wote wanapewa na Mungu mwenyewe kwa njia ya Ubatizo na Kipaimara. Kwa Sakramenti, hasa kwa Ekaristi takatifu, mapendo kwa Mungu na kwa watu, yaliyo roho ya utume wote, yanashirikishwa na kulishwa. Lakini waamini walei wanaitwa kwa namna ya pekee kuonesha uwepo wa Kanisa na utendaji wake mahali pale na katika mazingira yale ambamo lenyewe haliwezi kuwa chumvi ya dunia, isipokuwa kwa njia yao tu. Hivyo kila mwamini mlei, kwa sababu ya karama na vipaji vyenyewe alivyopewa, anakuwa shuhuda na wakati huohuo chombo hai cha maisha na utume wa Kanisa lenyewe “kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo” (Efe 4:7).

Roho Mtakatifu katika ujenzi wa Umoja wa Kanisa
Roho Mtakatifu katika ujenzi wa Umoja wa Kanisa

Ni katika muktadha huu, Askofu Edward Elias Mapunda wa Jimbo Katoliki la Singida ambaye pia ni Mwenyekiti wa Idara ya Utume wa Walei, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC anawatakia kheri na baraka tele katika maisha na utume wao, waamini walei wanapoadhimisha Sherehe ya Pentekoste, Sherehe ya Waamini Walei. Kanisa linawathamini na kuwatazama waamini walei kama amana na hazina kubwa ya Mama Kanisa kutokana na wingi wao. Kanisa linathamini utume wao na michango yao ya: sala, hali na mali katika mchakato wa kulitegemeza Kanisa. Barani Afrika waamini walei waendelee kukita utume wao kwa ajili ya maisha na utume wa familia. Mababa wa Sinodi ya Kwanza ya Maaskofu Katoliki Barani Afrika iliyoadhimishwa kunako mwaka 1994, walikazia umuhimu wa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia na Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, ikawekwa kuwa ni kielelezo na chemchemi ya kiroho ya kila familia ya Kikristo. Mababa wa Sinodi walikazia umuhimu wa wajibu na dhamana ya wanandoa na familia; umuhimu wa jukumu la ndoa kama Sakramenti na kwamba, wanaitwa na kuhamasishwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia katika ulimwengu mamboleo. Kumbe, waamini walipewa wajibu wa kuokoa na kuendeleza tunu msingi za maisha ya ndoa na familia na hivyo kuwa tayari kushirikiana na familia nyingine. Hayati Baba Mtakatifu Benedikto XVI katika Wosia wake wa Kitume “Africae munus” yaani “Dhamana ya Afrika” alikazia familia kwa kusema kwamba, familia ni hekalu la uhai, ni shule ya: Upendo, haki, amani, msamaha na upatanisho. Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu.

Karama za Mashirika mbalimbali ni  zawadi za Roho Mt.
Karama za Mashirika mbalimbali ni zawadi za Roho Mt.

Familia ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanazisaidia familia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Familia ni mahali pa kuinjilisha na kuinjilishwa. Askofu Edward Elias Mapunda anawaalika waamini walei kuwajibika barabara kuhakikisha kwamba, kweli familia inakuwa ni Kanisa la nyumbani, shule ya maadili na utu wema. Kumbe, waamini walei wanapaswa kuchakarika kuanzia kwenye familia hadi kwenye ngazi ya Kitaifa, waoneshe imani yao katika matendo, kwani Mama Kanisa anategemea ushuhuda wao unaomwilishwa katika matendo adili na matakatifu. Waamini walei waendelee kuhamasisha miito mitakatifu kwani wao ni vitalu vya miito ya kipadre, kitawa, ndoa na familia. Kutokana na uhaba wa Makatekista na waalimu wa dini shuleni, waamini walei wanahamasishwa kujitokeza kwa wingi ili kufundisha dini na katekesi. Mashirika na vyama mbali mbali vya kitume viendelee kujichimbia katika imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Waamini walei wasitangetange katika imani yao, kwani Kanisa Katoliki linatosha, kwani lina mafundisho ya kina na kwamba, wawe na uhakika kwamba, Kanisa Katoliki linaweza kuwapeleka mbinguni.

Pentekoste 2023
27 May 2023, 10:06