Tafuta

Askofu mkuu Robert Francis Prevost anasema, dhamana na utume wake ni kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Askofu mkuu Robert Francis Prevost anasema, dhamana na utume wake ni kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa.  (Vatican Media)

Dhamana na Wajibu wa Maaskofu: Kutangaza na Kushuhudia Imani na Ujenzi wa Umoja wa Kanisa

Askofu mkuu Robert Francis Prevost katika mahojiano maalum na Vatican News anazungumzia kuhusu: Dhamana na wajibu wa Maaskofu kwanza kabisa ni kutangaza na kushuhudia uzuri na furaha ya kukutana na hatimaye kumfahamu Kristo Yesu; mchakato wa ujenzi wa umoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro, Askofu na mchakato wa Sinodi na kwamba, Askofu anapaswa kuwa ni mratibu na msimamizi mwaminifu wa rasilimali na mali ya Kanisa kwa ajili ya uinjilishaji!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mkuu Robert Francis Prevost, wa Shirika la Mtakatifu Augustino, O.S.A. alizaliwa tarehe 14 Septemba 1955, Jimbo kuu la Chicago, Illinois, nchini Marekani. Tarehe 29 Agosti 1981 akaweka nadhiri za daima kwenye Shirika la Mtakatifu Augustino, O.S.A. Tarehe 19 Juni 1982 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 14 Septemba 2001 akachaguliwa kuwa ni Mkuu wa Shirika la Mtakatifu Augustino hadi tarehe 4 Septemba 2013. Tarehe 26 Septemba 2015, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Chiclayo, nchini Perù. Tarehe 30 Januari 2023 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Rais wa Baraza la Kipapa kwa Ajili ya Maaskofu na Rais wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini na kumpandisha cheo na hivyo kuwa ni Askofu mkuu. Tarehe 12 Aprili 2023 akasimikwa rasmi kuwa Rais wa Baraza la Kipapa kwa Ajili ya Maaskofu na Rais wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini na hivyo kuchukua nafasi ya Kardinali Marc Armand Ouellet, aliyekuwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu. Askofu mkuu Robert Francis Prevost katika mahojiano maalum na Vatican News anazungumzia kuhusu: Dhamana na wajibu wa Maaskofu kwanza kabisa ni kutangaza na kushuhudia uzuri na furaha ya kukutana na hatimaye kumfahamu Kristo Yesu; mchakato wa ujenzi wa umoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro, Askofu na mchakato wa Sinodi na kwamba, Askofu anapaswa kuwa ni mratibu na msimamizi mwaminifu wa rasilimali na mali ya Kanisa. Askofu mkuu Robert Francis Prevost anasema, dhamana na utume wake ni kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Kwa wakati huu, amepewa dhamana ya kufanya kazi kwa karibu zaidi na Baba Mtakatifu katika Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu. Daima amekuwa tayari kujisadaka kwa ajili ya utume na maisha ya Kanisa, kama ilivyokuwa nchini Perù, kwa kufanya utume wake kwa muda wa miaka 8 kama Askofu na Miaka 20 kama mmisionari.

Askofu mkuu Robert Francis Prevost
Askofu mkuu Robert Francis Prevost

Vigezo muhimu vinavyopaswa kuzingatiwa kwa mtu kuteuliwa kuwa Askofu, kama msimamizi wa mafumbo ya Kanisa na wala si mtawala anayeelemewa na uchu wa mali na madaraka. Askofu anapaswa kuwa ni wakili wa Mungu na kiongozi anayejiaminisha na kutembea mbele ya Mungu; Mkatoliki, mkomavu wa kisaikolojia na maisha ya kiroho. Askofu anapaswa kuwa ni mtu wa Mungu; mtu wa watu na asiyependa makuu. Lakini, kimsingi Askofu anapaswa kuwa mtu mnyenyekevu, mpole na ambaye yuko tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu. Huu ni mwongozo unaoobubujika kutoka katika Neno la Mungu na ambao unapaswa kufuatwa. Askofu anapaswa kuwa ni kielelezo cha ukaribu wa Mungu kwa waja wake: Ukaribu kwa watu wa Mungu, Mapadre na Maaskofu: Uongozi ndani ya Kanisa ni huduma ya huruma na upendo inayosimikwa katika mchakato wa ujenzi wa umoja, ushiriki na utume wa Kanisa, mambo msingi katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Katiba mpya ya Kitume: “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu” inabainisha umuhimu wa kuwashirikisha watu wa Mungu katika uteuzi wa Maaskofu, jambo muhimu sana na dhamana inayotekelezwa sasa na Balozi za Vatican kwenye Makanisa mahalia. Huu ni wajibu wa kuwasikiliza waamini walei na watawa ili kupata maoni yao juu ya Askofu mtarajiwa. Baba Mtakatifu katika utekelezaji wa Katiba hii ya kitume, aliwateuwa wanawake watatu kuwa ni wajumbe wa Baraza la Kipapa la Maaskofu.

Maaskofu ni mashuhuda wa Imani na Kweli za Kiinjili
Maaskofu ni mashuhuda wa Imani na Kweli za Kiinjili

Barua binafsi ya Baba Mtakatifu Francisko “Motu proprio” ijulikanayo kama “Vos estis lux mundi” yaani “Ninyi ni nuru ya ulimwengu”: Sheria mpya kwa ajili ya Kanisa Katoliki dhidi ya nyanyaso za kijinsia.  Katika barua hii, Baba Mtakatifu anabainisha sheria, kanuni na taratibu mpya zinazopaswa kutekelezwa pale kunapojitokeza shutuma za nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Maaskofu mahalia pamoja na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume wanapaswa kuwajibika barabara. Sheria hizi zinawalazimisha wakleri na watawa kutoa taarifa pale kunapokuwepo na shutuma kama hizi. Kila Jimbo linapaswa kuwa na mfumo maalum utakaoiwezesha jamii kutoa taarifa za shutuma za nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha wakleri na watawa kwamba, wao ni nuru ya ulimwengu na kwamba, Kristo Yesu anawaita na kuwataka kuwa waaminifu na mfano mahiri wa tunu msingi za maisha, uadilifu na utakatifu. Hii ni sehemu ya mafundisho mazito yaliyomo kwenye barua binafsi ya Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya mapambano dhidi ya nyanyaso za kijinsia zinazoweza kutendwa na wakleri pamoja na watawa. Nyanyaso za kijinsia ni uhalifu unaosababisha madhara makubwa ya kimwili, kisaokolojia na kiroho si tu kwa waathirika bali hata kwa Jumuiya ya waamini. Viongozi wa Kanisa wanapaswa kuwa mstari wa mbele kupambana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Kwa sasa sheria, kanuni na taratibu zipo, jambo la msingi ni kubadilika kiakili na kifikra.

Sheria zinakataza udhalilishaji wa watoto wadogo
Sheria zinakataza udhalilishaji wa watoto wadogo

Baba Mtakatifu anakazia ujenzi wa Kanisa la Kisinodi kwa kujikita katika: Utamaduni wa kusikiliza, kukutana na kufanya mang’amuzi ya pamoja. Neno la Mungu ni ufunguo wa mang’amuzi na mwanga wa maisha ya kiroho, ili kweli maadhimisho ya Sinodi yaweze kuwa ni sehemu ya mchakato wa toba na wongofu wa ndani. Hili ni tukio la neema na mchakato wa uponyaji unaotekelezwa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Katika kipindi hiki cha maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu, Kristo Yesu anawataka waamini kutomezwa na malimwengu; kuwa wazi kwa kuendelea kusoma alama za nyakati ili kuondokana na tabia ya kutekeleza shughuli za kichungaji kwa mazoea, ili hatimaye, kutambua kile ambacho Mwenyezi Mungu anataka kwa ajili ya Kanisa lake katika nyakati hizi na wapi anataka kulipeleka Kanisa lake. Hakuna maadhimisho ya Sinodi bila ya uwepo na ushiriki mkamilifu wa Askofu mahalia. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kwa njia ya furaha ya Injili, kumwomba Mwenyezi Mungu neema itakayoliwezesha Kanisa kuwa maskini kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Maskini ni walengwa wa kwanza wa Injili
Maskini ni walengwa wa kwanza wa Injili

Maskini wanayo mengi ya kulifundisha Kanisa na waamini wajiruhusu wainjilishwe na maskini. Kimsingi, maskini wanapaswa kupewa upendeleo wa pekee katika Taifa la Mungu. Kristo Yesu, aliyejifanya maskini, akajisadaka bila ya kujibakiza pale Msalabani na hivyo kujitoa kuwa chakula cha kiroho, Ekaristi Takatifu, Mkate ulioshuka kutoka mbinguni, awawezeshe waamini pia kuwa ni Ekaristi safi kwa jirani zao, ili waweze kujimega na kujitoa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Maaskofu wanapaswa kuwa ni wasimamizi na waratibu wazuri wa rasilimali na mali ya Kanisa, ili kuliwezesha Kanisa mahalia kushiriki katika huduma kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Makanisa mahalia yasaidiane kukabiliana na changamoto za hali ngumu ya uchumi, bila kusahau msimamo thabiti wa maisha ya kiroho. Askofu mkuu Robert Francis Prevost anawahimiza Maaskofu kutumia kwa busara mitandao ya kijamii kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji, lengo likiwa ni kuwafikia watu wengi zaidi. Ili kufikia lengo hili, kuna haja kwa Maaskofu kuhakikisha kwamba, wanajinoa kikamilifu, wawe na busara ya kupima kile wanachotaka kurusha kwenye mitandao ya kijamii. Matumizi ya mitandao ya kijamii ni fursa ya uinjilishaji mpya lakini pia kuna hatari zake. Mawasiliano haya yanaweza kuleta hatari kwa ushirika wa Kanisa, ndiyo maana kuna haja ya kuwa na busara katika matumizi ya mitandao ya kijamii.

Askofu mkuu Prevost

 

04 May 2023, 16:40