Tafuta

Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Taasisi ya Kipapa ya Maisha, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, ameshiriki katika Kongamano la 17 la Dunia Kuhusu Afya ya Jamii, mjini Roma. Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Taasisi ya Kipapa ya Maisha, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, ameshiriki katika Kongamano la 17 la Dunia Kuhusu Afya ya Jamii, mjini Roma.  (AFP or licensors)

Maisha, Afya Bora na Kanuni Maadili Ni Mambo Msingi Kwa Wote

Katika hotuba yake amekazia kuhusu hitaji la haki zaidi na usawa katika upatikanaji wa dawa na huduma bora ya afya. Maisha, Afya Bora na Kanuni Maadili ni mambo msingi kwa kila mtu, hasa wakati huu wa kipeo cha changamoto ya maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ambayo yamepelekea pia kipeo cha kisiasa kinachojikita katika masuala ya ikolojia, nishati, pamoja na vita na madhara yake: Umuhimu wa maisha, ujuzi na maarifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Taasisi ya Kipapa ya Maisha, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, ameshiriki katika Kongamano la 17 la Dunia Kuhusu Afya ya Jamii, mjini Roma, tarehe 3 Mei 2023. Katika hotuba yake amekazia kuhusu hitaji la haki zaidi na usawa katika upatikanaji wa dawa na huduma bora ya afya. Maisha, Afya Bora na Kanuni Maadili ni mambo msingi kwa kila mtu, hasa wakati huu wa kipeo cha changamoto ya maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ambayo yamepelekea pia kipeo cha kisiasa kinachojikita katika masuala ya ikolojia, nishati, pamoja na vita na madhara yake: Ni katika muktadha huu, afya ya umma inapaswa kupewa msukumo wa pekee kwa umuhimu wa maisha ya binadamu; Pili ni ujuzi na maarifa kuhusu baiyolojia, usafi, magonjwa pamoja na umuhimu wa kuwa na takwimu sahihi bila kusahau masuala ya kiuchumi, kijamii, kitamaduni na kiikolojia.

Hakuna usawa katika huduma za afya
Hakuna usawa katika huduma za afya

Tatu ni kwamba kuna uhusiano wa karibu kati ya afya na magonjwa, hali inayotengenezwa na kuzalishwa kijamii, kutokana na mtindo na hali ya maisha! Kumbe, wajibu wa walimwengu si tu katika kudhibiti na kutibu magonjwa, lakini pia ni kwa jinsi gani afya inalindwa na kudumishwa. Yote haya ni matokeo ya hali halisi ya kijamii na mazingira ambamo jamii mbalimbali za binadamu zinaishi, kiasi kwamba, zinachangia katika afya ya binadamu na maisha katika ujumla wake. Ubora wa huduma ya afya na hali ya maisha zinatofautiana sana kutoka nchi moja hadi nyingine. Hii inatokana na kiwango cha mshahara, elimu na ujirani, ingawa maisha na afya ni mambo msingi kwa kila binadamu, lakini, licha ya matamko mbalimbali bado maisha na huduma za afya hazina usawa, changamoto ni kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inarekebisha hali hii, kwa kuwajibika zaidi, ili haki iweze kutendeka.

Ushirikiano na mshikamano ni muhimu katika huduma ya tiba
Ushirikiano na mshikamano ni muhimu katika huduma ya tiba

Kumbe, kuna haja ya kuwekeza zaidi katika ushirikiano wa Kimataifa kama ilivyojitokeza katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Vinginevyo, viwanda vyenye hati miliki za utengenezaji na usambazaji wa dawa vitaendelea kunufaika na hivyo kusababisha ukosefu wa haki na usawa hata katika mapambano dhidi ya magonjwa ya mlipuko. Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Taasisi ya Kipapa ya Maisha amehitimisha hotuba yake kwa kukazia kwamba, Kanisa linapenda kutangaza Injili ya matumaini kwa wagonjwa. Linaendelea kutoa shukrani kwa wadau mbalimbali wanaochakarika usiku na mchana katika ujenzi wa ulimwengu unaosimikwa katika usawa na afya tele, dhidi ya magonjwa na vita! Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya maisha na matumaini ya maisha bora zaidi.

Askofu mkuu Paglia

 

04 May 2023, 14:56